Saturday, October 6, 2012
TAMKO LA PAMOJA LA KONGAMANO LA KITAIFA LA KUZUNGUMZIA NAFASI
YA ZANZIBAR KATIKA MJADALA WA KATIBA MPYA, UKUMBI WA SALAMA, HOTELI YA BWAWANI,
TAREHE 06 OKTOBA, 2012
Sisi washiriki wa Kongamano la Kitaifa la Wazanzibari tuliloliitisha kuzungumzia Nafasi ya Zanzibar katika Mjadala wa Katiba Mpya leo hii Jumamosi, tarehe 06 Oktoba, 2012 katika Ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar tunatambua kwamba fursa iliyopo mbele yetu katika Mjadala huu wa Kitaifa ni fursa adhimu ambayo inapaswa kukumbatiwa na kila Mzanzibari Mzalendo katika kuamua Mustakbali wa Zanzibar na watu wake.
Katika kuikumbatia fursa hii, tunatambua,
kuheshimu na kuthamini hatua iliyofikiwa ambapo Wazanzibari kutoka makundi na
taasisi tofauti wameungana na kuja pamoja katika kusimamia na kuendesha
harakati zenye lengo la kuirejesha Zanzibar yenye mamlaka kamili kitaifa na
kimataifa itakayofuatiwa na mashirikiano ya Muungano wa Mkataba kati yake na
Tanganyika.Sisi washiriki wa Kongamano la Kitaifa la Wazanzibari tuliloliitisha kuzungumzia Nafasi ya Zanzibar katika Mjadala wa Katiba Mpya leo hii Jumamosi, tarehe 06 Oktoba, 2012 katika Ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar tunatambua kwamba fursa iliyopo mbele yetu katika Mjadala huu wa Kitaifa ni fursa adhimu ambayo inapaswa kukumbatiwa na kila Mzanzibari Mzalendo katika kuamua Mustakbali wa Zanzibar na watu wake.
Hata hivyo, tunaelewa pia kuwa zimekuwepo
jitihada za makusudi za kujaribu kuuvunja umoja huu wa Wazanzibari kwa kutumia
hoja dhaifu zenye lengo la kutuondoa katika mstari ili kuzima vuguvugu la
Wazanzibari.
Hatua ya leo ya kuwa na wasemaji na washiriki
kutoka makundi na taasisi tofauti ni kudhihirisha kwamba njama za kutugawa
tutazishinda kwa njia za amani na za kidemokrasia.
Kutokana na hali hiyo, ndiyo leo hii tumeamua
sisi Wazanzibari tunaotoka makundi na taasisi tofauti lakini tunaounganishwa na
UZANZIBARi na imani yetu kwamba wakati umefika wa ZANZIBAR kurejesha mamlaka
kamili kitaifa na kimataifa, kutoa tamko LIFUATALO.
KWAMBA umoja wetu ndiyo nguvu yetu na ngao yetu,
hivyo tumeamua kuunganisha nguvu zetu katika kusimamia madai halali ya
Wazanzibari na kwamba tunakataa njama zote za kutaka kutugawa ili kuendeleza mipango
ya wasioitakia mema Zanzibar ya kutaka kuendelea kuidhibiti.
KWAMBA tutaendeleza harakati hizi za Wazanzibari
kwa njia za amani na za kidemokrasia.
KWAMBA hatutositisha harakati zetu za amani na kidemokrasia hadi lengo la ZANZIBAR yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa litimie, na kwamba juhudi zozote za kutaka kubadilisha matakwa ya Wazanzibari kwa kuwakisia na kuwakadiria cha kuwapa hazitokubalika. Tunachokisimamia ni HAKI yetu na si OMBI au fadhila kutoka kwa yoyote.
KWAMBA tuna imani na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa chini ya Raisi Muheshimiwa Dk. Ali
Mohammed Shein na pia tunaimani na viongozi wetu. Na tunaamini Serikali yetu na
viongozi wetu hao ni wazalendo wa Zanzibar na kwamba ridhaa yao imetoka kwa
wananchi wa Zanzibar. Hivyo basi, tunaamini na kuwategemea kuwa kama
wanavyoendelea kutuahidi watasimamia na kutetea matakwa na maamuzi ya
Wazanzibari walio wengi.
KWAMBA tunatoa wito kwa Jumuiya ya kimataifa
kufuatilia kwa kina mchakato wa katiba mpya na kufuatilia matakwa ya
Wazanzibari wanayoyatoa katika mijadala mbali mbali inayoendelea. Tunaitegemea
jumuiya ya kimataifa hatimae iunge mkono matakwa ya Wazanzibari yanayotolewa
kwa njia ya amani na kidemokrasia.
KWAMBA Zanzibar tunayotaka kuiona ni Zanzibar itakayojengwa chini ya misingi YA UHURU, USAWA, DEMOKRASIA, UVUMILIVU, HAKI ZA BINAADAMU, AMANI NA UJIRANI MWEMA, NA YENYE MAISHA YA NEEMA KWA WATU WAKE WOTE.
ZANZIBAR KWANZA
Limetolewa leo
Tarehe 06 oktoba 2012
ZANZIBAR.
No comments :
Post a Comment