Toleo la 270
28 Nov 2012
MSIMU mpya wa chaguzi umeanza barani Afrika. Msimu wa awali ulianza mwanzoni mwa mwaka hadi Oktoba, kwa chaguzi za mabunge au za marais au za mabunge pamoja na marais. Huu msimu mpya ulioanza Novemba, utaendelea hadi mwakani…
Katika msimu wa awali chaguzi zilifanywa Algeria, Angola, Cameroon, Congo-Kinshasa, Misri, Gambia,Guinea-Bissau (uchaguzi wa dharura wa urais), Lesotho, Libya (uchaguzi wa Bunge la Katiba), Mauritius, Congo-Brazzaville, Senegal na Somalia.
Kutokana na hali ya Somalia chaguzi zilizofanywa huko zilikuwa za aina ya kipekee. Wananchi hawakuwachagua wabunge wala hawakumchagua rais. Wabunge waliteuliwa na koo zikiwa ‘wawakilishi’ wa wananchi na halafu wabunge wakamchagua rais.
Chaguzi kadhaa zilizokuwa zifanywe mwaka huu zimeahirishwa. Guinea-Bissau, kwa mfano, ilifanya uchaguzi wa dharura wa kumchagua rais baada ya kufariki Rais Malam Bacai Sanhá lakini imeuahirisha ule wa Bunge hadi mwakani.
Guinea-Conakry imeufuta uchaguzi wa Bunge uliokuwa ufanywe mwaka huu na haijulikani lini utafanywa.
Libya kwa upande wake ingawa ilifanya uchaguzi wa Bunge la kutunga katiba imeuahirisha uchaguzi wa Bunge jipya hadi Mei 8, mwakani. Sitoshangaa pakizuka fujo utakapofanywa uchaguzi huo.
Madagascar iliyokumbwa na misukosuko ya kisiasa imeahirisha nayo uchaguzi wa Bunge na wa urais hadi Mei 8, mwakani. Nchi ya Mali iliyoshuhudia mapinduzi na uasi wa kujitenga kaskazini mwa nchi hiyo ilikuwa iwe na uchaguzi wa urais Aprili na wa Bunge Julai. Chaguzi hizo zimefutwa.
Uchaguzi wa Bunge uliokuwa ufanywe Togo Oktoba sasa utafanywa mapema 2013.
Msimu mpya wa uchaguzi ulianza Novemba 3 nchini Swaziland kwa uchaguzi wa mabaraza ya miji uliofuatiwa Novemba 13 na uchaguzi mkuu na wa urais huko Sierra Leone.
Desemba 2, 2012 Burkina Faso itachagua wabunge. Desemba 7 Ghana nayo itaingia uwanjani kwa uchaguzi wa Bunge na wa urais. Huu wa urais utakuwa na msisimko kwa vile mchuano ni mkali baina ya Rais John Mahama na mshindani wake mkuu Nana Akufo-Addo.
Labda chaguzi zinazosubiriwa kwa hamu na msisimko mkubwa zaidi ni zile zitakazofanywa Kenya, Machi mwakani. Wakenya watajichagulia rais, wabunge, magavana, maseneta, serikali za mitaa na wawakilishi wa wanawake katika mabaraza ya magatuzi.
Ni vigumu kung’amua upepo utavumia upande gani. Swali linalowahangaisha wengi ni: nani atayeibuka mshindi katika uchaguzi wa urais? Ni mapema kutabiri kwa vile miungano ya kisiasa bado ingali inaundwa na kila uchao kunazuka mipangilio mipya ya nani anaungana na nani.
Uchaguzi ujao wa Kenya una funzo kubwa kwa uchaguzi wa 2015 wa Tanzania na hasa kwa Zanzibar kutokana na matamshi ya uchochezi ya baadhi ya viongozi wa CCM wa huko.
Matamshi ya kwamba CCM haitokubali na lazima ishinde Zanzibar hata pakinyesha mvua ya mawe yanaashiria maandalizi ya njama za kufanya ghiliba na magube wakati wa uchaguzi.
Matamshi ya uchochezi ni dalili mbaya. Yanatukumbusha yaliyojiri Kenya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 kadhia ambayo hatima yake ni kufikishwa Uhuru Kenyatta na William Ruto, wanasiasa mahiri na wenye uzito na uwezo mkubwa, mbele ya Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) mjini Hague.
Ni dhahiri kwamba CCM kitakuwa na kazi ngumu katika uchaguzi ujao. Ingawa juu juu mabadiliko ya hivi karibuni katika safu ya utendaji yanaonyesha kama yamebadili taswira ya uongozi ndani ya chama hicho sidhani kama uongozi huo utaweza kupambana vilivyo na changamoto zinazokikabili chama hicho. Changamoto kubwa ni ile ya kuwafukuza chamani vigogo vya CCM vilivyoroa ufisadi.
Kwanza kuna viongozi kadhaa katika safu hiyo ya hao wanaoitwa viongozi ‘wapya’ ambao huko nyuma ama wao wenyewe walituhumiwa kwa ufisadi au walihusishwa na mafisadi wakubwa nchini. Swali ni kuwa je, viongozi hao kweli watakuwa na ujasiri wa kuwang’oa wenzao au watakuwa na ajizi kufanya hivyo na wataendelea kulindana?
Labda wanachama wa CCM wangekuwa na matumaini mema zaidi lau wangepatiwa viongozi ambao kweli ni wapya, walio vijana, washupavu, waso ila waso waa na wenye moyo wa kizalendo. Viongozi kama hao hawatoiogopa milihoi na mishetani mingine ya ufisadi. Siamini kama viongozi aina hiyo hawamo ndani ya CCM. Na kama hawapo basi chama hicho kimekwisha.
Pili sifikiri kama CCM kitaweza kidhati kujisafisha iwapo hakitorejelea maadili mithili ya yale ya enzi za Nyerere hasa yanayohusiana na uongozi. Kwa mfano, iwe mwiko kwa kiongozi kujiingiza katika shughuli Fulani fulani zinazoweza kumtumbukiza katika kisima cha ufisadi. Tena iwe mwiko kwake kuwa na tabia za kihuni kama mathalan kuhutubia umma kwa kutumia maneno ya utovu wa adabu.
Nikiziangazia chaguzi barani Afrika ninaona kuna mambo mawili makuu yanayojitokeza. La kwanza jinsi wagombea wa ubunge na wa urais wanavyotumia fedha, tena fedha nyingi mno, kuwanunua wapiga kura.
La pili nikutokuwako tofauti za kiitikadi miongoni mwa vyama. Tofauti kubwa labda ipo katika nchi kama Tunisia, Libya au Misri ambako kuna mvutano kati ya wenye kutaka tawala ziendeshwe kwa kufuata Shari’ah yaani kwa misingi ya Kiislamu na wale wenye kushikilia kwamba dini zisiingizwe katika mifumo ya utawala.
Kadhalika zimetoweka zile tofauti za jadi kuhusu uchumi baina ya wahubiri wa ubepari na wasoshalisti au wajamaa. Inavyoonyesha ni kwamba Waafrika tumejisahau na tumeukumbatia mfumo wa kiuchumi wa lile liitwalo soko huru licha ya kushuhudia jinsi unavyoangamiza maisha ya watu katika nchi kadhaa duniani.
Kuna mengi ambayo serikali zetu na sisi raia tunayoweza kufanya kubadili namna chaguzi zinavyoendeshwa barani Afrika. Lililo muhimu zaidi ni kuwafanya wanasiasa wetu waachane na tabia ya kuutumia uchaguzi kuwa ngazi ya kuyapandia madaraka kwa lengo la kujitajirisha binafsi badala ya kulitajirisha taifa.
Chanzo: ZanzibariYetu
No comments :
Post a Comment