Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, October 29, 2012

CUF: MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 29/10/2012

UVUNJIFU WA HAKI ZA BINADAMU, MATESO NA MAUWAJI YA WASIO NA HATIA ZANZIBAR, CUF YATOA TAMKO KALI
Written by   //  29/10/2012 
Mkurugenzi wa Haki za binadamu, habari Uenezi na mahusiano na umma - Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma


MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 29/10/2012
SERIKALI INAUKUZA MGOGORO ULIOPO BADALA YA KUUDHIBITI
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwanza napenda kuchukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwenu kwa kukubali wito wa kuja kutusikiliza. Sisi Chama cha Wananchi, CUF, tunatambua na tunathamini mchango wenu mkubwa na jitihada zenu nyingi, katika kusaidia kuhamasisha hali ya amani na utulivu ndani ya nchi yetu. Ni katika kuendeleza hali ya amani na utulivu ndani ya Nchi, suala lililopelekea kukuiteni leo hapa na kukuelezeni kile ambacho sisi tunakiona kuhusiana na hali tete inayoendelea hapa Zanzibar, na Tanzania kwa ujumla.

Ndugu Waandishi,
Naamini mnatambua kuwa Msingi mmoja, Mkuu wa Chama cha CUF, ni kulinda, kusimamia na kutetea haki za binadamu pamoja na kuleta amani, umoja, mapenzi na mshikamano miongoni mwa wananchi wote baada ya kuchoshwa na hali ya uhasama, chuki, migogoro, mifarakano, mapambano na ugomvi wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu hapo kabla. Mpasuko wa kisiasa uliokuwepo, ulisababisha kutokea maafa na mauwaji makubwa ya wananchi na Wana-CUF, wasiokuwa na hatia, zaidi ya 45 mnamo Januari, mwaka 2001, yaliyotekelezwa na Jeshi la Polisi la Tanzania na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, SMZ. 
Kupitia Maridhiano ya Wazanzibari, yaliyoasisiwa na Rais Mstaafu wa awamu ya Sita ya Uongozi wa Zanzibar, Dr Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, ambaye pia kwa sasa ni Makamo wa Kwanza wa Raisi wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, November 5, 2009 ndipo Zanzibar Mpya ya amani, utulivu, umoja na mshikamano ikazaliwa. 
Ndugu Waandishi,
Ndiyo matarajio yetu sote bila shaka kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, SMZ, pamoja na majukumu yake mengine, inawajibika kuwajali, kuwathamini, na kuwalinda Wananchi wote, na mali zao, chini ya Misingi ya Hikma, Haki, Sheria, na Uadilifu. Matumaini hayo ya umma yamekuwa yakizorota na kutoweka kabisa, usoni mwa kila mwenye hisia za kibinaadamu na mpenda haki, ndani na nje ya Visiwa vya Unguja na Pemba, kadiri siku zinavyokwenda, licha ya Nchi kupita katika wimbi la machafuko, hivi karibuni. 
Ndugu Waandishi,
Kiini na chanzo cha hali hiyo bila shaka kinaeleweka, ambapo kama ilivyoripotiwa kutoka baadhi ya Mamlaka za Serikali, machafuko hayo, pamoja na sababu nyengine, yametajwa kutokana na fujo za tarehe 17 na 18 Oktoba, 2012 zlizofanywa na baadhi ya watu au vikundi ambavyo kimantiki kufanya hivyo ni kwenda nje ya busara na utiifu wa Sheria. Fujo hizo zimesababisha uharibifu mkubwa wa mali za umma, wananchi mmoja mmoja na hata vyama vya siasa. Miongoni mwa vitendo hivyo ni kuvunjwa kwa maduka, vyombo vya usafiri, kukatwa miti ovyo na nguzo za umeme, uharibifu wa miundombinu zikiwemo barabara, pamoja na kuchomwa moto Maskani za CCM. Matukio mengine ya kusikitisha na kuhuzunisha zaidi kupitia vurugu hizo ni kuuwawa kikatili kwa Askari Polisi, Koplo Said Abdulrahman, na watu wasiojulikana pamoja na kuuliwa kwa risasi kijana Salim Hassan Mahoja  katika maeneo ya Amani Fresh na watu waliotajwa kuwa wahusika wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama. 
Ndugu Waandishi, 
Jeshi la Polisi likishirikiana na Vyombo vyengine vya Ulinzi na Usalama, vikiwemo Vikosi vya SMZ, limeanzisha oparesheni inayoitwa ya kuwasaka wahalifu na wafanya fujo za tarehe 17 na 18, Oktoba, mwaka huu. Katika kile ambacho kinashangaza sana, ni jinsi oparesheni hizo zinavyoendeshwa na kusimamiwa katika maeneo mbali mbali ya manispaa ya Zanzibar, hususan katika Mkoa wa Mjini Maghribi. Bila shaka pahala popote duniani panapohitajika kufanywa Oparesheni za kuwasaka wahalifu wa aina yoyote, mamlaka husika ndizo zinazobeba dhamana na jukumu la kutumia utaalamu, mafunzo na mbinu zinazoepusha ukiukaji wa haki na kufanikisha lengo lililokusudiwa, kwa kufuata Sheria. Hatimaye ni kuwashika wahalifu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake na anaefikishwa katika vyombo hivyo hutakiwa apate fursa ya kusikilizwa. 
La kushangaza zaidi, Jeshi la Polisi upande wa Zanzibar, likishirikiana na Vikosi vya KMKM, KVZ na JKU wamekuwa wakiliendesha zoezi hilo la kuwasaka wahalifu kwa uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu, vitisho, unyanyasaji wa raia na mauwaji. Matukio ya Zanzibar hayana tofauti kubwa na matukio ya kule Mwanza na Dar es Salaam. Kule Mwanza kamanda wa polisi wa Mkoa huo Libertus Barlow aliuliwa kwa kupigwa risasi siku ya tarehe 13, Oktoba 2012 na hatukuona serikali ikiwaamuru askari wake kufanya uvamizi wa vijiji, uvunjaji majumba, upigaji kiholela wa watu, maonevu ya wanawake, wizi na uharibifu wa mali na mauwaji kama inavyofanyika hivi sasa hapa Zanzibar. Kilichofanyika Mwanza ni msako ulifanyika kitaalamu kwa taratibu za kiupelelezi na kiasi cha watu watano tayari wamekamatwa kwa lengo la kufikishwa katika vyombo vya sheria na kuripotiwa katika vyomba vya habari. 
Halkadhalika katika matukio ya Dar es Salaam hivi karibuni, tuliona jeshi la polisi likishirikiana vyombo vya ulinzi na usalama likitumia mbinu kadhaa kukabiliana na waandamanaji na kuwakamata watuhumiwa wa fujo hizo. Hatukuona vitendo vya uvamizi na mateso ya watu wasio na hatia kwa muda wa siku nne mfululizo kama inavyofanyika hapa Zanzibar. Hatusemi serikali isiwasake waliofanya fujo na wahalifu waliomuua Coplo Said Abdulrahman, iwasake na iwafikishe wahusika wote katika vyombo vya sheria lakini sio watumie kisingizio hicho kufanya hujuma, mateso, unyanyasaji na muwaji kwa wasio na hatia ambao wengi ni wafuasi wetu wa CUF. 
Ndugu waandishi,
Tokea tarehe 25 Oktoba 2012 jeshi la polisi na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama kwa hali ya utumiaji mkubwa wa nguvu limekuwa likivamia maeneo ya Amani, Magogoni, Daraja-bovu, Mwanakwerekwe, Mtoni, Kinuni, Kwamtipura, Mboriborini, Kilimahewa, Mpendae, Mikunguni, Nyerere, Kwarara, Tomondo na Nyarugusu ambapo hufanya msako nyumba hadi nyumba, na barabarani, kuwapiga, kuwatesa, na kuwakamata raia wasiokuwa na hatia bila ya kujali na kuiheshimu Sikukuu ya Iddi. Majumba yanavunjwa na waliomo ndani kuvamiwa na kuteswa. Kituo cha ushoni cha kuwaendeleza mayatima Bububu (JUDAMA) kilivamiwa na watoto wa kike mayatima kupigwa vibaya. Wengine walipigwa na kuchukuliwa wakiwemo Khalid Shindano na Suleiman Kichwa. Wengine walikamatwa na kunyolewa ndevu zao hadharani. Pia yuko aliepigwa hadi kupoteza maisha. Waliokamatwa na kunyolewa ndevu ni pamoja na Khamis Khatibu na Moh’d Omar wote wa Fuoni. 
Ndugu waandishi,
Chama cha CUF kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kijana aitwae Hamadi Ali Kaimu, mwenye umri wa miaka 22, mkaazi wa Nyerere. Kijana huyu akiwa yuko katika shughuli za kulisha ng’ombe wake huko kwao Nyerere alivamiwa siku ya Ijumaa ya tarehe 26/10/2012 siku ya Idi Mosi na vikosi hivyo vya ulinzi na usalama wakiendeleza zoezi lao la kusaka wahalifu. Kijana Hamadi alipigwa vibaya sana hadi kupoteza maisha. Baada ya wazee wake kumtafuta katika vituo mbali mbali vya polisi hawakufanikiwa kumpata ndipo walipokwenda kumtafuta katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja. Baada ya kukosa taarifa zake sehemu ya mapokezi lakini walielekezwa wende chumba cha maiti na ndipo walipogundua kijana wao, Hamad Ali Kaimu ameshafariki huku mwili wake ukiwa na majeraha sehemu mbali mbali.
Walioathirika na vipigo vya uvamizi huo mpaka siku ya Jumapili ya tarehe 28/10/2012 ni wakiwemo hawa wafuatao:
Baadhi ya waliovamiwa na kupigwa vibaya
JINAPAHALA ALIPOPIGWA
1.Juma AbdiDukani Bububu
2.Khamis (Mshona viatu)Dukani Bububu
3.Asma na watoto wakeNdani ya nyumba yao Bububu
4.Juma na mke wakeDukani Bububu
5.Kocha TaibuDukani Bububu
6.Muuza magazetiBarabarani kazini kwake Bububu
7.Ali  Yussuf ChokiDukani Bububu
8.Ubwa na wateja wakeGareji Bububu
9.Shamis AmiriDukani Bububu
10.Mtoto mdogo wa miaka mitatu (3) wa Bi Salma FakiNyumbani kwao Bububu
11.Zahor KhalfanBububu
12.AhmedBububu
13.Mashavu MbaroukBububu
14.Khalfan Moh’dBububu
15.Suleiman Ali AlawiBububu
16.Ali SuleimanBububu
17.Said SuleimanBububu
18.Salma AbdallaBububu
19.Raya Moh’d (Robo)Bububu
20Ali Abdalla SalehBububu
21Salum RazaBububu
22.Khalfan Abdalla AliBububu
22.Nayadi Moh’dKikwajuni
23.MirajiJang’ombe

Ndudu waandishi,
Chama cha Wananchi, CUF kinalaani kwa nguvu zake zote vitendo vya fujo na uvunjifu wa amani vilivyofanywa siku ya tarehe 17 na 18 Mwezi huu viliyoambatana na mauwaji ya Coplo Said Abdulrahman, sambamba na hilo kilanaani kwa nguvu zote na kusikishwa mno na mauwaji, vipigo, uonevu, unyanyasaji, mateso kwa raia wasio na hatia, kurejeshwa kwa hali ya chuki, uhasama, kupaliliwa kwa vitendo vya ubaguzi baina ya uunguja na upemba. CUF inalaani azma ya kuwanyanyasa wananchi na hujuma hizo zilizopindukia mipaka zinazohamasishwa na baadhi ya Watendaji wa Vikosi na Vyombo vya Dola, kwa utashi na maslahi binafsi. Tunaamini vitendo hivi vinatoa fursa pana kwa wale ambao hawautaki umoja wa wazanzibari na kutoitakia mema Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar. 
Ndugu waandishi,
Chama cha Wananchi, CUF, kinalaani azma na vitendo vyote hivyo vinavyoiweka haiba ya Nchi katika hali ya machafuko, wakati ambao Wananchi wamekuwa watulivu licha ya hali tete ya kisiasa. Wazanzibari wengi tayari wameshapoteza maisha huko nyuma tutokako na wengine kuachwa na ulemavu wa maisha kupitia hujuma kama hizi zinazofanywa na askari wetu kwa visingizio hivi na vile. Sisi tunadhani hayo yametutosha na ndio tukaamua kuingia katika enzi mpya ya Maridhiano, yaani kuishi kwa amani, utulivu na kuheshimiana. CUF inaamini Vitendo hivyo bila shaka havitatui mgogoro na tatizo lililojitokeza bali ni uvunjifu wa haki za binadamu na vinapalilia zaidi hasama na kushawishi mwendelezo wa uvunjaji wa amani. 
Chama Cha wananchi CUF, kinamtaka Kamishna wa Jeshi la polisi Zanzibar, Bwana Mussa Ali Mussa kuhakikisha anakomesha vitendo vyote vya unyanyasaji vinavyofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia wasio na hatia na hapo hapo kuwachukulia hatua wale wote wanaotenda unyanyasaji huo. Chama cha wananchi CUF kinamtaka waziri wa nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mhe Mohammed Aboud Mohammed kuhakikisha serikali inaheshimu haki za raia wake chini ya misingi ya utawala bora. 
Pamoja na kuiwacha Sheria ichukue mkondo wake, ni vyema Serikali na Vyombo vyake vya Dola kutekeleza wajibu na majukumu yao kwa kuzingatia sheria, haki, hikma na uadilifu, bila kuwahujumu na kuwasumbua Wananchi wasi na hatia, ikieleweka kuwa wao ni sehemu muhimu ya maisha na raia halali wa Nchi hii.
Naomba kuwasilisha.
HAKI SAWA KWA WOTE
Salim Bimani
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma


Baba wa Marehemu Hamadi Ali Kaimu aliyeuliwa na vipigo vya jeshi la polisi siku ya Idi mosi
Chanzo: Mzalendo

No comments :

Post a Comment