Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, November 26, 2012

MANSOOR YUSUF HIMID: ‘Karume, Maalim Seif wamefuzu mtihani wa uongozi Zanzibar’




Mansoor Yusuf Himid, mwakilishi wa Kiembe Samaki, Zanzibar
WIKI iliyopita tuliona jinsi malumbano ya ama kuwa Muunguja au Mpemba  hayana tija wala mwisho mwema, umuhimu wa kumuenzi hayati Abeid Amani Karume kama Baba wa Taifa na leo tuendelee na makala yetu…
Kwa upande mwingine, ujasiri na upeo mkubwa wa Dk Amani Abeid Karume, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (mstaafu) ni kutambua na kukubali kwamba nchi anayoiongoza inaumwa na siasa zake zinakwenda kinyume na dhamira ya kweli ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Pia ni Dk Karume kutokukubali kumuachia mrithi wake maradhi aliorithi yeye, huku akijua kwamba hatua hiyo itamchukiza sana sana kwa baadhi ya wenziwe walio wahafidhina (zealots) pamoja na mazingira hayo magumu, yeye alichukua hatua ngumu lakini sahihi ya kuwataka Wazanzibari wenyewe wafanye maamuzi juu ya hatma ya nchi yao.
Kupitia kura ya maoni Wazanzibar walio wengi waliamua kwa sauti moja kwamba wamechoka na siasa za mivutano na hasama, kiongozi makini na mwema anapaswa kuongoza sio kuongozwa, na huo ndo mtihani wa uongozi, tuseme tusemavyo lakini Dk Karume na Maalim Seif wamefuzu mtihani huo wa uongozi.
Huku kwetu Zanzibar ni dhambi kubwa kumtaja tu kwa vizuri kiongozi wa upinzani, seuze kummiminia sifa, hiyo ni dhambi kubwa zaidi isio na mfano. Humalizii tu kuitwa msaliti wa chama chako na Mapinduzi, bali utaitwa Hizibu (Zanzibar Nationalist Party-ZNP) namba mbili, namba moja akiwa Jamshid mwenyewe (Sultani wa mwisho Zanzibar).
Hizbu likiwa ndo tusi baya na la mwisho kupewa mwanasiasa Zanzibar hasa anayetokana na CCM, lakini ukweli ni kwamba Maalim Seif Sharrif Hamad anastahili kila sifa ya kuacha utashi wa nafsi yake na wa chama chake kwa kuweka maslahi ya Zanzibar mbele, na kukubali dhamira njema ya CCM na hatimaye kushirikiana na CCM kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na kujenga mustakbal mwema wa Zanzibar na kizazi chake.
Siku zikapita, miezi ikayoyoma na hatimaye ni Rais Kikwete yule yule kwa kuthibitisha umakini, busara na wingi wa hekima ya uongozi wake amethubutu, ameweza kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nilimsikiliza kwa makini wakati akizindua Tume ile pale Ikulu Dar es Salaam, kubwa alilotuasa ni kuweka mbele uzalendo na maslahi ya Taifa letu kwa kila mmoja kutoa maoni anayodhani yatasaidia katika kupata Katiba mpya.
Kwetu sisi Wazanzibari Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatugusa katika baadhi ya mambo ambapo kati ya yote hayo kilele cha umuhimu ni suala zima la Muungano ambao umetimia miaka 48 tangu kuundwa kwake mwaka 1964.
Ukelele wa mabadiliko ya muundo wa Muungano ulikuwa katika kila pembe ya viunga vya Zanzibar, kule Mtende, Makunduchi, Kijini, Kibuteni, Jambiani, Ndijani, Uzini, Bambi, Umbuji, Pongwe, Uroa, Chwaka, Mkwajuni, Nungwi, Matemwe, Limbani, Jadida, Wete, Ziwani, Wambaa, Chake Chake ilimradi kila pahala.
Kwa bahati mbaya, tunataka kurudishwa kwenye siasa za chuki, hasama na kutoheshimiana na kuvumiliana hata kwa mawazo, kila anayezungumza kwa kutaka mabadiliko katika mfumo wa Muungano basi tayari ni msaliti wa chama chake na Mapinduzi, utafikiri chama na Mapinduzi ni hati miliki ya baadhi yetu, wengine sote sio, huna haki ukiwa Mtanzania na Mzanzibari kueleza kwa upeo, fikra zako juu ya namna unavyotaka Muungano wako uwe, kwani huu Muungano ni wa Watanzania wote kama hawakusema wao atasema nani? Na kwanini tusiseme ni Haki yetu kusema, Watanzania hatukuwasemea Wakenya wakati wanarekebisha Katiba yao wamesema wenyewe.
Nakubaliana na raia wenzangu na Serikali yangu kwamba katika mchakato huu hatupaswi kukubali kutoa nafasi kwa wanaohubiri utengano, ubaguzi, udini, na matumizi ya lugha chafu na za kibaguzi pamoja na kutumia fujo kama njia ya kufikia malengo yao, na wote wanaofanya hivyo wanapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria kwani tunakotoka kubaya sana, hatupaswi Wazanzibari wenye akili timamu kushabikia vurugu, tutajimaliza wenyewe, maana wazee wanasema vita vya panzi neema kwa kunguru!
Lakini papo hapo sikubaliani hata kidogo na dhamira ya wachache kutaka kuwanyima wananchi wa Zanzibar haki na uhuru wao wa kutoa maoni yao kwa kisingizio chochote kile, iwe vitisho, iwe kushurutishwa na kupangiwa, iwe kwa kubatizwa majina ya uhizibu, usaliti wa Mapinduzi na Chama, kwani naamini hatuwezi kupata Katiba na muundo wa Muungano ulio bora kwa kuviza maoni na matumaini ya watu.
Tukumbuke kuwa kwenye wengi hapaharibiki jambo nami naamini kwa uelewa wa wananchi hakuna jambo litakalokwenda kombo zaidi ya kuhuisha mahusiano ya kale baina ya watu wa Zanzibar na Tanganyika.
Tukifikiri vinginevyo, tutakuwa tunazidanganya nafsi zetu na hatutafika kwani siku zote watu makini hawapaswi kuhofia mawazo ya wenzao kwa visingizio kuwa wanataka kumrudisha Sultan na kuvunja Muungano! Haya ni mawazo tu si risasi wala mzinga, iwe Muungano wa Serikali mbili, tatu, mkataba au mfumo wowote ule mujarab utakaotuondosha hapa tulipo kwenda kuzuri zaidi penye heshima, na tunachohofia nini kwani Wazanzibari tulio wengi Muungano tunautaka na sisemi haya kwa kebehi au kujikosha na kujipendekeza, hapana.
Kama husadiki pita kila pembe ya Zanzibar zungumza na Wazanzibari utapata jibu hilo hilo wapo wenye jazba na machungu yao hao watakwambia bila ya kukuficha kwamba Muungano hawautaki, lakini wengi wape na wachache usiwapuuze, wasikilize. Hatimaye kila mtu anataka kuheshimiwa utu wake tu! Kwani kinachotakiwa na Wazanzibari ni Muungano wa haki, ulio sawa na wa heshima.
Pamoja na maelezo yote haya mimi bado ninaamini kwamba nchi yetu iko kwenye mikono salama ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein na viongozi wenziwe wakuu wa nchi na wasaidizi wao, la umuhimu kwetu Wazanzibari ni kuacha kulalamika sana na kuelewa kwamba tunapaswa kuwasaidia kwa dhati na kuwa wakweli kwa kusimama na ukweli.
Viongozi wa dini, wa jamii na sisi wa siasa tunapaswa kuacha viburi na jazba na kuhubiri na kutenda mema, hata kama yale tutakayoyasema yatachukiza kwa baadhi, lakini yakiwa yenye manufaa kwa jamii na hatma njema ya nchi yetu, basi ndio njia sahihi hiyo na ndio njia pekee ya kuondokana na hali tulionayo.
Siasa za majibizano za kila Jumamosi na Jumapili zinaongeza hofu na sintofahamu tu miongoni mwa Wazanzibari, lugha chafu, matusi, ubaguzi, hasama, udini na uchochezi haujatufikisha popote, wala hatufiki popote, ila tutaendelea kubaki na umaskini wetu na baya zaidi tutajirithisha umaskini wa roho pia.
Haya yatapita kama yalivyopita mengine kwani hufika muda katika maisha ya nchi na watu wake siasa za kuridhiana, kuvumiliana, kuheshimiana na kujenga umoja na maelewano zikaonekana na wachache kuwa ni za udhaifu mkubwa na wanao hubiri siasa hizo kuonekana nao ni watu wasio shupavu, lakini historia inatudhihirishia kwamba hali hiyo haidumu na haijapata kudumu popote duniani, inahitaji moyo na dhamira njema kuondokana nayo.
Wazanzibari tuko wapi, vipi tanataka nchi yetu na Muungano wetu uwe, ni swali ambalo sote tulitafutie jibu na tukumbuke kwa mba Marehemu Abeid Amani Karume alisema, “Angalieni khatma!”
Mwandishi wa makala haya ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki(CCM) Zanzibar
Namba yake ni +255777424305.
Chanzo: ZanzibariYetu

No comments :

Post a Comment