Zoezi la sensa Zanzibar lafikia mfundani
Na Khamis Mohammed
HUKU zoezi la sensa ya watu na makaazi likiwa limemalizika, wananchi wengi waliendelea kujitokeza kushiriki, ingawa pia baadhi yao waliendelea kugomea zoezi hilo siku moja kabla ya kufungwa.
Wakizungumza na Zanzibar Leo katika maeneo tofauti ya visiwa vya Unguja, baadhi ya masheha na wasimamizi, walisema, wamefanikiwa kwa asilimia kubwa kuwahamasisha wananchi kushikiriki kikamilifu zoezi hilo la kitaifa kwa kutoa takwimu sahihi kulingana na madodoso husika.
Walisema, pamoja na wananchi wengi kujitokeza kwenye zoezi la sensa na makaazi ya watu, bado kulikuwepo na changamoto kadhaa zilizowakabili ambazo hata hivyo, hazikuweza kuathiri zoezi hilo.
Naibu Sheha wa Pangawe, Makame Mwadini Masoud, alisema, asilimia kubwa ya wananchi katika shehia walijitokeza huku idadi ndogo ya watu ikiendelea kugomea, lakini kwa ujumla zoezi hilo likipata mafanikio ndani ya shehia hiyo.
"Kadri ya tulivyokuwa tukielekea siku za mwisho, watu wengi walijitokeza hasa wale ambao awali walitugomea, lakini tuliwaandisha bila kujali kauli walizokuwa wakizitoa kabla zilizokuwa zikipinga kuhesabiwa kwao", alisema.
Hata hivyo, naibu sheha huyo alielezea haja ya kuangaliwa uwezekano wa kuongezwa siku ili kuhakikisha wale wato waliojitokeza katika siku za mwisho wanaandikishwa na kufikiwa malengo ya asilimia mia moja.
Naye naibu wa sheha wa Chwaka, Asha Mohammed Abdi, alisema, kati ya kaya 30 zilizokuwa zimegomea zoezi hilo, ni kaya tano tu hadi jana mchana ndizo zilizokuwa zikiendelea kususia zoezi hilo.
"Hawa waliogoma tulikuwa tukiendelea kuwashawishi wajiandikishe na ni matarajio yetu itakapofika jioni, tunaweza kufikia mahali pazuri kwa kushiriki kikamilifu".
Akizungumzia juu ya zoezi hilo, msimamizi wa shehiya hiyo, Mtumweni Abdalla Abdalla, alisema, wanamatarajio makubwa ya kufakikisha kwa asilimia kubwa zoezi hilo baada ya wananchi kuendelea kujitokeza katika siku ya mwisho ya zoezi hilo.
Sheha wa Tomondo, Mohammed Omar Said, alisema, zoezi la sensa limepata mafanikio ingawa baadhi ya watu waliendelea kugoma bila ya kuwa na sababu za msingi zilizowafanya wagome.
Naye Sheha wa Fumba, Issa Hassan Shoka, alisema, watu wengi walijtokeza katika siku ya mwisho ya zoezi huku akielezea haja ya kuongezwa muda kwa zoezi hilo la kitaifa.
"Naomba kama kutakuwa na uwezekano basi zoezi hili liongezwe muda japo siku tatu ili kuwafanya watu waliokuwa hawajiandikisha kutumia muda huo kushiriki kikamilifu".
Zoezi la sensa ya idadi ya watu na makaazi lililoanza usiku wa kuamkia Agosti 26 mwaka huu, lilitarajiwa kufikia tamati jana baada ya kuendelea kwa siku saba nchini kote hapa Tanzania.
Source: Mapara
No comments :
Post a Comment