Mnyika amvaa Waziri Muhonga
5th October 2012
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), alieleza kuwa ufafanuzi uliotolewa na Maswi unatoa mwanya kwa mikataba mibovu kulindwa wakati ambapo kuna madai aliyotoa toka mwaka 2011 kwamba baadhi ya mikataba hiyo imeingiwa kifisadi.
“Tafsiri ya ufafanuzi huo uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini ni kwamba hata kama mikataba iliyopo ina mapungufu yasiyozingatia maslahi ya taifa, matokeo ya mapitio hayo hayatarekebisha mikataba iliyopo bali mikataba ya baadaye,” alisema.
Aidha, alisema taarifa ya Katibu Mkuu huyo ni ya kurudi nyuma tofauti na kauli za awali za Waziri Muhongo zilizokubaliana na madai yake ya mwaka 2011 ndani na nje ya Bunge, ya kutaka mikataba yote ipitiwe upya, isiyozingatia maslahi ya taifa ivunjwe au ifanyiwe marekebisho makubwa na mikataba mipya isiingiwe mpaka kwanza kuwepo sera na sheria bora zenye kulinda uchumi na usalama wa nchi.
Septemba 15, mwaka huu wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC), Waziri Muhongo aliagiza bodi hiyo kuipitia mikataba yote 26 ya utafutaji mafuta na gesi asili ili kujiridhisha endapo maslahi ya taifa yalizingatiwa.
Mnyika alisema kuwa Waziri Muhongo na Katibu Mkuu wake wanapaswa kuendelea kuonyesha kwa maneno na matendo tofauti yao na viongozi waliowatangulia katika Wizara hiyo, kwa kutoa ufafanuzi wa ziada na kuchukua hatua zaidi vinginevyo taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Septemba 21, mwaka huu itakuwa ni mwendelezo wa kulinda udhaifu wa kimfumo uliojikita katika Wizara hiyo na serikali kwa ujumla.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment