SMZ yabadili utaratibu usafiri majini |
Monday, 13 August 2012 21:23 |
ABIRIA wanaosafiri kwa vyombo vya baharini kati ya Zanzibar, Bara na Pemba kuanzia sasa wanapaswa kuwa na vitambulisho kabla ya kuuziwa tiketi za kusafiria. Waraka uliotolewa na Mamlaka ya Usafiri na Vyombo vya Baharini ya Zanzibar (ZMA), unaeleza kwamba wasafiri wote lazima waonyeshe vitambulisho ndipo wauziwe tiketi za safari zao. “Kuanzia Jumatatu ya tarehe 13 Agosti, 2012 abiria wote watakaonunua tiketi za kusafiria za vyombo vya baharini lazima wawe na vitambulisho vinavyoonyesha taarifa zake muhimu,” unasema waraka huo wa Agosti 10, mwaka huu. Waraka huo umevitaja vitambulisho vinavyotakiwa kuwa ni kitambulisho cha Mzanzibari, leseni ya udereva, kadi ya benki, vitambulisho vya kazi, pasi ya kusafiria, barua ya Sheha na kadi za ZSSF/NSSF na Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii. Mwandishi wa habari hizi alimshuhudia mwananchi mmoja akitaka tiketi jana na kuelezwa kuwa, lazima awe na kitambulisho naye akajibu kuwa ana kitambulisho cha kupigia kura na wauzaji wakasema watampa tiketi japokuwa waraka huo haukukitaja kitambulisho hicho. Kaimu Mkurugenzi wa ZMA, Abdallah Hussein Kombo alipoulizwa jana kuhusu hatua hiyo alisema lengo lake ni kudhibiti abiria na kujua taarifa za watu wote wanaosafiri katika vyombo vya baharini. “Hakuna malengo zaidi ni hayo tu ya kudhibiti abiria na kujua ni nani wanasafiri,” alisema Mkurugenzi huyo. Waraka huo umesambazwa kwa mameneja na wakurugenzi wa kampuni za Shirika la Meli Zanzibar, Azam Marine/Coastal Ferries, Sea Star Services, Mega Speed Liners, Fast Ferries Ltd, African Shipping, Jack Enterprises na Hammy Distributors. Uamuzi huo umekuja baada ya siku za karibuni wakati wa utoaji maoni ya Katiba Mpya katika mikoa ya Kusini Unguja na Kusini Pemba, baadhi ya watu kupendekeza kuwa utaratibu wa kutumia pasipoti kwa wasafiri kati ya Bara na Zanzibar urejeshwe. |
Source: Mwananchi
No comments :
Post a Comment