Ujio wa shirika la simu za mkononi la ZANTEL hapa Zanzibar umekuwa wa faraja kubwa na mafanikio mema kwa Wazanzibari walio wengi. Ikiwa ni moja ya shirika la simu linaloungwa mkono kwa asilimia 99.5 na Wazanzibari wote wanaotumia simu za kiganjanai tangu kuanzishwa kwake mapema miaka ya 2000, Zantel inakuwa ni shirika pekee lililofanikiwa kuliteka soko la wateja bila kuyumba hapa visiwani kuliko shirika lolote nchini.
Tunakumbuka kuwa Zantel ilianza visiwani na kufanya kazi kwa miaka kadhaa bila kuvuka maji kuingia bara kwa kile kilichoitwa ‘kipindi cha ukiritimba’ ambao binafsi niliuona ni moja kati ya maafa makubwa yaletwayo na Muungano kwa kila jambo la maendeleo linaloilenga kuinufaisha Zanzibar.
Muhula wa Ukiritimba umekwisha sasa na Zantel imeingia bara huku upendeleo mkubwa wa huduma sambamba na makako makuu na nyadhifa kuu za shirika hilo kuhamishiwa bara. Bila shaka ule ukiritimba ulilenga kuinyang’anya Zanzibar mamalaka haya na kwa sasa hili limefanikiwa.Kimya.
Kuna faida lukuki kwa Zantel kuingia katika eneo la bara ikiwemo ongezeko la wateja na watumiaji wa huduma za shirika hili lenye upendo wa kipekee hapa nchini. Wakati maendeleo kama haya yakizidi kulineemesha Shirika, sisi watumiaji hasa hasa kutoka Zanzibar, na hasa hasa kutoka mashamba na ameneo mengi ya Pemba haturidhishwi na jinsi Zantel inavyotoa huduma.
Ukiachilia mbali kuwa siku hizi hata zile ajira za kulinda minara kuwa hutolewa na kuombwa bara na kwa maana hiyo hata minara iliyojengwa maeneo ya kwetu hulindwa na watu wanaotoka maeneo ya mbali na Zanzibar kwa vile utaratibu wa maombi ya kazi hizi umehaulishwa kwenda bara kwa sasa. Hili naamini si haki lakini tumeshazowea Wazanzibari kunyang’anywa na kudhulumiwa kwa kila jambo ambalo wenzetu wa bara wana mamlaka nalo. Hili tuliache, sio geni.
Zantel, hata unapoikabili kudhamini miradi na masuala madogo madogo yahusuyo maendeleo ya hapa Zanzibar na jamii kwa ujumla inakuwa ngumu kutoa udhamini wa aina hio. Tunatambuwa kwamba ili shirika lidhamini lazima lizingatie faida gani linapata kwa udhamini huo, lakini kwanza naamini miradi mingi inayolengwa kudhaminiwa na Zanatel ina faida nao na jengine ni kuwa hata kama haina faida, kama shirika la ndani ya nchi yetu lilikuwa litowe mchango kwa jamii bila kujali faida na hasara baadhi ya wakati kwani ‘mcheza kwao hutunzwa’. Zantel hili hawalifanyi badala yake, wanadhamini kwa mamilioni ya fedha mashindano kama vile ya Bongo Star Search ambayo mchango wake kwa taifa na jamii sio mkubwa kiivyo.
Kama haya hayatoshi, Zanteli inawabaguwa kwa kiasi kikubwa watumiaji wake kwa kuwanyima huduma muhimu za mawasiliano ya simu na Internet hasa hasa sehemu za vijijini. Kuna maeneo hapa Unguja na Pemba mawasiliano ya Zantel ni mgogoro na hakuna linalofanywa na hata ukiwapigia simu na kuwashauri hupati la kushika. Kuna maeneo hadi leo lazima upande juu ya mti ili upige simu. Kwa nini iwe hivi? Hivi ndio Zantel inatujali kweli?
Baya zaidi, huduma za Internet zinazotolewa na Zantel inaonekana kuwa zinakusudiwa kwa watu wa mjini tu kwa sasa. Kwa sasa Unguja mjini internet ya Zantel haiadimiki na tena ina kiwango kizuri. Chake chake, Konde na Wete kule Pemba internet ya kumwaga. Micheweni kwa Zantel haifanyi kazi na takribani ukanda wote wa Kaskazini mashariki ya Pemba sijui Unguja licha kuzungukwa na minara isiyohisabika kwa sasa. Hudumua hii imelengwa kwa watu wa mjini tu.Hii sio haki.
Kuna siku nilienda katika shirika hili la simu kule Pemba kuomba huduma ya Intenet. Awali niliulizwa ninakoishi na ninakoitaka hiyo huduma. Nilitaja Shamba huko yaani nje ya miji hiyo yenye watu wanaostahikiwa na huduma ya Internet, wastaarabu na walioendelea kuliko sisi. Kabla ya kujibiwa niliulizwa iwapo gari zinafika huko. Nikajibu kuwa hapo Chake chake sikuja kwa Punda wala Baisikeli.
Bada ya mabishano mafupi wakanambia huko mawimbi yao hayafiki ijapokuwa kuna minara kila kona katika eno hilo. Isitoshe walinijibu kuwa hata ingekuwa inaingia, basi hawawezi kuleta Internet kwa mtu mmoja tu. Hapo ikawa wamemaliza. Na kweli sasa inapata mwaka hakuna huduma hii eno lote hilo.
Nionavyo, licha ya kubaguliwa ndani ya nchi yetu tena katika karne ya 21, nashangaa kuona nchi huru kama hii ikiendekeza mambo ya kikale ya ‘Ushamba’ na ‘umji’ ambayo yalipita tangu Azimio la Arusha hapa Tanzania. Nashangaa kuna sababu gani ya kuwa watu wa mjini tu ndio wapewe huduma hizi ilhali watumiaji wa simu wa Zantel wapo kotekote kwa idadi inayolingana mjini na mashamba? Naamini na kwa huzuni na uchungu mkubwa, na kwaniaba ya wateja wengine wote wa Zantel, kwamba bila kutafuna maneno, Zantel haitutendei haki.
Chanzo: Mzalendo
No comments :
Post a Comment