Kifo cha Daudi Mwangosi
Wahamaza yatoa tamko
Kifo cha Daudi Mwangosi - Wahamaza yatoa tamko
KUHUSU: KIFO CHA DAUD MWANGOSI
Tumepokea kwa masikitiko na mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha mwandishi wa habari wa Channel Ten mkoani Iringa, DAUD MWANGOSI.
Mshtuko zaidi umekuja baada ya kujuwa kwamba kumbe mwandishi mwenzetu AMEUAWA, na mbaya zaidi ameuliwa na POLISI wa Serikali. Haya ni mauaji mabaya sana. Hayana sababu yoyote ya kutekelezwa. Na kwa hakika hayakubaliki kwa kigezo chochote kile.
Tunasema kwa kinywa kipana TUNAYALAANI sana mauaji haya. Tunasikitika kuona kwamba serikali taratibu inawarudi raia zake, na sasa inaua waandishi wa habari, siku chache tangu alipouliwa kijana mbichi eneo la Msamvu, mjini Morogoro, katika mazingira ambayo pia yenyewe yanatia shaka.
Tena ni mwezi mmoja tu tokea serikali, inayojinasibu kuwa inaheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu, ithubutu kutumia sheria mbaya kufungia gazeti la MwanaHALISI kwa muda usojulikana.
Vitendo vyote hivi vinaonesha ni kwa namna gani, na kiwango gani Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inashauku hasa ya KUZIMA sauti za wasio na sauti.
Ijuwe inajijengea taswira ya kuchukuliwa kuwa inapenda kukandamiza haki za binadamu na kudhoofisha utawala bora. Na hili nalo halikubaliki.
Sisi tunasema wazi kwamba harakati zozote katika jamii, ziwe ni za wananchi kujiletea maendeleo yao, au kwa ajili ya kudai haki hii au ile, pamoja na zile zinazolenga kulinda amani katika nchi kama ambavyo vyombo vya dola nchini petu hupenda kusema, zaweza na zinapaswa kuendeshwa kwa utaratibu mzuri unaodumisha amani.
Hakuna sababu ya kufanya haya kwa kuruhusu damu ya mwananchi hata mmoja kumwagika kizembe.
Kutokana na taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari kuhusiana na mazingira yalivyokuwa kabla ya MWANGOSI kuuliwa, tunaamini kwamba Polisi walijuwa fika kuwa mtu waliyekuwa wanasongana au kugombana naye na hatimaye kumuua, alikuwa ni mwandishi wa habari.
Ni hatari kubwa kukuta Polisi waliweka chuki na utashi binafsi mbele ya hekima na busara waliyopaswa kuitumia.
Ona sasa kilichotokea baada ya ukorofi wao. Ni kitu cha aibu kubwa kwao na kwa wale waliowapa silaha na hatimaye kuzitumia vibaya kama vile wanapambana na majambazi au magaidi.
Sasa basi, tunataka ufanywe UCHUNGUZI HURU kupitia watu wajuzi, wanaoheshimika na ambao kazi yao na matokeo watakayokuja nayo, yataaminika.
Katibu wa Jumuiya ya Wahabari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) ….................................... Salma Said
No comments :
Post a Comment