Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, October 6, 2012

BOMOA BOMOA DAR!

Nyumba 114 zabomolewa bondeni Dar
6th October 2012

Polisi wa kutuliza ghasia wakisimamia zoezi la ubomoaji hiari wa nyumba kandokando ya Mto Msimbazi eneo la Kinondoni Hananasif, Dar es Salaam jana. Zaidi ya nyumba 100 zimebomolewa kwenye eneo hilo ili kuwalazimisha wakazi wake kuhamia maeneo salama na kuondoka eneo hilo kwa kuhofia mafuriko. Hata hivyo wakazi hao wamelaumu kwa kutopatiwa mahema na vyoo kwenye maeneo waliyotakiwa kwenda huko mabwepande.
Serikali imebomoa nyumba 114 zilizojengwa kwenye bonde la Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Bomoa bomoa hiyo iliyofanyika jana kuanzia majira ya saa 12:00 alfajiri imesababisha kaya zaidi ya 2000 kukosa sehemu la kulala.

Nyumba zilizobomolewa ni zile zilizojengwa ndani ya bonde la Mto Msimbazi eneo la Hananasifu mtaa wa Mkunguni B na kuzusha mtafaruku kwa wananchi hao ambao walionekana wakihangaika kuokoa mali zao.

Wakati wa ubomoaji huo uliofanywa na Manispaa ya Kinondoni,  kulikuwepo na ulinzi mkali wa askari polisi wenye silaha mbalimbali ikiwemo bunduki za moto pamoja na mabomu ya machozi.

Hata hivyo taarifa iliyotolewa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Hananasifu, Rose Nyande ni kwamba ubomoaji huo ni mwanzo wa kuwahamisha wakazi wanaoishi mabondeni kama alivyoahidi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadick hivi karibuni.

NIPASHE JUMAMOSI ilishuhudia baadhi wa wananchi hao wakiwa na nyuso za huzuhi na baadhi yao wakiangua vilio wakati wakishuhudia nyumba zao zikibomolewa na watu maalum waliopewa kazi hiyo.

Wakizungunza kuhusu tukio hilo, wananchi hao waliilalamikia Serikali kuchukua hatua hiyo bil kuwapa taarifa na kusababisha wengi wao kushindwa kuokoa mali zao.

Mkazi wa eneo hilo Mzee Yusufu Tipa alisema kazi ya ubomoaji huo umefanywa kwa kushtukizwa kwani walivamia majira ya saa 12:00 na kutakiwa kuondoka kwenye nyumba zao haraka ili nyumba hizo zibomolewe na watu maalum walioletwa kwa kazi hiyo.

"Kila mtu hakufahamu kama kutakuwa na zoezi hili, watu wengi wamepotesa mali zao wakati wakihangaika kuziokoa katika nyumba zao, hatukutendewa haki hata kidogo," alisema Mzee Tipa.

Alisema wao hawapingi kuhama eneo hilo na kwenda Mabwepande kama Serikali inavyotaka, wanachopinga ni jinsi zoezi hilo lilivyoendeshwa kibabe kama wao ni wakimbizi kutoka nje ya nchi.

"Tulichofanyiwa hapa ni kama wakimbizi, hatukuruhusiwa kuuliza chochote na kama mtu akijaribu kukataza watu kuingia ndani anakamatwa, hili jambo halivumiliki ikiwa sisi wananchi ndio tuliopiga kura kwa serikali hii," aliongeza kusema.

Aidha, Neema Nampanda alisema baada ya watu wanaofanya kazi ya kubomoa kuvamia eneo hilo, kulitokea mtafaruku uliosababisha watoto wengi kukimbia na haijafahamika wapi walipoelekea.

Alisema kutokana na hali hiyo wamejikuta wakifanya kazi ya ziada ya kuwatafuta watoto wao huku wakati huo wakiendelea kuokoa mali zao zilizokuwemo ndani ya nyumba hizo.

'Hapa unaponiona sijui watoto wangu wapo kwa majirani au wamekimbilia wapi, kwani walipofika kulikuwa na vurugu kubwa kiasi ambacho watoto walikimbia kwa hofu," alisema Nampanda.

Kwa ujumla hali katika eneo hilo ilionekana imezizima kwa majonzi wengi wa wakazi hao walionekana kukaa nje ya nyumba zao pamoja na vifaa vyao mbalimbali na baadhi yao walianza kubomoa wenyewe nyumba zao kabla wabomoaji hao hawajafika.

Hata hivyo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Hananasifu, Rose Nyande alisema kwamba zoezi hilo limeendeshwa kihalali kwa kuwa walishatoa taarifa za wananchi hao kuhama mara moja kutokana na eneo hilo kuwa hatarishi kwa maisha yao.

Alisema watu wote waliobomolewa nyumba walishapewa viwanja eneo la Mabwepande lakini walipotakiwa kuhama eneo hilo walikaidi.

"Tunachokifanya hapa ni kubomoa nyumba ambazo wamiliki wake wamepatiwa viwanja, wale ambao hawajapewa hatutazigusa na malalamiko yao kuwa hatukuwaeleza juu ya zoezi hili sio kweli," alisema Nyande.

CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment