Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, January 30, 2020

MAELEZO YA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, MGOMBEA UENYEKITI WA ACT – WAZALENDO KATIKA HAFLA YA KUCHUKUA FOMU YA KUGOMBEA UENYEKITI TAREHE 30/01/2020 !

 
Ndugu Waandishi wa habari,

Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyenzi Mungu, Muumba mbingu na ardhi ambaye kwa utukufu wake ametuwezesha leo hii kukutana hapa salama usalimini.

Niwashukuru waandishi wa habari kwa kuitikia mwaliko wetu huu. Aidha niwashukuru nyote mliohudhuria katika hafla hii kwani kwa kuwepo kwenu ndio mmeifanya shughuli hii kuweza kufana. Nasema ahsanteni sana.

Ndugu Waandishi wa habari,

Kama mnavyofahamu kuwa Chama chetu Cha ACT – Wazalendo kimo katika utaratibu wa kupanga safu yake mpya ya Uongozi. Chaguzi katika ngazi ya Matawi, Wadi/Kata, Majimbo na Mikoa, kwa kiasi kikubwa zimeshakamilika kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara na baadhi ya maeneo ambayo hayajakamilisha ndio wapo kwenye utaratibu wa kukamilisha Chaguzi hizo  hivi sasa.


Katika ngazi ya kitaifa utaratibu kama ilivyotangazwa na Kaimu Katibu Mkuu kuwa pazia la utaratibu wa kuchukua fomu limefunguliwa rasmi tarehe 27/01/2020 kwa wanaotaka kugombea nafasi mbali mbali za uongozi. Leo hii mimi, Maalim Seif Sharif Hamad nimeamua kutumia haki yangu ya kikatiba kama mwanachama hai wa ACT – Wazalendo kugombea nafasi ya MWENYEKITI WA CHAMA TAIFA.

Nafahamu kuwa nafasi ya Mwenyekiti kwa mujibu wa Katiba ya ACT -Wazalendo ni nafasi ya Uongozi na sio nafasi ya kiutendaji. Unapokuwa kiongozi wa Chama unakuwa ndio alama (Symbol) ya Chama na kile unachokisimamia. 
Nimeamua kuomba nafasi hii kwa sababu naamini nina uwezo na uzoefu wa kutosha wa kuitumikia nafasi hii. Pia nimeamua kuomba nafasi hii kwasababu naamini Wanachama waliowengi wanapenda niwemo katika safu ya Uongozi wa chama chetu kwa kuamini uwezo wangu na uzoefu nilionao bado unahitajika katika kukijenga chama chetu. Sikutaka kuwavunja moyo Wanachama wenzangu!

Ndugu Wanahabari,

Nimeamua kuomba ridhaa kwa Wananchama wenzangu kuwa Mwenyekiti wa Chama ili nipate kushirikiana na wenzangu kutoa uongozi katika Chama hasa wakati wa misukosuko. Tujenge umoja na mafahamiano ndani ya Chama, Umoja kati ya Wanachama na Viongozi, Umoja miongoni mwa Wanachama na Umoja miongoni mwa Viongozi.

Kwa kushirikiana na Viongozi na Wanachama wenzangu nataka kusimamia mwenendo wa chama kulingana na Katiba za Nchi, Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya Chama.

Nataka nitumie uwezo na uzoefu wangu kuendelea kujenga moyo wa kujiamini na kujitolea, kujenga hamasa kwa Viongozi, Watendaji na Wanachama kwa ujumla ili wote kwa pamoja wajifakharishe kwa chama chao cha ACT – Wazalendo.

Nataka kushirikiana na wenzangu kuongoza ujenzi wa Chama kwa kuingiza (install) utamaduni wa utendaji sahihi kwa kuendeleza moyo wa kujitegemea, nidhamu na kujali wakati ili Viongozi na Wanachama wetu wawe mfano wa kuigwa katika kutekeleza majukumu yao.

Kwa kushirikiana na wenzangu nataka kuona kuwa baada ya kipindi cha miaka 5 ikikamilika Chama kimekuwa – (transformed) kuwa injini imara ya kusimamia chaguzi za kiserikali kwa mafanikio makubwa na kuwa taasisi imara yenye nguvu inayoungwa mkono na Wananchi waliowengi na kuwa mfano nchini na nje ya nchi katika kuongozwa kwa misingi ya uwazi, usimamizi wa ukweli na utetezi wa mamlaka ya umma.

Kwa mashirikianao pamoja kati ya Viongozi na Wanachama nataka kuona ifikapo  mwaka 2025 Chama kiwe kinaongoza Halmashauri za Wilaya na Miji mingi na kuwa sehemu ya Uongozi wa Kitaifa wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakati huo huo ACT - Wazalendo iendelee kuongoza Serikali ya Zanzibar.

Ndugu Wanahabari,

Hiyo ndio ACT - Wazalendo ninayokusudia kuijenga kwa kushirikiana na wenzangu pindi wakinipa ridhaa ya kuwa Mwenyekiti wao kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Nawashukuru nyote kwa kunisikiliza.

Ahasanteni sana.

No comments :

Post a Comment