03 Dec 2012
Na Gladness Mboma
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imekanusha kutoa taarifa za kusitisha matumizi ya noti za zamani kwani hakuna sababu za msingi ambazo zingewafanya waziondo mara moja.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na BoT kwenda katika vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilisema kuwepo kwa matoleo mawili ya noti katika mzunguko wa fedha hakuna athari zozote kiuchumi.
Taarifa hiyo imekuja baada ya gazeti moja la kila siku (sio Majira), kudai noti za zamani ambazo mpaka sasa zipo katika mzunguko zinasababisha kuwepo kwa fedha bandia za kughushi.
Benki hiyo ilidai kuwa, uamuzi wa kuingiza noti mpya katika mzunguko wakati zile za zamani zikiwepo, ulilenga kuepuka gharama zisizo za lazima.
“Hakukuwa na sababu ya kuziondoa ghafla noti za zamani ambazo bado zina hali nzuri ya kutumika ili kutoa noti mpya, uamuzi huu ulilenga kuwapunguzia usumbufu wananchi kukimbilia kwenye mabenki ili kutaka kubadilishiwa noti zao.
“Utaratibu huo ni wa kawaida kabisa na unatumiwa na Benki Kuu nyingi duniani kwa sababu hizo hizo, toleo la zamani bado ni fedha halali na zitaendelea kutumika sambamba na zile za toleo jipya hadi zitakapomalizika katika mzunguko kutokana na uchakavu wake na zikifika BoT, hazitarudishwa tena kwenye mzunguko,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, ubora wa noti mpya utengenezaji wake ulizingatia viwango vya kimataifa, kuongezewa ubora na alama za usalama ili kudhibiti watu wanaoghushi pia ni rahisi kutambua noti bandia hivyo kuepuka hasara ambayo mwananchi anaweza kuipata,
Tatizo la noti bandia kuingia katika mzunguko sio la noti zilizopo Tanzania pekee bali lipo katika nchi zote duniani pamoja na zile
zinazoendelea kama Marekani, Canada na Uingereza.
Tatizo la uhalifu wa kughushi noti limekuwepo karne nyingi duniani ambapo kila nchi inatumia kiasi kikubwa cha fedha kupambana nalo.
Chanzo: Majira
No comments :
Post a Comment