Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar Jaji George Kazi Kulia akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi namna Mahakama ya Watoto itakavyofanya kazi alipofika Mahonda kukagua ujenzi wa Mahakama ya Watoto.
Nyuma ya Balozi Seif Ali Iddi ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Ndugu Issa Juma.
Mhandisi Mkuu wa Jeshi la Polisi Mrakibu wa Polisi Paschal Macorwa akimpatia maelezo Balozi Seif hatua iliyofikia ya Ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Watoto Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Balozi Seif kulia akiwa pamoja na Mhandisi Mkuu wa Jeshi la Polisi Mrakibu wa Polisi Paschal Macorwa wakifurahia hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Mahakama ya Watoto Mahonda alipofika kukagua maendeleo ya ujenzi wake.
Mkuu wa Kituo cha Afya Mahonda Dr. Ramadhan Makame Khamis kushoto akimueleza Balozi Seif hatua iliyofikiwa ya matayarisho kwa ajili ya Kambi ya Uchunguzi wa Afya kwa Wananchi wa Wilaya ya Kaskazini “B” inayotarajiwa kufanyika Kituoni hapo Tarehe 3 na 4 Mwezi ujao.
Balozi Seif kati kati akishauri baadhi ya hatua zinazopaswa kukamilishwa kabla ya kuanza kwa Kambi ya uchunguzi wa Afya hapo Kituo cha Afya Mahonda mnamo Tarehe 3 na 4 Mwezi ujao.(Picha na – OMPR - ZNZ.)
Na Othman Khamis OMPR.
Mrajis wa Mahkama Kuu ya Zanzibar Jaji George Kazi alisema Mtoto anapaswa kuandaliwa mazingira maalum yatakayomuwezesha kutoa ushahidi ulio huru endapo atafanyiwa vitendo vya udhalilishaji au kujitetea kama amefanya makosa ya jinai akiwa chini ya Umri wa miaka 18.
Alisema Serikali imeanzisha Sheria ya Mtoto nambari 6 ya Mwaka 2011 kwa madhumuni ya kuipa mamlaka Mahakama kusikiliza na kuamua makosa ya Jinai dhidi ya Mtoto kwa kosa lolote linaloshukiwa kutendwa kabla ya Mtoto hajafikia umri huo isipokuwa makosa ya Uhaini, Kuua na Kubaka.