Mbunge mashuhuri katika bunge la Tanzania ameikosoa vikali serikali ya nchi hiyo kwa hatua yake ya kutopigia kura azimio la Umoja wa Mataifa linalotaka serikali ya Myanmar ikomeshe operesheni za kijeshi zinazolenga kukandamiza jamii ya wachache ya Waislamu Warohingya nchini humo.
Siku ya Alkhamisi iliyopita Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayohusika na haki za binadamu ilipitisha rasimu ya azimio linaloitaka serikali ya Myanmar ikomeshe operesheni za kijeshi ambazo "zimesababisha ukiukaji ulioratibiwa na uvunjaji wa haki za binadamu" za Waislamu Warohingya wanaoishi katika jimbo la Rakhine.
Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 135 zilizounga mkono, nchi 10 zililipinga na nyengine 26 ziliamua kutopiga kura, Tanzania ikiwa moja ya nchi hizo.
Akiandika katika ukurasa wake wa kijamii wa Facebook, Zitto Kabwe ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, amesema: "Juzi Umoja wa Mataifa kulikuwa na kura ya Azimio la kulaani vitendo vya unyama dhidi ya watu wa kabila la Rohingya huko Myanmar. Nchi yetu haikupiga kura (abstained). Ni kitendo cha aibu sana Tanzania kushindwa kulaani vitendo vya namna hii".
Msimamo huo wa Tanzania umetafsiriwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kidini wa nchi hiyo kama kielelezo cha kubadilika sera za serikali ya sasa ya Dar es Salaam katika suala la kutetea haki na uadilifu duniani.
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni serikali ya Tanzania ilianzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel. Na hii ni katika hali ambayo msimamo wa huko nyuma wa Tanzania tangu enzi za uongozi wa Rais wa kwanza wa nchi hiyo hayati Mwalimu wa Julius Nyerere ulikuwa ni wa kutetea harakati za ukombozi za wananchi wa Palestina katika kukabiliana na dhulma na ukaliaji mabavu wa ardhi zao unaofanywa na utawala haramu wa Israel.../
http://parstoday.com/sw/news/africa-i36555-tanzania_yalaumiwa_vikali_kwa_kutopigia_kura_azimio_la_un_la_kutetea_waislamu_wa_myanmar
No comments :
Post a Comment