Na Chris Alan
KWA wanaoufahamu mchezo wa soka, wanajua kuna sheria 17 zinazoutawala. Moja ni kupata ‘free kick’ pale mchezaji anapomchezea mwenzake rafu. Refa hupuliza filimbi na kuashiria faulu. Mpira unawekwa mahali pa kupigwa kiki kuelekea goli la mtenda kosa. Soka lina utamu na karaha zake.
Katika siasa pia kuna faulu zinazoweza kumpa mtu free kiki. Hutafutwa kwa udi na uvumba ili kutoa nafuu na faida ya kisiasa kwa anayepiga kiki.
Umma unashuhudia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akijitahidi kila uchao kusaka free kiki. Amejitahidi mno. Na kwa bahati mbaya wale walioko juu yake ama kwa kujua au kwa kutokusoma vema mbinu zake, wamejiachia.
Makonda amebobea sasa katika kusaka free kiki. Nikumbushe historia; yu kijana mchanga katika siasa, lakini nani asiyemkumbuka akiwa pale makao makuu ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), alivyomporomoshea kauli chafu Edward Lowassa? Alimuita mwizi, fisadi na muovu, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015.
KWA wanaoufahamu mchezo wa soka, wanajua kuna sheria 17 zinazoutawala. Moja ni kupata ‘free kick’ pale mchezaji anapomchezea mwenzake rafu. Refa hupuliza filimbi na kuashiria faulu. Mpira unawekwa mahali pa kupigwa kiki kuelekea goli la mtenda kosa. Soka lina utamu na karaha zake.
Katika siasa pia kuna faulu zinazoweza kumpa mtu free kiki. Hutafutwa kwa udi na uvumba ili kutoa nafuu na faida ya kisiasa kwa anayepiga kiki.
Umma unashuhudia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akijitahidi kila uchao kusaka free kiki. Amejitahidi mno. Na kwa bahati mbaya wale walioko juu yake ama kwa kujua au kwa kutokusoma vema mbinu zake, wamejiachia.
Makonda amebobea sasa katika kusaka free kiki. Nikumbushe historia; yu kijana mchanga katika siasa, lakini nani asiyemkumbuka akiwa pale makao makuu ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), alivyomporomoshea kauli chafu Edward Lowassa? Alimuita mwizi, fisadi na muovu, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015.
Hata baada ya kumtusi Lowassa, hakuna kiongozi aliyethubutu kumkemea. Si kutoka CCM wala serikalini. Waliomtuma walimshangilia.
Aliendeleza kiburi hadi kudiriki kutafuta wahuni na kushirikiana nao kumshambulia Jaji Joseph Warioba, akiwa mwenyekiti wa Tume ya Katiba, aliyekuwa mmoja wa wazungumzaji kwenye mdahalo wa kitaifa kuhusu katiba mpya. Nani asiyejua kuwa wanausalama ndio walimnusuru Jaji Warioba asidhurike kutokana na vurugu zile kwenye mdahalo uliofanyikia ukumbi wa Ubungo Plaza ndani ya Blue Pearl Hotel?
Umma ulipigwa bumbuwazi yenye ganzi kusikia katika kipindi hichohicho Makonda ameteuliwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni. Likazuka swali, kwa kigezo kipi? Cha kudhalilisha viongozi wakubwa Lowassa na Jaji Warioba?
Au ulikuwa ni mkakati wa kuanza kujenga aina mpya ya viongozi katika CCM, kuingiza aina ya watu wanaodhalilisha viongozi, watu wasiokuwa na maadili, watumwao kusema lolote hata kutusi wakubwa?
Hadi Rais John Magufuli anaingia madarakani, hakuna anayejua fika sababu hasa za Makonda kuteuliwa. Vile kupandishwa kuwa mkuu wa mkoa, ndio ikashtua zaidi. Kwani Makonda sera ya uteuzi nchini imebadilika kutoka mtu kuwa muadilifu?
Tangu awe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amekuwa bingwa wa kusaka free kiki. Ameumiza watu wengi. Ameleta sokomoko nyingi mkoani, ikiwemo kuchonganisha hata viongozi wa vyombo vya usalama na mamlaka za juu za utawala.
Novemba mwaka jana, wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anazindua mradi wa Kuboresha Miundombinu ya Umeme katika Jiji, Makonda aliwatuhumu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Kamishna Simon Sirro na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Suzan Kaganda, kuwa “huenda wamehongwa na wafanyabiashara wa shisha ndiyo maana wanalegalega kusimamia kudhibiti biashara hiyo na uvutaji wake.”
Alikwenda mbali zaidi, akadai wafanyabiashara hao walikuwa wanataka kumhonga Sh. 50 milioni kila wiki ili anyamazie uovu wao; lakini aliwakatalia. Anaamini wakubwa wenzake, Sirro na Kaganda, “wamechukua.”
Busara ya Waziri Mkuu Majaliwa ikasukuma amgeuzie kibao. Akamwambia Makonda anawajibu wa kushughulikia suala hilo, na akishindwa amshughulikie. Majaliwa kwa kujua ametegwa, alikataa kumpa Makonda free kiki.
Ni Makonda huyuhuyu aliagiza kuhakikiwa kwa silaha zote mkoani akiamini kazi hiyo ingesaidia kupunguza ujambazi. Ni jambo jema kuhakiki silaha, lakini itakumbukwa kazi hiyo ilifanywa mwaka 2014, kila silaha ilipigwa chapa ya namba mpya. Kila mwenye silaha alitii. Palitumika muda na nguvukazi kubwa.
Baada ya tangazo la Makonda, Rais Magufuli alionekana akihakiki silaha zake Ikulu. Baadaye wamiliki silaha Dar waliendelea na kazi hiyo iliyokuwa usumbufu tu kurudia kitu kilichokwishafanywa muda mfupi uliopita. Mwishowe nchi nzima ilitakiwa kuhakiki tena silaha.
Baada ya kusaka kiki kila wakati na akiungwa mkono na wakubwa, sasa Makonda ameibuka na staili ya ajabu ya kudhibiti dawa za kulevya. Anataja wasanii kwenye vyombo vya habari akiwatuhumu kujihusisha na dawa hizo. Wengi wameitwa na kuripoti polisi. Baadhi wamesomewa mashitaka mahakamani na kudhaminiwa.
Kati yao, ni msanii mmoja tu amethibitika kukutwa nazo. Ni msokoto mmoja wa bangi na karatasi za kusokotea. Msokoto mmoja! Wengine ni watumiaji waliokuwa kwenye matibabu ya kuachana na utumiaji. Makonda anatafuta kiki hata kwa hawa waathirika.
Baada ya kiki ya dawa za kulevya kutopata kasi aliyotaka, akaibuka tena na orodha ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya aliyodai ameifanyia uchunguzi. Ametaja majina ya watu wakubwa – wanasiasa, wafanyabiashara na hata viongozi wa dini.
Nimeiona orodha yake ameiandika kwa mkono, tena harakaraka. Majina mengine yamekosewa, mengi ni jina moja moja, mengine majina ya utani. Kwake amepata kiki ya kutokea. Mpambanaji wa dawa za kulevya amewapiku polisi, kikosi maalumu cha kupambana na dawa za kulevya. Anawajua wabwia unga, wasafirishaji, wauzaji lakini pia anajua mbinu za kusafirisha.
Pamoja na kujitapa kuyajua yote hayo, hakuwa na subira ya kutega mitego ili akamate wahusika wakiwa kazini. Kaibuka na kuwatangaza watu. Kwa ushahidi gani? Eti wakaseme polisi na kusaida taarifa. Free kiki ya kulazimisha.
Duniani hakuna taifa linalotumia nguvu kubwa kudhibiti dawa za kulevya kama Marekani, nchi inayopakana na mataifa ambako tatizo hilo linatajika hasa kwa miaka mingi. Mtandao wa Drug War Facts unasema kwa mwaka huu wa 2017 serikali ya Marekani imeomba kutumia Dola 31.07 bilioni kupambana, mwaka 2016 zilitumika Dola 30.6 bilioni.
Ni fedha nyingi kwelikweli, lakini pamoja na vifaa vya kisiasa, askari waliobobea na utashi hasa wa kuangamiza biashara hiyo, bado Marekani inatajwa kama nchi iliyofurtu ada kwa tatizo hilo. Marekani ilianza zamani, bado inaendelea.
Tanzania, mtu anayeitwa Makonda akijulikana alivyo na historia inayoyumbayumba kuhusu uadilifu kitabia, asiye na rekodi ya mfano kama mtendaji mwema, anataka kutafutia kiki janga hili. Hana rasilimali watu, vifaa na hata fedha za kudhibiti tatizo. Tegemeo lake ni kutaja majina ya watu huku akitarajia matangazo ya mteremko ya vyombo vya habari. Kudhibiti janga kwa kusababisha janga!
Hakika Makonda safari hii ametumbukiza miguu kwenye mabuti makubwa, mazito yasiyoendana na saizi ya vidole vyake. Badala yake, ninachokiona, amevuruga kazi ambayo vyombo vilivyofunzwa na kufuzu vingeliifanya vizuri kwa kampeni ya kitaifa; bali pia ametengeneza mgogoro na anaowatuhumu, maana mtuhumiwa aliyemtangaza bombani akishathibitika hahusiki, atamsafisha vipi? Utafutaji free kiki utamponza tu.
No comments :
Post a Comment