Sunday, October 21, 2012
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad
akiwahutubia wafuasi ya wapenzi wa chama hicho
katika viwanja vya Buguruni jijini Dar es Salaam.
Wafuasi na wapenzi wa CUF wakimsikiliza Katibu
Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif
Hamad wakati akiwahutubia katika viwanja vya
Buguruni jijini Dar es Salaam.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa ulinzi na usalama wa ADC
Bw. Al-Badawi akizungumza katika mkutano wa
hadhara wa CUF baada ya kuamua kurejea CUF
akitokea ADC. Kabla ya kwenda ADC na baadae
kurejea CUF Al-Badawi alikuwa mwenyekiti wa
CUF Wilaya ya Temeke
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad
akimkabidhi shati la chama hicho kijana Joseph
Christian ambaye alikuwa katibu mwenezi wa
CHADEMA tawi la Chuo Kikuu Dodoma.
Joseph amekihama CHADEMA na kujiunga na CUF
kwenye mkutano wa hadhara huko Buguruni jijini
Dar es Salaam.
(Picha na Salmin Said, OMKR)
Na Hassan Hamad, OMKR
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim
Seif Sharif Hamad amesema chama chake kitaendelea
kutetea na kutekeleza sera yake ya kuwaunganisha
watanzania popote walipo bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Amesema operesheni mchakamchaka hadi
mwaka 2015 iliyozinduliwa na chama hicho hivi karibuni
imekuwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo, na
kwamba tayari imeanza kuleta mafanikio katika
mikoa iliyoanza kutekelezwa ukiwemo mkoa wa Arusha.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika viwanja vya Buguruni
jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwahutubia wafuasi na
wapenzi wa chama hicho kwenye mkutano maalum
wa hadhara uliolenga kuwakaribisha wanachama
wapya na kuwapokea wanachama walioamua kurejea
CUF baada ya kukihama na kuhamia vyama vyengine.
Katika mkutano huo Maalim Seif aliwapokea na
kuwapa kadi za chama hicho wanachama kadhaa
walioamua kurejea chama hicho wakitokea chama
cha ADC wakiongozwa na aliyekuwa Mkurugenzi
wa ulinzi na usalama wa ADC Bw. Al-Badawi.
Kabla ya kujiunga na ADC, Bw. Al-Badawi alikuwa
mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Temeke, na sasa
ameamua kurejea CUF kwa kile alichokieleza kuwa
ni ubabaishaji ndani ya chama hicho kipya
kinachohusishwa na mbunge wa jimbo la Wawi
Mhe. Hamad Rashid Mohd.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar amesema Tanzania imekuwa ikipita
katika kipindi kigumu cha migogoro na uvunjifu wa
amani, mambo ambayo yanapaswa kupigwa vita ili
kurejesha hali ya amani na kuvumiliana.
Amedai kuwa chanzo kikuu cha migogoro ya kijamii
ikiwemo ya ardhi na mizozo ya kidini inatokana na
kutokuwepo kwa mikakati imara ya kuendesha nchi,
na kwamba viongozi wanapaswa kujifunza kutokana
na migogoro hiyo, ili kuweka mikakati imara ya kuendesha
nchi kwa uhakika.
“Nchi haiendeshwi kwa kuigiza, bali kwa kuwa na
viongozi wenye dira ya mabadiliko kwa maendeleo
ya wananchi”, alisisitiza Maalim Seif.
Amesema kutokana na viongozi kutokuwa na dira na
mikakati imara ya kuendesha nchi, Watanzania
wameshindwa kunufaika na rasilimali za nchi yao ambazo
ni nyingi na zinaweza kuwabadilisha kiuchumi.
Amefafanua kuwa iwapo wananchi watanufaika moja
kwa moja na rasilimali zao, wataweza kuzitunza na
kuzilinda ili ziwe endelevu, na kwamba kinyume
chake ni kuzihujumu rasilimali ambazo watahisi
haziwanufaishi.
“Popote pasipo na haki hakuna amani, tunataka
kila Mtanzania ajihisi kuwa ana haki sawa katika nchi
hii, sio kuwa na raia wa madaraja, yaani daraja la kwanza,
la pili na la tatu”,alifahamisha huku akishangaliwa na
umati wa watu waliojitokeza kwenye mkutano huo.
Katika hatua nyengine, aliyekuwa katibu mwenezi wa
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA
katika tawi la Chuo Kikuu Dodoma bw. Joseph Christian
amejiengua katika chama hicho na kujiunga na CUF.
Akizungumza katika mk
utano huo bw. Joseph amesema ameamua kujiengua
CHADEMA na kujiunga na CUF kwa madai kuwa
chama hicho kimekuwa kikiendeshwa kwa misingi ya
undugu na ukabila, na kuwatelekeza vijana wenye lengo
la kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini.
Amewatahadhamisha vijana kuwa makini na sera za chama
hicho na kuacha kukurupuka kuvamia sera
za vyama wasivyovifahamu.
Nae Mwenyekiti wa ADC Wilaya ya Kinondoni
Bw. Saburi Mtoro, ambaye pia ameamua kukihama
chama hicho na kujiunga na CUF amemuahidi Katibu Mkuu
wa CUF kuwa wanachama wote wa ADC katika
Wilaya hiyo watajiunga na CUF.
Chanzo: ZanziNews
No comments :
Post a Comment