Balozi Seif wa kwanza kutoka Kulia akizungumza na Uongozi wa Kampuni ya Global Agence Limited ya Nchini Uturuki Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Viongozi wa Taasisi ya Tarbim iliyo chini ya Kampuni ya Global Agence Limited yenye Makao Makuu yake Nchini Uuruki wakifuatia Filam Maalum ya Historia ya kazi zinazofanywa na Kampuni ya Global Agence Limited.Kutoka Kulia ni Bwana Fidelis Bashasha, Bw. Abdulla M. Khalfan na Bw. Seif Abdallah Kassim.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akisalimiana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Global Agence Limited ya Nchini Uturuki Bwana Baddal Calikusu aliyefikia Ofisini kwake Vuga na Ujumbe wake kwa mazungumzo. Nyuma ya Balozi Seif ni Meneja wa Usafirishaji ambae pia ni Mkuu wa Maendeleo ya Biashara wa Taasisi ya Tarbim iliyo chini ya Kampuni ya Global Agence Limited Bwana Osan Liman.
Na. Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameushauri Uongozi pamoja na Watalaamu wa Kampuni ya Global Agence Limited ya Nchini Uturuki kusaidiana na Wataalamu Wazalendo katika kufanya utafiti wa kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo katika Sekta ya Maji Visiwani Zanzibar.
Alisema Tafiti hizo zinazopaswa kwenda kitaalamu zaidi zinaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa uimarishaji sambamba na upatikanaji wa huduma za Maji safi na Salama katika maeneo mbali mbali Mjini na Vijijini Unguja na Pemba.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa ushauri huo wakati akibadilishana mawazo na Uongozi wa Ngazi ya juu wa Kampuni ya Global Agence Limited kutoka Nchini Uturuki ukiongozwa na Mwenyekiti wake Bwana Baddal Çalikuşu { baddal chalkusu } ambao uko Zanzibar kwa ziara ya kuelezea Taaluma iliyokuwa nao Kampuni hiyo katika kuendesha miradi inayosaidia utatuzi wa huduma za Maji.
Alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na vianzio vingi vya maji hasa wakati wa Msimu wa mavua za Masika lakini hatimae rasilmali hiyo huishia Baharini na mengine kukauka kabisa bila ya matumizi sahihi ya msingi.
Balozi Seif alisema Maji ya mvua kwa Mataifa yaliyoendelea Kiteknolojia hutumiwa kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani baada ya kufanyiwa mchujo, ujenzi wa Mabwawa yanayotumika kwa kufugia samaki sambamba na matumizi ya kilimo mashambani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba upo umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Wataalamu wa Kampuni hiyo ya wale Wazalendo wa Mamlaka na Taasisi za Maji Nchini ili kuona rasilmaji ya Maji Visiwani Zanzibar inatumiwa kitaalamu na kwa uangalifu zaidi.
Mapema Meneja wa Usafirishaji ambae pia ni Mkuu wa Maendeleo ya Biashara wa Taasisi ya Tarbim iliyo chini ya Kampuni ya Global Agence Limited Bwana Osan Liman alisema Taasisi yao imekuwa ikifanya Utafiti na kusaidia Taaluma ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama katika maeneo mbali mbali Duniani.
Bwana Osman alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Wataalamu wa Taasisi hiyo iliyoasisiwa mnamo Mwaka 1957 hivi sasa wameboreka zaidi Kiteknolojia kasi iliyosababisha kuendelea kutoa huduma kwa zaidi ya Nchi 50 Duniani.
Alisema kwa sasa wanaendelea kutafuta mbinu na njia zitakazosaidia kukabiliana na tatizo la huduma za Maji katika kiwango cha Kisasa kinachokwenda sambamba na matumizi ya Mita zinazochangia matumizi hayo kwa kiwango na uangalifu mkubwa.
Bwana Osman alieleza kwamba mbali ya Sekta ya Maji lakini Kampuni ya Global iliyozaa Taasisi mbali mbali za Kiufundi imekuwa ikiendesha Miradi ya Kihandisi kwenye Sekta za Afya, Miundombinu, huduma za Umeme, Habari na Mawasiliano pamoja na Kilimo.
Kampuni ya Global Agence Limited kutoka Nchini Uturuki inatoa huduma za Kitaalamu katika Mataifa tofauti Ulimwenguni yakiwemo yale ya Bara la Afrika kama Angola, Ghana, Misri, Tunisia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Sudan, Mauritania ambapo kwa sasa pia wapo Bagamoyo Nchini Tanzania kufanya utafiti katika Sekta ya Maji.
No comments :
Post a Comment