Ahmed Rajab
SIMON Bolivar alikuwa mwanamapinduzi wa Venezuela aliyeiaga dunia Desemba 17, mwaka 1830 akiwa na umri wa miaka 47. Kuna wanaoamini kwamba alikufa kwa kulishwa sumu. Miongoni mwao ni Hugo Chávez, Rais wa Venezuela, ambaye kwa sasa anatibiwa Cuba baada ya kupasuliwa kwa ugonjwa wa saratani.
Oktoba 7, mwaka huu, Chávez kwa mara ya nne alishinda uchaguzi wa urais. Alishinda licha ya ule msaada wa dola zisizopungua milioni 50 ambazo inasemekana Marekani mwaka huu iliwapa wapinzani wake wamshinde.
Lakini yeye ndiye aliyewatwanga na katika uchaguzi wa magavana uliofanywa Jumapili iliyopita chama chake cha Kisoshalisti kiliongeza idadi ya viti vya magavana ilivyoshinda. Januari, kama atakuwa mzima, Chávez ataapishwa kwa muhula mwingine wa urais wa miaka sita.Chávez anaona fahari kujinasibisha kuwa ni mrithi wa dhati wa Bolivar.Tangu ashike madaraka miaka 13 iliyopita hachoki kukumbusha kwamba siasa zake za ‘Chavismo’ zinalenga kuyatekeleza mapinduzi ya kibolivar.
Vyombo vya habari vya Marekani na vya vibaraka wake vimezoea kumfanyia tashtishi na kumcheza shere Chávez vikimfananisha na bahaluli au Juha Kalulu.Hayo si ya ajabu kwani ni kawaida yao kumkebehi kila kiongozi wa wanyonge anayethubutu kusimama kidete na kwenda kinyume cha ubepari wa utandawazi.
Kwa hakika, Chávez alianza kufanyiwa vitimbwi alipotangaza mara ya mwanzo kwamba atawania urais 1998. Alisema anataka kuijenga upya nchi yake kwa misingi mipya. Wengi walimcheka. Kwa mtizamo wao katika mwanzo wa karne ya 21 Chávez alikuwa mtu mwenye fikra za kizamani zilizopitwa na wakati. Alikuwa mwanamapinduzi wa mrengo wa kushoto aliyekuwa akiungwa mkono na Wakomunisti wachache waliobaki nchini mwake na makundi kama sita ya mielekeo mbalimbali ya kisoshalisti.
Nadhani Tanzania hii leo akisimama mtu na kusema anataka kuurejesha ujamaa ataonekana mwehu — hata akisema kama ujamaa anaoutaka ni wa aina mpya. Itakuwa hivyo kwa sababu wengi wetu tuna fikra finyu na tumezoea kuyumbishwa na wimbi litokalo nchi za kimagharibi.
Cháveza na mbwembwe za aina yake.Pia ana mtindo wa aina yake wa uongozi ulio na dosari zake lakini wenye kumpa haiba kubwa. Si watu wote wenye kumpenda. Maadui zake wanasema ulimi wake hauna akili. Hauna ubongo.
La muhimu ni kwamba yeye ni miongoni mwa viongozi wachache wa dunia hii wenye kuwajali watu wao. Ni kiongozi ambaye Bara la Afrika halikujaaliwa kumpata. Inasemekana kwamba nchi yake ni ya tano, ikiwa pamoja na Finland, yenye wakaazi wenye furaha mno duniani. Hayo si mafanikio madogo.
Chávez ameweza kuupunguza ufukara kwa hatua mbili muhimu: ya kwanza ni kulitaifisha Shirika la Taifa la Mafuta la Petróleos de Venezuela (PDVSA) na ya pili ni kuugawa kwa haki utajiri wataifa na sio kuwanufaisha wachache tu katika jamii. Umasikini umeporomoka kutoka asilimia 70.8 katika 1996 na sasa ni chini ya asimilia 21.
Ufukara wakutupwa umepungua kutoka asilimia 40 katika 1996 na kufikia sasa kasoro ya asilimia saba. Mwaka 1990 asilimia 7.7 ya watoto walikuwa wakifa kutoka na utapiamlo lakini sasa takwimu hiyo imeshuka na kuwa asilimia 2.9.
Tangu Chávez awe rais idadi ya wasio na ajira imepungua kutoka asilimia 11.3 na kuwa asilimia 7.7. Katika kipindi cha miaka 10 uchumi wa Venezuela umetanuka kwa asilimia 47.7 na leo uchumi huo ni madhubuti kushinda uchumi wa Marekani na nchi kadhaa za Ulaya.
Kuna mafanikio mengine ambayo Venezuela imeyapata ikiongozwa na Chávez. Wazee zaidi ya milioni mbili na laki moja wanalipwa malipo ya uzeeni na idadi hiyo inazidi kuongezeka. Kabla ya Chavez watu 387,000 tu ndio waliokuwa wakilipwa malipo hayo.
Elimu ni bure kutoka ya chekechea hadi ya chuo kikuu. Wananchi milioni tano wanalishwa bure na serikali. Venezuela haina watoto masikini wa mitaani au chokora kama wanavyoitwa Kenya. Dawa zinapatikana kwa bei rahisi. Venezuela pia ina maduka mahsusi yenye kuwauzia watu wa chini vyakula na vitu vingine kwa bei za chini.
Swali la kujiuliza ni: Ilikuwaje Venezuela chini ya Chávez ikaweza kupiga hatua kubwa hivyo katika muda mfupi? Huenda ukajibu kwamba nchi hiyo inachimba na kusafirisha mafuta na hivyo inajipatia mapato makubwa. Lakini Afrika ya Kusini, Algeria, Angola, Chad, Cameroon, Congo-Brazzaville, Congo-Kinshasa, Cote d’ Ivoire, Equatorial Guinea, Gabon, Ghana, Misri, Morocco, Nigeria, Tunisia, Sudan na Sudan ya Kusini zote hizo zinachimba au zinachimba na kuuza mafuta lakini wengi wa watu wa nchi hizo wanaishi maisha ya dhiki na usumbufu mkubwa.
Alipoingia Ikulu mara ya kwanza 1998, Chávez aliingia akiwa na kikapu cha ahadi akilini mwake. Aliahidi kwamba ataufyeka ufisadi uliokuwa ukiila nchi yake kama unavyoila Tanzania. Aliahidi kwamba atakuwa na sera mbadala kwa nchi yake, sera ambayo itajitenga kabisa na ile ya uchumi wa kiliberali mamboleo iliyokuwa ikifuatwa nchini humo na ambayo sisi Tanzania na kwingineko Afrika tumeing’ang’ania.
Badala ya kutegemea zile ziitwazo ‘nguvu za soko’ na utandawazi serikali yake ikaanza kupanga maendeleo ya nchi kwa kutumia rasilimali zake na sio kwa kuwategemea wawekezaji. Kadhalika, Chávez alizivunja nguvu Shirika la Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) na Benki Kuu ya Dunia katika uendeshaji wa uchumi wa nchi yake.
Alichofanya ni kuthibitisha kwamba kuna sera mbadala za kiuchumi zinazoweza kufuatwa na nchi kama zetu badala ya hizi tunazozikumbatia.
Jengine alilolifanya Chávez ni kuwa macho na kutoipa Marekani nafasi ya kuichezea nchi yake kinyume cha wafanyavyo viongozi wetu. Kwa mfano, amekataa kuziruhusu ndege za Marekani kuingia katika anga ya Venezuela kwa kisingizio cha kuwafukuzia wenye kufanya biashara haramu ya mihadarati. Viongozi wetu wanaipa Marekani fursa hiyo kwa kisingizio cha kuwafukuzia magaidi.
Makala hii imechapishwa katika Gazeti la Raia Mwema
Makala hii imechapishwa katika Gazeti la Raia Mwema
No comments :
Post a Comment