dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, January 15, 2022

HAMAD MASOUD OF ACT WAZALENDO: WOULD HE HAVE BEEN A GOOD FIT FOR MAO TSE TUNG'S POSITION?.........MJUWE!

HAMAD  MASOUD HAMAD

Angekua hai Maalim Seif Sharif Hamad, leo hii tungemwita Engineer Hamad Masoud Hamad, Mshauri wake (Maalim Seif) wa masuala ya Kisiasa (Political Advisor to the First Vice President of Zanzibar).

Hapa Zanzibar Engineer Hamad ni mmoja wa wanasiasa makini, machachari, asiyeyumba, anayesimamia, kukitetea na kukipigania anachokiamini.

Engineer Hamad alizaliwa tarehe 15 November, 1957  katika kijiji cha Kangagani, Pemba na alipata elimu yake ya msingi katika Skuli ya Kangagani (1964 - 1969), Elimu ya Secondary (First Cycle) katika Skuli ya Ole (1970 - 1972), Elimu ya A Level katika Chuo cha Ufundi cha Karume (1973 - 1976) kilichopo nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Mwaka 1977 - 1981, Engineer Hamad aliendelea na masomo yake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika Fani ya Uhandisi Ujenzi na kutunukiwa Shahada ya B.Sc Engineering na mwaka 1983  - 1984  alijiunga na Chuo Kikuu cha Loughborough University of Technology cha Uingereza na Kutunukiwa Shahada ya pili  ya Master of Science in Engineering (M. Sc. Eng.) ya Chuo hicho.

Engineer Hamad amehudhuria na kushiriki katika Mafunzo mbali mbali ya Fani ya Uhandisi, Utawala, Uongozi na Siasa katika nchi zaidi ya 15 zikiwemo Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Denmark, Finland, Sweden, Norway,  South Africa, India, Italy, USA, Belgium, Switzerland na Netherlands. Nchi nyengine ambazo Engineer Hamad ametembelea kwa Missions mbali mbali akiwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi ni Libya, Kenya, Nigeria, UAE, nk.

Engineer Hamad ni mwanachama (member) wa Jumuia/Taasisi kadhaa za Kimataifa na ametunikiwa vyeti mbali mbali.

Mfano; mwaka 2011 aliteuliwa na Taasisi ya Kimataifa iitwayo CHARTED INSTITUTE OF LOGISTICS & TRANSPORT (CILT) kuwa  Chartered Member. Mwaka huo huo alitunukiwa tunzo  iitwayo  DISTINGUISHED ALUMNI AWARD for Outstanding Performance & Achievement in Engineering and Infrastructure ya Chuo Kikuu cha Loughborough kilichoko Uingereza na hivi juzi tu tarehe 16 Disemba 2021, Engineer Hamad ametunukiwa  na Chuo Kikuu cha Jumuia ya Madola (University of Commonwealth) & London Graduate Schools, Cheti cha MASTERCLASS in   Business Management  and Leadership.

Akiwa Mjumbe wa BLW, katika kipindi cha 1995 - 2000, Engineer Hamad alikamatwa na kuwekwa gerezani yeye na Viongozi na Wanachama wengine 17 kwa miaka mitatu ( 3) 1997 - 2000 kwa kesi ya Uhaini, kesi ambayo ilikua ya kubuni na hatimae Serikali ikawafutia mashtaka na wakawa huru.

Engineer Hamad, mwaka 2000 hadi 2015 akachaguliwa tena na tena na Wananhi wa Jimbo la Ole kuwa Mwakilishi wao. Engineer Hamad ni Nembo  (ICON) na Fahari (Pride) ya watu wa Jimbo la Ole.

Akiwa na miaka 24 tu Engineer Hamad baada ya kumaliza masomo yake ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salam, mwaka 1981 alianza kazi ya Uwalimu katika Chuo cha Ufundi cha Karume na akawa Mkuu wa Idara  ya Uhandisi Ujenzi( Head of Civil Engineering Department)

Mwaka 1985 baada ya kumaliza masomo yake ya Shahada ya Pili (M. Sc.Engineering) alihamishiwa Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, katika Idara ya Maji, Zanzibar, akiwa Mhandisi Mkuu na Disemba mwaka 1985, Engineer Hamad aliteuliwa na Rais wa Zanzibar kuwa Mkurgenzi wa Maji hadi August 1990.

Kama anavyoeleza mwenyewe, Engineer Hamad safari yake ya kisiasa ilianza mwaka 1992 akiwa kijana pekee katika harakati za Kisiasa. Hata hivyo, tarehe hiyo haifuti jitihada zake za nyuma za kumuunga Mkono Maalim Seif Sharif Hamad wakati wote kuanzia mwaka aliofukuzwa ndani ya CCM na hatimae kuekwa kizuizini.

Ni wakati huo pia ambapo Engineer Hamad aliungana na wenzake wengi kuanzisha vuguvugu la kisiasa na harakati za kuhakikisha kua Maalim Seif anakua huru na Chama mbadala cha kutetea haki na maslahi ya Zanzibar kinaanzishwa.

Mwaka 1995 ndio mwaka ambao unaweza kuita mwaka wa Engineer Hamad katika siasa za mfumo wa Vyama vingi ambapo mwaka huo alichaguliwa rasmi kua Mwakilishi na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Jimbo la Ole alikozaliwa na kukulia kupitia Chama cha Wananchi CUF.

Nafasi hii aliitumikia mpaka mwaka 2015 akiwa na nafasi mbali mbali za Baraza la Wawakilishi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kama vile, Makamo Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, Waziri Kivuli wa Maji, Nishati, Ujenzi na Ardhi kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano kuanzia mwaka 2010 hadi 2012 alipouzulu ili kulinda heshma yake na heshima ya Chama chake kufuatia kuzama kwa meli ya MV. Skagit na hatimae badae akawa Mjumbe wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo wa Baraza la Wawakilishi.

Pamoja na Engineer Hamad kushika nyadhifa zote hizo za Kiserikali, yeye ndie Kiongozi ambae alishika nafasi nyingi zaidi za Kisiasa ndani ya Chama chake kuanzia mwaka 1992 hadi 1999 akiwa Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa Chama cha Wananchi CUF, mwaka 1999 hadi 2001 akiwa Mkurugenzi wa Organization, mwaka 2001 hadi 2002 akiwa tena Mkurugenzi  wa Haki za Binadamu, mwaka 2002 hadi 2010 akiwa tena Mkurugenzi wa Organization  na hatimae mwaka 2012 akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Zanzibar.

Engineer Hamad pia alikua Mjumbe wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi  CUF kuanzia mwaka 1992 hadi pale yeye na Viongozi wenzake walipoamua kukiacha Chama hicho na Kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo ambapo kwa sasa yeye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho chenye wafuasi wengi Visiwani Zanzibar.

Pamoja na nyadhifa zote hizo na nyengine nyingi alizowahi kuzitumikia, Engineer Hamad hakuacha kupata madhila ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo aliitumikia kwa muda mrefu na katika nyadhifa mbali mbali. Inasemekana yeye ndie Kiongozi pekee ambae kila Uchaguzi unapofanyika hukamatwa na Vyombo vya dola na kuekwa ndani mpaka pale Uchaguzi unapomalizika. Hii unaweza kusema ni kutokana na hofu ya Viongozi wa CCM na Serikali yao kwa Hamad Masoud Hamad hasa kutokana na misimamo yake na fikra zake za Kisiasa Visiwani  Zanzibar.

Mfano mmoja wa hivi karibuni ni mwaka 2020 mapema karibu na siku ya kupiga kura, Engineer Hamad alikamatwa Airport Pemba akitokea Unguja na hatimae kuekwa ndani mpaka Uchaguzi ulipomalizika.

Hata hivyo, baada ya joto na heka heka za Uchaguzi kumalizika na Maalim Seif na wenzake kuamua kushiriki katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif alimpendekeza Engineer Hamad kwa rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi kua Mshauri wake (Mshauri wa Makamo wa Kwanza) wa masuala ya Kisiasa.

Jambo hili si watu wengi wanalifahamu hasa ikizingatiwa kua, kabla ya pendekezo hilo kufanyiwa kazi na Engineer Hamad kuteuliwa rasmi kua Mshauri wa Maalim Seif Sharif Hamad (Makamo wa Kwanza wa Rais) katika mambo ya siasa, Maalim Seif Sharif Hamad alifariki dunia.

Hata hivyo, suala hilo linakumbukwa na Engineer Hamad mwenyewe kama moja ya mambo mengi makubwa aliyopata kufanyiwa na Maalim Seif Sharif  Hamad kutokana na imani yake dhidi yake, uwezo wake wa utendaji na ufahamu wake nzuri wa siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Hivyo; Engineer Hamad Masoud Hamad anabaki kua  mmoja wa wanasiasa machachari Visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kutokana na umahiri wake, moyo wake wa kujitolea na misimamo yake isiyoyumba linapokuja suala la maslahi ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ndio maana kama tungemuuliza Maalim Seif Sharif Hamad leo hii "Engineer Hamad ni nani?". Angetujibu "Ni mshauri wake wa masuala ya Kisiasa".


No comments :

Post a Comment