Marehemu Daud Mwangosi
Kifo cha Daudi Mwangosi: Unyama huu hadi lini?
Marehemu Daudi Mwangosi mwisho kulia
Sikika imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.Kwa mujibu wa vyombo vya habari, marehemu Mwangosi alikuwa kazini akitimiza wajibu wake wa kutafuta habari. Tumestushwa zaidi baada ya kuona picha za mnato zikionyesha jinsi ambavyo mtu anayedaiwa kuwa ni mwandishi huyo akishambuliwa na idadi kubwa ya askari polisi na baadae kupoteza maisha.
Katika siku za karibuni, tumeshuhudia ongezeko la matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na jeshi la polisi, ambayo siyo tu yanasababisha uharibifu mkubwa wa mali za wananchi bali pia baadhi yao kupoteza maisha. Mfano, mwezi uliopita, tuliarifiwa kuwa kijana aliyeuawa mkoani Morogoro alikuwa akiuza magazeti na wala hakuhusika katika vurugu kwa namna yoyote. Vivyo hivyo, marehemu Mwangosi alikuwa akitimiza wajibu wake wa uandishi wa habari.
Uhai ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania. Hivyo, ni jukumu la polisi kulinda maisha na uhai wa wananchi wote bila kujali itikadi au kazi zao.
Hakuna sheria inayohalalisha kujeruhi, kutesa wala kuua mwananchi yeyote kwa sababu tu ati amekataa kutii amri ya polisi. Sikika inasikitishwa zaidi na utamaduni unaozoeleka ndani ya jeshi la polisi kwamba matukio ya kujeruhi, kutesa au vifo ni halali iwapo wanasiasa au wananchi hawakutii amri.
Kwa mtazamo wetu, amri ya serikali au polisi haitakiwi kuwa juu ya Katiba inayolinda haki ya kuishi. Hivyo, kisingizio cha kukiuka amri ya polisi hakitakiwi kuwa sababu ya kujeruhi wala kuua binadamu yeyote. Hata kama polisi watatoa maelezo kukanusha kuwa picha ya mtu anayeteswa si mwandishi, je wanayo haki ya kumjeruhi, kumtesa au kumdhalilisha mtanzania yeyote kama inavyoonekana kwenye picha hizo?
Tangu matukio haya ya kujeruhi, kutesa na hata kuua wananchi yalipoanza, hakuna hatua za dhati zilizochukuliwa na serikali wala jeshi la polisi. Vitendo hivi vinavyofanywa na polisi siyo tu vinapunguza imani ya jeshi hilo kwa wananchi, bali pia vinakiuka wajibu wa msingi wa jeshi hilo ambao ni kulinda usalama wa raia.
Ni matumaini yetu kwamba waliohusika na kifo cha Daudi Mwangosi na watanzania wengine waliopoteza maisha katika mazingira ya aina hii, watachukuliwa hatua stahiki. Pia, maaskari wanaoonekana katika picha hizo wakimtesa na kumnyanyasa raia wafikishwe kwenye vyombo vya sheria ili iwe funzo kwa wengine.
Tunatoa pole nyingi kwa familia na ndugu wa marehemu Daudi Mwangosi pamoja na tasnia ya habari hapa nchini.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi, Amen.
www.sikika.or.tz
No comments :
Post a Comment