November 26, 2012
Toleo la 269
21 Nov 2012
VIOJA vilivyozuka Zanzibar siku mbili hizi, na hasa baada ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) huko Dodoma, vimewashangaza wengi na kufungua ukurasa mpya katika historia ya visiwa vyetu…
Tukiviangalia kwa darubini ya mchakato unaoendelea wa kulitafutia taifa Katiba Mpya, ni wazi kwamba Wazanzibari wana mawili ya kuchagua. Imma waendelee na mfumo uliopo sasa wa Muungano wao na Tanganyika ukiendeshwa na Serikali mbili au wawe na mfumo mpya wa Muungano utaoirejeshea Zanzibar mamlaka yake kamili, lakini utaokuwa juu ya msingi wa Mkataba.
Kusema kwamba mfumo wa sasa wa Muungano ni mfumo bora duniani na wa kupigiwa mfano, ni kuikanyaga hali halisi ilivyo. Ni kusema uwongo; ni uzandiki mtupu! Kuhoji kwamba hatuwezi kuwa na Muungano wa Mkataba kwa sababu hakuna mfano wake duniani, ni hoja dhaifu sana na isiyo na mantiki.
Wazanzibari wengi walishangaa walipowasikia baadhi ya viongozi wa Serikali yao ya Umoja wa Kitaifa wakishikilia kwamba Muungano uendelee vivi hivi ulivyo. Kwa kushikilia hivyo wanakuwa wanapinga Zanzibar isirejeshewe mamlaka yake ya utawala ambayo kwa sasa yamehaulishwa Bara yakiwa chini ya mwavuli wa yale yaitwayo ‘Mambo ya Muungano.’
Labda jambo linaloshangaza zaidi ni kuwaona viongozi hao wakiung’ang’ania huu muundo wa sasa i-lhali umeshindwa kwa miaka 48 kutanzua migogoro iliyojitokeza kwa muda wote huo, na itayoendelea kujitokeza, baina ya sehemu mbili hizi za Muungano.
Migogoro hiyo ndiyo ile ambayo huitwa ‘kero za Muungano’ katika jaribio la kuifanya ionekane kuwa ni mambo yasiyo na maana au umuhimu, mambo madogo ya kipuuzi tu! Wazanzibari wanaielewa sera rasmi ya CCM kuhusu muundo wa Muungano. Ni msimamo wenye kukataa kuzitia maanani hisia na haki za kimsingi za wananchi wengi wa Zanzibar.
Tumewashuhudia wananchi hao wakizielezea hisia zao wakati walipokuwa wakitoa maoni yao kuhusu Muungano wautakao. Tumewasikia wengi wao wakisema kwamba ingawa hawataki kuuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hata hivyo, wanahisi kwamba njia pekee ya kuizika migogoro iliyopo ni kuubadili muundo wa Muungano.
Wanachotaka ni kila moja ya nchi hizo mbili irejeshewe mamlaka yake kamili ya utawala. Lengo, wanasema ni kuzifanya nchi zote mbili ziwe na usawa, zikiwa zimeungana na kuwa na Muungano wa Mkataba.
Kilichowafanya Wazanzibari washikwe na fadhaa, na kilichowachekesha wengine si ukaidi wa CCM wa kutobadili au kulainisha sera zake kulingana na maoni ya Wazanzibari wengi. Ukaidi huo ukijulikana. Hakuna aliyetaraji vingine!
Kilichowapiga butwaa ni matamshi ya ujuba yaliyotolewa bila ya woga na baadhi ya viongozi wa CCM. Hawa ni viongozi ambao kwa bahati mbaya hadi hii leo bado hawawezi kutofautisha baina ya majukumu ya vyama vya kisiasa na yale ya kidola katika mfumo wa kidemokrasia wenye vyama vingi.
Jingine ni jinsi viongozi hao walivyowatumia (na kuwatia moyo mkubwa) wanachama wa kawaida wa CCM ili wamkashifu kwa izara na matusi yasiyosemeka Amani Abeid Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa Chama chao wenyewe. Walionyesha utovu wao wa adabu kwanza Dodoma wakati Amani Karume alipokuwa akitoa hotuba yake ya kustaafu Umakamu Mwenyekiti wa CCM.
Baadaye, ndipo walipowatumia wanachama wa kawaida walioandamana kwa shangwe, huku wakipiga bendi kwenda kulikokuwa kumetundikwa mabango ya picha za Amani Karume na kuyabandua na mapicha kuyachana.
Wazanzibari wanahisi kwamba Karume amefanyiwa yote hayo kwa sababu ya uzalendo wake wa Kizanzibari. Wanamuona kuwa ni kiongozi anayewataka Wazanzibari wenzake waiweke nchi yao mbele badala ya vyama vyao vya kisiasa wanapoyazingatia maslahi ya Zanzibar.
Zaidi kwamba anawataka wawe wamoja na waiendeleze hali ya amani na utulivu wa kisiasa Visiwani. Gazeti la kiungwana kama Raia Mwema haliwezi kuyakariri maneno ya matusi na kashfa yaliyoandikwa kwenye vipeperushi vilivyosambazwa Zanzibar dhidi ya Karume.
Ni matamshi yasiyo na haya wala staha. Yanakirihisha, yanatapisha na hayastahili kutamkwa dhidi ya wapinzani, seuze dhidi ya viongozi wake wenyewe wa hicho chama kinachojinata kuwa ni cha uadilifu. Hivi ni vitendo vya kihayawani ambavyo labda vinaashiria mwanzo wa kuangamia kwa CCM, na ni vitendo vyenye kukifanya chama hicho, badala ya kuwa Chama Cha Mapinduzi, kijulikane kuwa Chama Cha Matusi.
Kwa bahati nzuri, enzi ya mfumo wa chama kimoja tu cha kisiasa kilicho halali imekwisha nchini mwetu. Inavyotakikana ni kwamba nchi hii isiwe tena na viongozi wachache wenye kuwashurutisha walio wengi kuzifuata sera wasizozipenda.
Viongozi wa Kizanzibari waliojitokeza hadharani wakitumia vyombo vya dola na mali za dola kufanikisha malengo yao ya kisiasa ya chama chao, katu hawawezi kutambua kwanini Wazanzibari wenzao wanataka mabadiliko.
Aidha, ni dhahiri kwamba wanajidanganya au wanajipotosha wakiamini kwamba mambo yote yatakuwa shwari ikiwa mwaka 2015 patapatikana Katiba Mpya itayouhifadhi muundo uliopo waMuungano. Kwa hakika, kuna wanaojiuliza ikiwa matokeo ya mchakato huu wa sasa yanajulikana tangu sasa, basi kuna maana gani kuwataka Wazanzibari washiriki katika zoezi hili?
Hebu kidogo niugeukie Muungano mwingine wenye kujulikana sana ulimwenguni. Huu ni Muungano ulioundwa Mei Mosi, mwaka 1707, ukiziunganisha kisiasa tawala ya Kifalme ya Uingereza na ile ya Uskochi. Tofauti moja kubwa iliyopo kati ya Muungano huo na huu wetu kwa wakati huu wa sasa, ni kwamba Waskochi, mnamo mwaka 2014, wataachiwa wajiamulie hatima yao katika Muungano huo!
Ni kusema kwamba baada ya miaka 300 na zaidi ya Muungano wao na Uingereza, wananchi wa Uskochi, hatimaye watakuwa na uhuru wa kuamua iwapo wanataka waendelee kuwa katika Muungano huo au la.
Wazanzibari hawakinzwi na wakati katika msako wao wa kutafuta haki zao. Na wala si lazima kwamba haki hizo zipatikane zote kufikia mwisho wa kipindi cha mchakato wa sasa wa Katiba. Juu ya yote hayo, lakini wengi wanaendelea kutumaini kwamba Tanganyika na Zanzibar zitaendelea kupiga hatua za kuelekea mbele kwenye demokrasia ya kweli yenye kuruhusu uhuru wa kusema, wa kutoa mawazo na wa kuchagua.
Chanzo: ZanzibariYetu
No comments :
Post a Comment