dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, April 2, 2016

Magufuli ajinyima mshahara wa JK


Wananchi wamempongeza Rais John Magufuli kwa kuweka wazi mshahara wake wa Sh. Milioni 9.5 kwa mwezi huku wakieleza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuendeleza vita dhidi ya wale wanaojilipa mishahara mikubwa.
 
Julai mwaka jana, mtandao wa Africa Review uliwahi kuandika kuwa Rais Jakaya Kikwete, wakati huo akiwa madarakani, alikuwa akishika nafasi ya tano miongoni mwa marais 38 wa Afrika kwa kulipwa mshahara mnono wa dola za Marekani 16,000 (sawa na Sh. milioni 34 wakati huo).
 
Ingawa taarifa hizo zilikanushwa haraka na Ikulu baada ya gazeti moja la kila siku kuzinukuu, Kurugenzi ya Masiliano ya JK ilishindwa kuweka wazi mshahara halisi wa Rais wakati huo hivyo kuzua hofu kuwa pengine ni chini kidogo tu ya hapo.Katika hali isiyo ya kawaida, jana Rais Magufuli alitaja mshahara wake kuwa ni Sh. milioni 9.5, huku akiahidi kuwa atatoa nyaraka zinazoonyesha mshahara huo (salalry slip) punde akitoka mapumzikoni  wilayani Chato mkoani Geita.
Juzi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zito Kabwe (ACT-Wazalendo) walimpa Rais Magufuli changamoto ya kutaja mshahara wake.
 
Changamoto hiyo ilifuatia kauli ya Rais Magufuli ya katikati ya wiki ambapo alisema anakusudia kufyeka mishahara ya wakuu wa taasisi za umma kutoka karibu Sh. milioni 40 kwa mwezi mpaka Sh. milioni 15 tu. 
 
Magufuli alifichua siri hiyo jana kwenye kipindi cha uchambuzi wa magazeti cha 360 kinachorushwa hewani na tevevisheni moja ya jijini, baada ya watangazaji kusoma habari iliyoandikwa na gazeti la Nipashe kuwa Zitto na Lissu wamemtaka Rais ataje mshahara wake ili ukatwe kodi.
 
Wakiwa katika mjadala huo, walipokea taarifa kuwa Rais kawasikia na katuma taarifa ofisi za Clouds kuwaeleza mshahara wake kuwa ni Sh. mililoni 9.5 na kwamba atatoa nyaraka za malipo hayo atakaporejea Dar es Salaam.
 
Hatua ya Rais Magufuli kutangaza mshahara wake ni ya kwanza Afrika hivyo kumfanya kuwa rais pekee barani aliyethubutu kuchukua hatua hiyo.
 
Akiwa Chato Magufuli alisema kuna wakurugenzi ambao wanajilipa mishahara inayofikia Sh. milioni 40 kwa mwezi wakati watumishi wengine wa umma wakiambulia mshahara ambao hauwezi kuwafikisha hata nusu mwezi.
 
Magufuli amechukua uamuzi mgumu wa kujilipa mshahara mdogo kuliko hata wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wanaolipwa mshahara wa Sh. milioni 11.9 kwa mwezi.
 
MAONI YA WANANCHI
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Lissu alisema ameshangazwa kusikia Rais analipwa mshahara mdogo kulinganishwa na ule wanaopata wabunge wa Sh. milioni 11.9.
 
“Rais atueleze hiyo milioni 9.5 ni mshahara baada ya makato au ni mshahara wake bila makato (basic salary) maana hii ni taarifa kali ya mwaka kama Rais analipwa mshahara mdogo zaidi kuliko sisi wabunge wake,” alisema Lissu
“Bado nina wasiwasi katika hilo kama mshahara huo ni baada ya makato maana haijawahi kutokea wabunge wa Tanzania kupokea mshahara mkubwa kumzidi Rais.” 
Lissu ambaye pia ni Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alisema mshahara wa wabunge baada ya makato ya kodi na mikopo huwa Sh. milioni 3.6.
 
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya siasa, alisema kuwa Rais ameamua kuweka wazi mshahara wake ili kuwajibu wale wote ambao wanafikiri analipwa mshahara mkubwa.
 
“Amefanya hivyo ili kuonyesha yupo makini kukabiliana na wale  wanaojilipa mishahara mkubwa,” alisema
 
Dk. Bana alisema kitendo hicho kinaonyesha jinsi Rais alivyo muwazi na kwamba uwazi huo unatakiwa mtu alipwe kwa mujibu wa utendaji wake wa kazi na siyo mkurugenzi kujilipa mshahara mkubwa wakati kazi zinafanywa na watendaji wake.
Alisema hilo ni funzo kwa wakurugenzi watendaji ambao wanajilipa mishahara mikubwa bila sababu na kuwataka wakuu wote wa mashirika ya umme kuweka wazi mishahara yao.
 
Dk. Ally Bashiru wa UDSM pia alisema kuna watu wanajilipa mishahara zaidi ya Rais ila alionya kuwa wasihukumiwe hadi watakapojulikana kwanza ni kazi gani wanazofanya.
 
“Kama kazi hiyo inaendana na fedha hizo wanazopewa ni sawa, lakini kama hawafanyi kazi na wanapokea mishahara mikubwa siyo sahihi,” alisema Dk. Bashiru.
 
Aidha, alisema Rais anatakiwa kufanya marekebisho ya sera ili kuleta usawa, kwani bado kuna mgongano wa kimaslahi kati ya mashirika ya umma na binafsi.
 
“Kudhibiti mshahara wa mashirika ya umma najua ni vigumu Rais kupangilia suala hilo japo bado kuna  mgongano wa kimaslahi,” alisema Dk. Bashiru. 
 
Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, alisema Rais amefanya uamuzi mzuri wa kuweka wazi mshahara wake.
 
“Lakini tungepaswa kufahamu mshahara wake pamoja na marupurupu yake japo bado sijaamini kama Rais analipwa mshahara mdogo kama huo maana aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mshara wake unamzidi Rais,” alisema Profesa Ngowi.
 
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Richard Mbunda, alisema kutajwa kwa mshahara wa Rais ni tafsiri ya kuendeleza vita dhidi ya wanaojilipa mshahara mkubwa.
Alisema lengo lake ni kuwepo na usawa wa mishahara katika taasisi za seriklai ili kusiwepo na utofauri mkubwa kata ya mfanyakazi.
 
Alisema kwa mtazamo wa pili ni kwamba siku zote mshahara wa Rais unakuwa ni siri ili kuzuia majadiliano hususani katika kipindi hiki ambacho watu wanaongea kwa uwazi.
 
“Suala hili litaleta mijadala mingi ambayo siyo vizuri... ni vizuri mshahara wa Rais iwe ni siri kuliko kuwa wazi,” alisema Mbunda
 
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, alisema anachofahamu ni kwamba hakuna mtumishi wa Ikulu anayelipwa Sh. milioni 9.5 hivyo kama Rais atakuwa ametajia kiasi hicho itakuwa sahihi.
“Kwa kuwa amewaahidi kuwaletea salary slip basi tusubiri,” alisema Msigwa.
 
WAKUU WENYE MISHAHARA KUFURU
Waziri Mkuu wa Singapore, Lee Hsien Loong anatajwa kuwafunika viongozi wenzake wote duniani katika jumla ya mshahara kwa mwaka, akimpita mara tatu mshindani wake wa karibu.
 
Mshahara wa Lee wa dola za Marekani milioni 2.32 kwa mwaka (sawa na Sh. milioni 425 kwa mwezi) unamfanya aongoze orodha ya 'top 10' ya viongozi 10 wa nchi wanaolipwa vizuri zaidi, kwa mujibu wa mtandao wa kompyuta wa habari za fedha wa 24/7WallSt.
 
Orodha kamili ni:
1 — Lee Hsien Loong, Singapore, $2.32 million
2 — Leung Chun-ying, Hong Kong, $760,000
3 — Johann N. Schneider-Ammann, Uswisi, $606,000
4 — Barack Obama, Marekani, $527,000
5 — Malcolm Turnbull, Australia, $522,000
6 — Werner Faymann, Austria, $452,000
7 — Xavier Bettel, Luxembourg, $336,000
8 — Justin Trudeau, Canada, $333,000
9 — Angela Merkel, Ujerumani, $322,000
10 — Charles Michel, Ubelgiji, $315,000.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment