dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, August 21, 2016

Lishe Bora kwa Maisha Yote!

Inajulikana kabisa kuwa nyumba imara hujengwa kwa mchanganyiko wa vitu vingi. Nyumba hii huonekana nzuri na yenye kupendeza wakati wote na pia haimomonyoki kirahisi wakati wa mvua au upepo mkali. Nyumba imara hujengwa kwa mchanganyiko kama wa cementi, mchanga, kokoto, nondo n.k. mchanganyiko huu huwa katika kiwango sahihi, hii ni kwamba kuna kiasi au uwiano sahihi katika mchanganyiko huu. Kimojawapo kati ya hivi kikipelea au kuwa katika kiasi pungufu basi nyumba haitakuwa imara, vilevile kimojawapo kikizidi basi nyumba haitakuwa imara pia. Hivyo nyumba ili iwe imara ni lazima mchanganyiko huu uwe katika uwiano ulio sahihi.

Mpaka hapo swali linakujia, je mwili wako unajengwa na nini? je kuna uhitaji wa uwiano sahihi?
Mwili wa binadamu hujengwa kwa chakula. Chakula hicho ni lazima kiwe chakula bora au mlo kamili. Mlo kamili unajumuisha makundi matano ya vyakula ambayo ni: nafaka, mizizi na ndizi, kundi la pili: vyakula vyenye jamii ya kunde na vyenye asili ya wanyama, kundi la tatu: mbogamboga, kundi la nne: matunda, kundi la tano: mafuta na sukari.

Mwili unahitaji chakula chenye mchanganyiko wa makundi haya ya chakula ili kuwa na afya bora na iliyo imara kama inavyolinganishwa na nyumba imara. Inajulikana kuwa mchanga ukizidi katika tofali nyumba itamomonyoka nakuanguka au cementi ikipungua pia nyumba itamomonyoka na kuanguka. Hii ni sawa na ulaji kwa binadamu, chakula kikiwa hakina au kina kiwango kidogo cha baadhi ya makundi ya chakula yaliyotajwa hapo juu lazima mwili utakuwa dhoofu, hata makuzi yake hayatakuwa mazuri. Magonjwa yatokanayo na utapiamlo ndio chanzo kikuu cha mwili kuwa na afya mbaya. utapia mlo hutokana na lishe duni au lishe iliyozidi.

Lishe duni ni hali ya mwili kukosa baadhi ya virutubishi vinavyohitajika mwilini, kama vile protini, wanga, mafuta, vitamini na madini. Mwili ukikosa baadhi ya virutubishi hivi hushindwa kufanya kazi zake za kimebotali vizuri na kusababisha madhara mengine mengi. Vilevile mwili ukiwa na lishe iliyozidi husababisha madhara makubwa hii inatokana na kubadilika kwa baadhi ya kazi za seli na ogani mbalimbali mwilini.

Magonjwa ya utapia mlo ni kama vile: kwashakoo, marasmasi, marasmasi na kwashakoo, upungufu wa damu (Iron Deficiency Anaemia), tatizo la ukosefu wa vitamini C, tatizo la Ukosefu wa vitamini A, tatizo la ukosefu wa madini Joto, na magonjwa yatokanayo na lishe iliyozidi ni kama kisukari, presha, magonjwa ya moyo ambayo ndio tatizo kubwa linalowakumba hasa matajiri wanaojikita zaidi katika vyakula vyenye mafuta mengi na sukari.

Kundi la chakula, chanzo chake, virutubishi vyake, na kazi yake mwilini

1. Nafaka, Mizizi na Ndizi


mchele, mahindi, mtama, ulezi, ngano, uwele, viazi vikuu, viazi vitamu, mihogo, magimbi, viazi mviringo, na Ndizi
Virutubishi: Wanga
Huupatia mwili nguvu za kuweza kufanya kazi

2.Vyakula vya aina ya mikunde na vyenye asili ya wanyama


Maharage, kunde, mbaazi, soya, karanga,njegere, njugu mawe,dengu, choroko, asili ya wanyama ni: nyama, mayai, samaki, dagaa, kumbikumbi, senene, maziwa na nzige.
Virutubishi: Protini
Hujenga mwili. Huwezesha mwili kutengeneza seli nyingine.

3.Mboga-mboga


mchicha, majani ya kunde, majani ya maboga, kisamvu, matembele, spinachi, mgagani, mlenda, mnavu, mchunga, karoti, pilipili hoho, nyanya chungu, biringanya, bamia, kabichi, figiri, sukuma wiki na chainizi.
Virutubishi: Vitamini na Madini
Huupa mwili kinga imara dhidi ya maradhi mbalimbali.

4.Matunda


mapera, maembe, machungwa, papai, nanasi, zambarau, dhabibu, mapesheni, machenza, ubuyu, ukwaju, limao
Virutubishi: vitamini na madini
Huupa mwili kinga dhidi ya maradhi.
Husaidia kwa baadhi ya virutubishi kutumika kwa ufasaha zaidi mwilini.

5.Mafuta na Sukari


mafuta ya kupikia, ufuta, karanga, mbegu za alizeti, siagi, samli, nyama yenye mafuta, sukari ni: asali, miwa, vyakula vinavyotengenezwa kwa sukari nyingi kama jamu, keki, n.k
virutubishi: mafuta
Huupa mwili nguvu.
Husaidia ufyonzwaji wa vitamini A,D,E na K.

Maji???????
Maji hayakuwekwa kwenye kundi lolote la chakula kwa sababu hayana virutubishi. Ni muhimu kunywa maji safi na salama kwani yanarahisisha umeng'enyaji wa chakula, kusafirisha virutubishi na kutoa uchafu ambao hutengenezwa mwilini wakati mwili unafanya kazi zake. Asilimia kubwa ya mwili ni maji hivyo ni vyema kunywa maji mara kwa mara ili kuwa na afya bora.

Kumbuka:
ni vema kula vyakula vyenye mchanganyiko wa kila kundi la chakula ili mwili uwe na afya nzuri, na kutopatwa na maradhi mara kwa mara, pia kunywa maji safi na salama wakati wote unapohitaji.

/Muungwana.

No comments :

Post a Comment