Marehemu Daudi Mwangosi
Wednesday, 5 September, 2012.
MSIMAMO WA BLOG LA ZANZIBAR NI KWETU JUU YA KUGOMEA HABARI KUHUSU VYOMBO VYA USALAMA NCHINI
ZANZIBAR NI KWETU inajibu kama ifuatavyo:
[1] Baada ya kupata maombi hayo kutoka kwa wanaukumbi wetu, bila ya kujali misimamo ya Wanahabari wengine au vyombo vyengine vya habari nchini vyenye kuregarega na vyenye kuenda mbele na kurejea nyuma, ZANZIBAR NI KWETU inaengeza muda wa kuwasusia polisi kwa wiki mbili baada ya moja tulioitangaza kabla. Mgomo huu kwa sasa utamalizaka tarehe 16 September, 2012, badala ya tarehe 9 September, 2012.
[2] ZANZIBAR NI KWETU inaamini kuwa, madamu bado tumo kwenye Muungano, Zanzibar na Bara ni kitu kimoja.
Unyama akifanyiwa mtu kutoka Bara na vyombo vya Usalama, hio itakuwa ni sawasawa na huo unyama kufanyiwa mtu kutoka Zanzibar.
Ushenzi akifanyiwa mtu kutoka Bara ni sawa na ushenzi huo kufanyiwa Mzanzibari.
Akiuliwa mtu kutoka Bara na polisi nchini ni sawasawa na kuuliwa Mzanzibari.
Kwahivyo, sisi hatukubali kugawiwa katika makundi ya wa-Bara na makundi ya wa-Zanzibari na baadae tukawapa mwanya/upenyo polisi kutuuwa zaidi with impunity.
Zaidi, tunawapa mkono wa hongera Jumuiya ya Wanahabari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) kwa msimamo wao wakishujaa walioueleza juu ya hili suala.
[3] Tunawagomea polisi wa Tanzania nzima sio tu kwasababu tunapenda kufanya hivyo. Nia yetu ni kuwafanya watambue kuwa wamefanya kosa kubwa sana kwa jamii yetu na wajirekebishe - kosa ambalo mpaka hivi sasa hawajalitambua, kwani hatujasikia hata polisi mmoja kukamatwa au mkubwa mmoja kujiuzulu, japokuwa waliofanya kosa hilo na wakubwa wao wanajulikanwa vizuri sana.
[4] ZANZIBAR NI KWETU inatoa wito kwa Wazanzibari wote wanaopenda maendeleo ya nchi yao kuyazingatia haya yaliotokea kwa makini sana, kwani ZNZ haina jeshi lake wenyewe. Jeshi la polisi na vyombo vyote vya usalama ni vya Muungano. Kama jeshi la polisi linathubutu kufanya unyama na ushenzi kama huu kule Bara, basi wataweza kufanya hivyo hivyo hapa ZNZ. In fact, tayari washafanya hivyo mara nyingi huko nyuma hapa ZNZ na roho tele za Wazanzibari zilipotea.
[5] ZANZIBAR NI KWETU inasikitika na kushitushwa na baadhi ya vyombo vya habari vinavyoelezea kuwa yaliotokea yalikuwa mauwaji ya kutisha na kusikitisha, lakini papo hapo havina misimamo thabiti na imara. Misimamo yao inabadilika kila baada ya dakika moja kama vimbaumbau wanavyobadilisha rangi zao. Hii sio sura nzuri na polisi wanafurahi kila tukiwa hatuna mshikamano.
[6] ZANZIBAR NI KWETU inasema kuwa ni USALITI kusema kwamba polisi wanatuhumiwa, kwani ukweli ni kuwa polisi hawatuhumiwi, bali polisi inaaminika na ni kwa uhakika mia kwa mia (100%) kuwa ndio waliomuuwa Ndugu Daudi Mwangosi. Kusema kama polisi wanatuhumiwa ni kutokuwa na uhakika na kuwa na shaka kwa jambo ambalo sote tunajua kuwa polisi ndio waliolitenda. Video zipo zinazoonesha hivyo na watu wapo walioshuhudia ukweli huo.
[7] Mwisho, sisi ZANZIBAR NI KWETU tunarejea tena kuandika kuwa jeshi letu la polisi bado lipo sawasawa na jeshi la kikoloni tulilolirithi miaka 50 nyuma na tutaendelea kulilaani kwa nguvu zetu zote kwa unyama na ushenzi walioutenda na kwa kushindwa kuzilinda jamii zetu mpaka hapo litakapobadilika!
MOLA AMLAZE PEMA PEPONI
DAUDI MWANGOSI. AMEN!
No comments :
Post a Comment