Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, March 25, 2017

Kizungumkuti cha Magufuli!

Image result for john pombe magufuli
/Raia Mwema
KWA mara nyingine, Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa mtata wa Dar es Salaam, amekwepa panga la Rais John Magufuli, ambalo limeangukia watumishi na viongozi wa serikali wengi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Hata hivyo, hatua hiyo imezua maswali kuhusu namna Rais Magufuli anavyowatenda tofauti wateule wake; ikizingatiwa kwamba amewahi kuchukua hatua kali kwa wengine kwa makosa madogo kuliko ambayo Makonda ametuhumiwa nayo hadi sasa.

Juzi Jumatatu, Rais Magufuli alizungumza hadharani jijini Dar es Salaam na kumkinga Makonda dhidi ya shutuma zilizomuandama kutokana na kitendo chake cha kuvamia akiwa na askari wenye silaha kituo cha redio na televisheni cha Clouds FM.

Wakati wadau wa sekta ya habari na watu wengine wakitarajia Rais achukue hatua dhidi ya tukio hilo lililozua mijadala katika mitandao ya kijamii tangu Jumapili iliyopita, Magufuli alimtetea Makonda hadharani; kinyume na anavyojulikana kwa kuchukua hatua haraka.
“ Makonda endelea na kazi. Nasema hivi, chapa kazi. Watu wa Dar es Salaam tumejielekeza sana kwenye udaku ambao hausaidii maendeleo. Udaku ambao haumalizi hata foleni ya Dar. Ningefurahi sana huko kwenye mitandao kama tungekuwa tunajadili jinsi ya kufanya mambo ya maendeleo.

“Mimi sionyeshwi njia ya kupita na mtu. Njia ya kupita tayari nilishaonyeshwa na ilani ya chama changu. Kuandikwa kwenye mitandao hata mimi ninaandikwa, kwa hiyo nijiuzulu? Kwangu mimi, kuandikwa siyo tija bali kuchapa kazi.

“Kuna wengine mmefikia hata hatua ya kunipangia. Nasema mimi ukinipangia ndio umeharibu. Watanzania mjue kampeni zimeshakwisha. Ulie, ugaregare lakini Rais ni mimi John Pombe Magufuli na kwangu ni kazi tu. Mimi ni rais ninayejiamini, sipangiwi mambo ya kufanya. Hata fomu ya kugombea nilikwenda kuichukua peke yangu, kwa hiyo Makonda wewe chapa kazi,” alisema Rais Magufuli.

Kauli hiyo iliyoshangiliwa na waliokuwepo kwenye tukio la uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa barabara za juu (flyover) eneo la Ubungo, iliwaduwaza wengi waliodhani juzi ndiyo ingekuwa siku yake ya kumaliza suala la Makonda.

Kwa takribani mwezi mmoja sasa, jina la Makonda limekuwa maarufu katika vyombo rasmi vya habari na mitandao ya kijamii kutokana na tuhuma za kughushi cheti cha kumaliza kidato cha nne.

Makonda mwenyewe hajawahi kukana wala kukiri tuhuma hizo na kwa aina ya staili ya uongozi wa Magufuli, ilitarajiwa kwamba angechukua hatua lakini hajafanya hivyo kwa kasi yake ile ile ya awali, tangu kuapishwa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kabla hilo halijamalizika, ndipo likaibuka sakata la Clouds; ambalo lilionekana kumshtua hata Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye, ambaye alilieleza kama lililotia aibu taifa letu.

Swali ambalo liko midomoni mwa wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa na wandani wa serikali ni kwamba; kuna nini kati ya Rais Magufuli na Makonda?

Ifuatayo ni mifano ya namna Magufuli alivyoshughulikia masuala ya viongozi wengine wa serikali yake.

ANNE KILANGO MALECELA

Mwezi Juni mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza kumvua madaraka aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, kwa madai ya kutoa taarifa zisizo sahihi kwake kuhusu suala la watumishi hewa mkoani kwake.

Akizungumza kwa uchungu Ikulu jijini Dar es Salaam, Magufuli alieleza kusikitishwa kwake na kitendo cha Mkuu wa Mkoa kusema mkoa wake hauna watumishi hewa ilhali watumishi hao wako.

Magufuli aliwaambia waandishi wa habari kwamba baada ya kupewa taarifa kwamba Shinyanga hakuna watumishi hewa, aliamua kutuma timu yake na hadi wakati anachukua hatua ya kumtumbua Kilango, walikutwa watumishi hewa 45.

Watetezi wa Anne-Kilango wanasema yeye alikuwa mgeni katika wadhifa wake huo na maelezo yake yalitegemea zaidi taarifa alizopewa na wasaidizi wake. Hata hivyo, huo haukuwa utetezi kwani Magufuli alimvua wadhifa wake huo.

Hata hivyo, katika hatua ambayo haikutarajiwa na wengi, Magufuli huyo huyo alimteua Anne Malecela huyo huyo kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Januari mwaka huu.

Wilson Kabwe

Aprili mwaka jana, Rais Magufuli alimsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe, wakati wa uzinduzi wa daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Kilichosababisha jambo hilo kilikuwa ni hatua ya Makonda kumtuhumu Kabwe kwa mambo kadhaa ya kiutendaji ikiwemo kuongeza mkataba wa maegesho ya magari kwenye jiji bila kupitia mchakato wa kutangaza zabuni, ulanguzi wa kodi za mapango kwenye stendi ya mabasi ya Ubungo na kusaini mikataba miwili ndani ya mwaka mmoja iliyosababisha upotevu wa mapato kwa jiji.

Baada ya tuhuma hizo zilizotolewa bila ya Kabwe kuwepo na kujitetea, Rais Magufuli, hapohapo darajani, aliuliza wananchi kama amtumbue bosi huyo wa jiji au la na wananchi walivyojibu “tumbuaa”, Magufuli akatangaza kumsimamisha kazi Kabwe.

Wilson Kabwe alifariki dunia baadaye mwaka jana lakini kinachokumbukwa ni muda aliouchukua Rais Magufuli kutoka kupokea tuhuma na kuchukua hatua.

Charles Kitwanga

Charles Kitwanga alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Rais Magufuli na alikuwa akichukuliwa kama mmoja wa wandani wake katika Baraza la Mawaziri.

Mei mwaka jana, wakati akijibu maswali ya wabunge bungeni, Kitwanga alizungumza huku akionekana kutawaliwa na ulevi.

Siku hiyo hiyo, Ikulu ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari iliyoeleza kwamba Rais amemvua Kitwanga wadhifa wake huo kwa sababu ya ulevi.

La muhimu, kwa mara nyingine tena, ni muda kutoka kuibuka kwa tuhuma au kutokea kwa tatizo na Rais kuchukua hatua.

DED aliyetishia trafiki

Oktoba mwaka jana, kuliibuka madai katika mitandao ya kijamii kuhusu kitendo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wilaya ya Mkinga, Emmanuel Mkumbo, kumtishia kwa bunduki askari wa usalama barabarani aliyekuwa akitimiza majukumu yake.

Siku hiyo hiyo, jioni, Ikulu ilitoa taarifa ya kumvua madaraka Mkumbo na kusema mtu wa kujaza nafasi yake atatangazwa baadaye.

Mwele-Ntuli Malecela

Desemba 16 mwaka jana, Ikulu ilitangaza kumtumbua Dk. Mwele Malecela katika wadhifa wake wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) katika hatua iliyowashtua wengi.

Siku moja kabla, Dk. Mwele alikuwa ametangaza ripoti ya utafiti iliyoonyesha kwamba asilimia 15 ya watu waliofanyiwa utafiti wamekutwa na virusi vya ugonjwa wa ZIKA.

Ugonjwa huo ni miongoni mwa magonjwa ambayo utangazwaji wake hutakiwa kuwa na baraka za wadau mbalimbali ikiwamo Serikali, Shirika la Afya Duniani (WHO) na wadau wengine na inaonekana kuwa kosa la Mwele lilikuwa kwamba hakuhusisha wadau wengine.

Hilo ndilo kosa lililomponza mwanasayansi huyo kupoteza kibarua chake ndani ya muda wa saa 24 tu tangu kufanyika kwa kosa.

Baadhi ya makosa ambayo wateule hawa walipoteza nyadhifa zao hayafanani kwa ukubwa wala shinikizo kutoka kwa watu wengine kulinganisha na Makonda, lakini Magufuli alichukua hatua haraka.

Swali ni je; kwa nini kigugumizi kwa Makonda ambaye pale inapotokea Makonda huyo anaweka tuhuma za wengine hadharani, Rais Magufuli amekuwa mwepesi kuchukua hatua na mfano mmojawapo wa hili ni tuhuma dhidi ya Wilson Kabwe, lakini tuhuma zinapoelekezwa kwa Makonda, kunajitokeza kinachoweza kutajwa na baadhi ya watu kuwa ‘kigugumizi’?

Hata hivyo, pamoja na hayo yote, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais ndiye mwenye mamlaka ya mwisho kuamua jambo gani afanye wakati gani na kwa sababu gani, hata kama atakuwa amepewa ushauri wa kiwango gani na baadhi ya washauri wake au vyombo vingine vya dola nchini.

No comments :

Post a Comment