SMZ kuzifutia usajili meli za Iran
KUFUATIA meli 10 za mafuta za nchini Iran, kupeperusha bendera ya Tanzania, katika bahari ya Tanzania, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), inakusudia kuzifutia usajili, ili kuepuka kuwekewa vikwazo vya kimataifa.
Tamko hilo limetolewa jana na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, wakati akisoma hotuba yake, ya kuahirisha baraza hilo huko katika ukumbi wa Baraza hilo Chukwani Mjini Zanzibar.
Alisema Serikali ya Zanzibar imo katika hatua za kuzifutia usajili meli hizo ambazo zinadaiwa zinafanya biashara na Makampuni ya mafuta ya Serikali ya nchi hiyo.
Balozi Seif, alisema kuwa serikali imeamua kuchukua uamuzi huo baada ya kufanya uchunguzi juu ya suala hilo ambapo wamebaini kuwapo kwa kasoro ambazo zilifanywa na Mamlaka ya usafiri wa baharini.
“Serikali ililifuatilia suala hili kwa undani na imegundulika kuwa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA) kupitia kwa Wakala wetu wa Dubai Philtex ilisajili meli 36 za Iran za Mafuta (crude oil tankers) na Makasha (containership) na kupeperusha bendera ya Tanzania” alisema Balozi Seif.
Alisema hapo awali taarifa za meli hiyo zilieleza kuwa zilisajiliwa Zanzibar na zinapeperusha bendera ya Tanzania na zimekuwa zinafanya biashara na Makampuni ya mafuta ya Serikali ya Iran.
Taarifa hizo zilieleza kuwa jambo hilo ni kinyume na Azimio la Umoja wa Mataifa Namba 1429 na amri ya utekelezaji wa azimio hilo (Executive Order) iliyotolewa na Serikali ya Marekani na Nchi za Jumuiya ya Ulaya.
Balozi Seif, alisema kutokana na hali hiyo serikali iliamua kulifanyia uchunguzi kupitia Wizara husika na kubaini kuwa nchi ya Iran imewekewa vikwazo vya kiuchumi na Umoja wa Mataifa.
Vikwazo hivyo Balozi Seif, alisema iwapo itatokea nchi yoyote kuisaidia kukwepa Azimio hilo, nchi hiyo nayo itawekewa vikwazo kama hivyo vilivyowekewa Iran.
Hivyo, Balozi Seif alisema baada ya kugundua ukweli kwamba meli hizo zinapeperusha bendera ya Tanzania, Serikali ya Zanzibar imo katika hatua za kuzifutia usajili meli hizo na pia kuifutia uwakala kampuni ya Philtex.
Aidha, Balozi Seif, alisema Serikali ya Zanzibar itafanya uchunguzi zaidi kujua ni vipi usajili huo ulifanyika.
Hata hivyo, Balozi Seif, alisema pamoja na kutokea tukio hilo, lakini bado serikali ya Zanzibar, itaendeleza uhusiano katika mambo mengine.
Aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud, kabla ya kuachia ngazi alitoa taarifa kwa Baraza la Wawakilishi Julai 24, 2012 kwamba kampuni zilizokuwa zikifanya hivyo zilivutiwa na aina ya viwango vya leseni za kufanya shughuli hizo katika bahari ya Zanzibar.
Chanzo: Zanzinews (Mapara)
No comments :
Post a Comment