dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, April 3, 2016

Wahisani kutimka si ufumbuzi gogoro la Zanzibar

Image result for mcc millennium


Wakati Rais wa Zanzibar Ali Mohamed Shein, anaendelea kupanga safu ya viongozi na watendaji wa serikali yake, baadhi ya wahisani wametangaza kuwa ‘no’ misaada kwa Zanzibar. Hawa ni Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani.

Uamuzi wa kusitisha misaada si mgeni katika siasa za Zanzibar, kwani nchi wahisani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1992 zimekuwa zikifanya hivyo.

Vitisho vya wahisani kwa Zanzibar na Tanzania vilianza mwaka 1995 kufuatia mgogoro mkubwa wa kisiasa baina ya CCM na CUF mara baada ya uchaguzi mkuu visiwani humo ukidaiwa haukuwa wa huru na haki.

Wahisani hao walisitisha kufadhili miradi ya maendeleo kama usambazaji huduma ya umeme vijijini, chanjo kwa watoto na wajawazito, ujenzi wa bandari ya Malindi na zaidi ya hapo waliiteteresha bajeti ya serikali.

Watu wenye uwezo walilazimika kusafirisha watoto hadi kliniki za Bara ili kupata chanjo na wale wanyoge waliendelea kubakia Zanzibar na watoto wao kuiishi kwa huruma ya Mungu. Kadhalika watumishi wa serikali waliathirika kwa kukosa mishahara kwa wakati baada ya bajeti ya serikali kutetereka kufuatia vikwazo vya wahisani hao.

Hata hivyo,  serikali ya Rais mstaafu wa Zanzibar Salmin Amour Juma, ilihakikisha huduma muhimu za matibabu, maji na elimu ziliendelea kupatikana baada ya serikali kuamua kubana matumizi kwa miaka mitano.

Uamuzi wa nchi wahisani kama EU kusitisha misaada kwa Zanzibar uliwaumiza wananchi wote bila ya kujali itikadi ya chama , dini rangi au asili yake kwa wakazi wote wa Unguja na Pemba.

Hata hivyo, ni jambo la kujiuliza watu wanaofurahia wahisani kusitisha misaada yao Zanzibar wanashangakua kwa faida ya nani kama wananchi ndiyo wanaoteseka na kuumia badala ya viongozi?

Wakati umefika kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kujifunga mkanda kwa kupunguza matumizi ya kianasa zikiwamo safari za nje , kuziba mianya ya ufisadi, pamoja na kuunda Baraza dogo la Mawaziri linlofanana na uwezo wa serikali kiuchumi.

Akisimamia azimio la Arusha kwa vitendo mwaka 1967 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema “Ni ujinga kutegemea pesa kama msingi wa maendeleo wakati tunafahamu vyema kwa nchi yetu ni masikini. Lakini, ni ujinga zaidi kufikiria kwamba tutajikomboa kutoka kwenye umasikini wetu kwa kutegemea misaada ya kigeni badala ya juhudi zetu wenyewe”.

Maneno ya Mwalimu ni njia muafaka ya kupita viongozi wetu wa kitaifa Bara na Zanzibar katika kukabiliana na vikwazo vya wahisani kwa kuongeza uwajibikaji na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma.

Ni jambo la kusikitisha kuona wanafunzi wanasoma wakiwa wamekaa chini kutokana na ukosefu wa madawati, lakini SMZ inaweza kununua magari ya kifahari kama VX, V8 kwa gharama kubwa wakati uchumni wake mdogo na gari za kawaida zinatosha kutoa huduma kwa viongozi na watendaji.

Hata hivyo, ahadi ya Rais Shein ya kutaka kuunda serikali ambayo itawajibika kwa wananchi kwa kasi kubwa ya mabadiliko kama Serikali ya Rais John Magufuli, imefufua matumaini makubwa kwa Wazanzibari.

Suala la uwajibikaji pamoja na kupambana na ufisadi na rushwa ni muhimu katika kujenga uchumi wa kujitegemea hasa katika kipindi cha mpito cha vikwazo vya wahisani Visiwani Zanzibar.

Lakini, hatua ya wahisani kuzuia misaada kwa Zanzibar si ufumbuzi wa kumaliza mgogoro wa uchaguzi kwa sababu wananchi wanyonge ndiyo watakaoumia badala ya viongozi na wanasiasa.

Nchi wahisani zinatakiwa kutafuta chimbuko la matatizo ya kisiasa ya Zanzibar na kusadia kupatikana kwa maelewano badala ya kutumia nguvu za kiuchumi kufikia suluhu ya Zanzibar.

Uchaguzi mkuu wa marudio umefanyika na Rais anaendelea kupanga serikali yake bila ya wapinzani wakuu CUF kuwamo baada ya kujiondoa katika uchaguzi, jambo ambalo linaongeza ufa na mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar.

Hata hivyo, hakuna atakayejenga Zanzibar zaidi ya Wazanzibari wenyewe lakini uamuzi wa wahisani wa kusitisha misaada utawaumiza wananchi wanyoge na kurudisha nyuma maendeleo ya Zanzibar yaliyoanza kuonekana tangu kufikiwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzai mkuu wa mwaka 2010.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment