Pamela Chilongola
Mwananchi
UONGOZI wa kiwanda cha kutengeneza dawa za kupunguza makali ya Ugonjwa wa Ukimwi (ARV) cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI), umesema hautasitisha uzalishaji wa dawa hizo kwa kuwa hauna barua inayowakataza kufanya hivyo kutoka mamlaka yoyote.
Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku 12 baada ya Serikali kupitia kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi kutangaza kufungia uzalishaji wa dawa hizo katika kiwanda hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa TPI, Ramadhani Madabida alisema jana kwamba kiwanda hicho bado kinaendelea kuzalisha dawa hizo kwa kuwa hakuna barua kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyowataka wasimamishe uzalishaji huo.
“Wenye mamlaka ya kukifungia kiwanda chochote cha dawa na kukithibitisha ni TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania),siyo Wizara ya afya,” alisema.
Alisema baada ya tukio hilo, TFDA iliwataka kwa barua, watoe maelezo ndani ya siku 14 kuhusu mzunguko wa dawa hizo na siyo kusitisha uzalishaji... “Sisi tuliletewa barua na TFDA ambayo ilitutaka tutoe maelezo ndani ya siku 14 kuhusu dawa feki za ARV zilizosambazwa na kudaiwa kuwa ni za kwetu na tuliwaeleza.”
Alisema walifanya hivyo kwa wakati na TFDA iliwahakikishia na kuwathibitishia kuwa hizo dawa hazikutengenezwa katika kiwanda hicho.
“Sisi hatuna uwezo wa uelewa wa utengenezaji wa dawa za ARV bandia zilizokutwa katika mzunguko, wenyewe wanajua zilipotengenezwa na si hapa, ni nje ya nchi na wanafahamu kinachoendelea,” alisema Madabida.
Alisema kiwanda hicho kinazalisha dawa hizo kama kawaida na hawana kitu cha kuwakwaza kutoendelea na uzalishaji.
Alisema wanatarajia kuongeza uzalishaji kwa asilimia 70 na Desemba mwaka huu wanatarajia kuzindua kiwanda kipya ambacho kitakuwa kikifanya kazi chini ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na kitakapokamilika, kitakuwa na uwezo wa kuuza dawa hizo ndani na nje ya Tanzania.
Pia alisema wanachukua hatua zao na kuhakikisha umma unaelezwa ukweli wa dawa za ARV bandia zilipopatikana.
Hata hivyo, kauli ya Madabida ilipingwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Donald Mmbando aliyesema jana kuwa kiwanda hicho kilipelekewa barua ya kujieleza na kusitisha uzalishaji ndani ya siku 14.
“Tuliletewa nakala ya barua kutoka TFDA ambayo wamemwandikia mmiliki wa kiwanda cha TPI kuwa atoe maelezo ndani ya siku 14 na kusitisha uzalishaji wa dawa hizo… Mmiliki anavyodai hajapewa barua, si kweli,” alisema Dk Mmbando.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFDA, Dk Hiiti Silo na Ofisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Gaudensia Simwanza hawakupatikana jana kutoa ufafanuzi juu ya sakata hilo baada ya simu zao kutopatikana.
Hatua ya TPI kutakiwa kusimamisha uzalishaji wa dawa hizo, ni baada ya kubainika kuwapo kwa dawa bandia katika mzunguko zenye alama ya biashara, TT-VR 30 toleo namba OC.01.85 mwanzoni mwa Septemba mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime baada ya TFDA kufanya ukaguzi.
Akitangaza hatua ya kukifungia kiwanda hicho, Dk Mwinyi alisema baada ya kufanya uchunguzi, walibaini kuwa nyaraka zinaonyesha kuwa TPI ndicho kilichoiuzia MSD ARV bandia.
“Wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi kwa sababu wanatakiwa kufanya uchunguzi wa kile wanachokipokea… Tunachoona hapa ni kwamba uchunguzi haukufanyika sawasawa ndiyo maana tumechukua hatua za kuwasimamisha,” alisema Dk Mwinyi alipokuwa akizungumza Dar es Salaam na kuongeza:
“Matumizi ya dawa hiyo inayotengenezwa na TPI yamesimamishwa na imeondolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya na kurudishwa MSD,” alisema.
Alisema tayari makopo 9,570 ya dawa hiyo yamerejeshwa MSD na kwamba bado makopo mengine 2,600 yapo katika utaratibu wa kukusanywa.
Waziri huyo alisema dawa hiyo ilitengenezwa Machi mwaka huu na muda wa matumizi yake unatarajiwa kumalizika Februari mwakani huku zikiwa na rangi mbili tofauti, njano na nyeupe.
Alisema dawa zilizokuwa na rangi ya njano zilikuwa na kiambata cha Efaverenz badala ya viambata aina ya Niverapine, Lamivudine na Stavudine vilivyopaswa kuwapo.
Dk Mwinyi alisema vidonge vilivyokutwa kwenye vifungashio vya dawa husika vilikuwa tofauti na vifungashio vilivyosajiliwa na TDFA.
|
No comments :
Post a Comment