Sunday, October 21, 2012
Na A. K Simai
Waingereza walipotaka kuwalemaza wananchi wake wasijihusishe na siasa
waliandaa mfumo maalum ambao uliwashughulisha wananchi wengi wa
kawaida na huku wakiwaachia tabaka dogo la mabepari na walio kwenye
matabaka ya juu (upper class) kushiriki siasa.
Walichokifanya ni kuwajengea mazingira ya kupenda michezo kwa ujumla na
hasa mpira wa miguu na kuujengea ushindani mkubwa mpaka imekuwa
ndiyo siasa ya wananchi wa kawaida kuzungumzia mipira kila kona na kila sehemu.
Homa hii siku hizi ipo hata nyumbani ambapo mtoto mdogo anaweza kukuelezea
Pia baada ya pirika pirika za kwenda mbio na maisha siku za wikiendi wamewawekea
sehemu za kujifurahisha kwa vinywaji na miziki ya kila aina ili izidi
kuwasahaulisha na msongamano wa mawazo wa wiki nzima na hivyo kuwa na
muda mchache kuzungumzia siasa za nchi.
Naam waingereza walifanikiwa vizuri sana maana sera hii inazidi kuendelezwa
na huku wanaoshiriki katika maamuzi muhimu na nyeti ya nchi ni kundi la wanasiasa
wachache wanaotoka katika matabaka maalum.
Wazanzibari walipotaka kuwalemaza wananchi wake waliwajengea maskani na
mabaraza ya mazungumzo ili wapate muda mwingi wa kuzungumzia siasa na yanayojiri
huku na kule katika mkondo hatari wa siasa.
Wanasiasa wakaichukua siasa na kuitoa pahala pake inapopaswa iwepo wakaipeleka
sehemu isiyopaswa kuwepo na kumshughulisha kila mmoja wetu na siasa.
Siasa ipo majumbani, siasa ipo barazani, siasa ipo makazini, siasa ipo mitaani,
siasa ipo kanisani, siasa ipo misikitini almuradi siasa wee siasa wee. Ilifika wakati
majirani walishindwa kuzikana kwa sababu ya siasa, ndugu kukhasimiana kwa
sababu ya siasa.
Wanasiasa wakajisahau wakiona muradi umepatikana kila ikizungumzwa siasa
kila kona wao huchekelea na kuendelea na siasa yao bila ya kujali siasa
inayoendelea kwengine.
Siasa hii ya mitaani sasa imekuwa. Mitaani imekuwa hakuwatoshi tena hasa baada
ya kukosa sehemu ya kutoa joto lao tokea vyama viwili vikuu vya siasa kuamua
kuacha tofauti zao za kisiasa walipounda serikali ya umoja wa kitaifa.
Vijana wengi hawana ajira, serikali imeshindwa kujifunza jinsi Uingereza ilivyoweza
kuwadhibiti vijana wake angalau kwa waliokuwa hawana ajira kuwapatia Misaada
( Benefits) wajikimu wakati wakitafuta ajira.
Vijana wengi mitaani ambao ndiyo asilimia kubwa ya wakaazi hawana
vivutio vya kuwapumbaza haswa siku za mapumziko kama ilivyo Uingereza
ambapo wamewekeza katika michezo kwa kiasi kikubwa wakiwa na malengo yao.
Vijana hawa huishia vijiweni na mwishowe kujiundia vikundi vya kihuni kama
ubaya ubaya, mbwa mwitu, kimya kimya na kutishia jina zuri la Zanzibar pamoja
na sifa yake kuwa visiwa vya amani. Wengine, Mola awarehemu, kujiingiza katika
madawa ya kulevya.
Athari za kujionea mambo yanayofanyika katika nchi za nje iwe kwenye televisheni
au kwenye mitandao imewaingia vijana wetu mpaka sasa kukitokea fujo la aina
yoyote basi , usalama, amani hupotea haraka sana, maduka kuvunjwa, mali
kuporwa, vifaa kuharibiwa kwa kile ambacho vijana wamekuwa wakikisubiri tu
kitokee na wao kuanza kazi zao. Mambo haya yalikuwa hayapo Zanzibar, yametokea
wapi? Hili ndilo la kujiuliza kama ni Serikali.
Hivi ni kweli wafuasi wa uamsho ndio wanaovunja Baa na kisha kuonekana
wakigida bia na ulevi hadharani?, Hivi ni kweli wafuasi wa uamsho ndio
waliokwenda kuitia moto maskani mama ya kisonge?, Hivi ni kweli wafuasi
wa uamsho ndio wanaoweka vizuizi katika barabara na kisha kuwapora watu kwa
nguvu? Hivi ni kweli wafuasi wa uamsho ndio waliomkamata na kumkata mapanga
askari wa FFU?
Masuala yote majibu yake yapo kwa suala la kimsingi la serikali kushindwa kuwa
na mfumo wa kuwajengea msingi mzuri kundi la vijana wanaotegemewa kuwa
taifa la kesho. Serikali imevuna ilichokipanda.
Yaliyojiri mwezi wa tano mwaka huu wakati mmoja wa viongozi wa Uamsho
alipokamatwa na Polisi na kuwekwa ndani iliigharimu sana serikali kwa jina la
Zanzibar kutiwa doa, kutumika vyombo vya Dola katika kuleta utulivu na tuliamini
matokeo ya vurugu zile yalikuwa ni fundisho kwa Serikali, Polisi na Uamsho
yenyewe ambayo ilithibitisha kutohusika na vurugu zile moja kwa moja.
Miezi mitano baadae imeonekana kwamba vyombo hivi ima vimefeli katika
mtihani wake uliopita au kimeingia kidudu mtu aliyetaka kujaribu kuirejesha ile
hali ambayo Wazanzibari wengi wanaopenda amani na utulivu wa nchi yao wanaiona
gharama yake kwa vitendo. Kitendo cha kutekwa nyara mmoja katika viongozi wa
uamsho na kuchukuliwa kusikojulikana kimeibua yaliyoibuka kama ilivyokuwa mwezi
wa tano. Mara hii tu angalau makanisa hayakuchomwa au kuharibiwa.
Baada ya siku tatu kiongozi kaonekana na tumesikia kauli yake yaliyojiri wakati
alipotekwa nyara na akihojiwa. Kwa kuwa kauli hizi ni za upande mmoja na
zitazokosa ushuhuda wa upande wa pili zitabakia kwenye miono na maoni tofauti
kwa wenye kuzisikia.
Uamsho wanapaswa kujiangalia tena na kurudi mezani kujitathmini kwa
nia zao njema walizonazo na mazingira au halisi iliyopo na njia zao
wanazozitumia hasa ukiangalia matukio yenyewe yanavyonasibishwa na Uamsho
kwa kuwa tu hisia zinatufanya tuamini hivyo.
Hali ya Zanzibar kwa sasa ni tete sana, tupo katika hatua muhimu ya kukusanya
maoni juu ya Katiba mpya. Hali kama hii itaakisi mawazo, fikra na maoni ya
wachangiaji na hivyo kupelekea kupata mawazo yaliyojaa hisia zaidi kuliko hali halisi
Uamsho ina takriban miaka kumi tokea kuanzishwa kwake. miaka kumi ni
muda mzuri wa kujifanyia tathmini yakinifu.Alhamdulillah Imekuwa ikifanya harakati
nyingi zenye kuleta tija kubwa kwa Waislamu na nchi kwa ujumla kama kushiriki
kikamilifu katika kuunganisha wananchi wa visiwa hivi waondokane na tofauti
za kisiasa na hatimaye kuzaliwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Ila Uislamu ni dini ya amani kama zilivyo baadhi ya dini nyingine, matendo maovu
ya wachache yanaharibu taswira ya Uamsho yenyewe kwanza na baya zaidi
kuharibu taswira ya Uislamu kwa ujumla.
Uislamu ndio unaopigwa vita na si Uamsho kama inavyoonekana kwasababu
ya kupelekea waislamu na uislamu kuingizwa na kujumuishwa kwenye kapu
moja la mambo mabaya.
Mimi binafsi ninakataa katakata kwamba vurugu zilizotokea zimefanywa
na wafuasi wa Uamsho, hawa ni wahuni tu wanatumia fursa na mwanya wanaopewa
na Uamsho katika harakati zake. Mfuasi wa uamsho hana definition ni nani ni
mwanachama (card holder) supporter ( anayewaunga mkono), sympathiser ni
nani hivyo mtu yeyote anaweza kujinasibu na kujilabu kwamba mimi ni Uamsho.
Kwa kuutendea haki Uislamu, nadhani iko haja kwa Uamsho kujaribu kukaa chini
ni kutafakari pamoja na kujitathmini katika mwenendo wa matukio yanayotokea
hapa nchini na jinsi jamii iliyokosa maadili sahihi ya malezi na makuzi inavyojidhihirisha
wakati wa vurugu na fujo.
Chanzo: ZanZews
No comments :
Post a Comment