Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia
wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika mkutano wa
hadhara uliofanyika viwanja vya Alabama,
Michenzani Mjini Zanzibar.
Wafuasi na wapenzi wa CUF wakimsikiliza Katibu Mkuu
wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad wakati
akiwahutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika
viwanja vya Alabama, Michenzani Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma na Haki
za Binaadamu wa CUF, Salum Bimani akiwahutubia
wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika mkutano
wa hadhara uliofanyika viwanja vya Alabama,
Michenzani Mjini Zanzibar.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Hamad
Massoud Hamad akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa
Chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika
viwanja vya Alabama, Michenzani Mjini Zanzibar.
ZANZIBAR 06/12/2012.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif
Hamad ametoa wito kwa Mwenyekiti wa Tume ya Kuratibu Maoni
ya Wananchi juu ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba
na tume yake kuweka bayana muundo wa Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya yatakayo jadili maoni ya wananchi, ili kuepusha Mabaraza
hayo kutawaliwa na wajumbe wa chama kimoja.
Maalim Seif alisema hayo jana huko katika viwanja vya Alabama
Michenzani, wakati alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara
ulioandaliwa na chama hicho, ikiwa ni siku moja kabla ya Tume
hiyo ya kuratibu maoni ya wananchi juu ya mabadiliko ya Katiba
kuanza kazi hiyo katika Wilaya ya Mjini hii leo tarehe 06/12/2012.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
alisema baada ya hatua hiyo ya kuchukua maoni ya wananchi
kukamilika, tume itarudi ofisini kuyajadili na baadaye yataundwa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ambayo pia yataweza kujadili maoni
hayo ya wananchi, kabla ya kuchukuliwa hatua nyengine.
Alisema kuwa lazima kuwe na uwazi na wananchi waelezwe Mabaraza
hayo yataundwa na wajumbe wepi, ili kuondoa dhana mbaya inayoweza kujengwa na wananchi kuwa wajumbe hao watatoka katika chama
kimoja cha siasa.
Alisema dhana kama hiyo ikijengeka inaweza kusababisha dosari
katika mchakato mzima wa mabadiliko ya Katiba, hivyo tume hiyo
ichukue hatua za makusudi kulitolea ufafanuzi suala hilo.
“Mheshimiwa Warioba lazima muwe wawazi, hadi sasa Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya hapana anayejua muundo wake, vyenginevyo unaweza
ukakuta wajumbe wote wanatoka katika chama kimoja”, alishauri
Maalim Seif.
Aidha, Maalim Seif alisema uwazi pia unahitajika wakati wa kuundwa
kwa Bunge la Katiba, ambapo mbali ya Wabunge wote na Wawakilishi
wote kuwa wajumbe kuna wajumbe wengine 164, ambao watateuliwa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa ushirikiano na Rais wa Zanzibar,
lakini hadi sasa utaratibu gani utatumiwa kuwapata wajumbe hao
haufahamiki.
Alisema ili kujenga imani kwa wananchi na kuepusha dhana mbaya
itahitajika uadilifu mkubwa kwa Rais, hasa kwa wale watakaotoka
Zanzibar basi kuna haja wawe angalau 55, na vile vile wasitoke
katika chama kimoja cha siasa.
Aidha, Maalim Seif alisema hata katika suala la kura ya maoni
itakayokuja kufuatia huko mbele, bado kuna masuala mengine
ya kujiuliza, kuhusu utaratiubu upi utatumika, wakati wa kura
hiyo kwa Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara na watu wa Tanzania
Bara wanaoishi Zanzibar.
Alieleza kuwa hofu hiyo inakuja kwa vile sheria ya mabadilikko ya
katiba inasema mabadiliko hayo yatapitishwa, iwapo angalau nusu
ya wananchi wa kila upande kati ya Tanzania Bara na Zanzibar wataunga
mkono mabadiliko hayo, hivyo amehimiza mambo hayo lazima kwanza
yawekwe wazi.
Kuhusu maoni ya wananchi juu ya mabadiliko ya Katiba, Maalim Seif
ametowa wito kwa Wazanzibari kutoa maoni ambayo yatazingatia zaidi
maslahi ya Zanzibar, na kusema kuwa mfumo wa Muungano wa serikali
mbili uliopo sasa kamwe hauwezi kuleta ufumbuzi wa matatizo ndani ya Muungano yaliyodumu tokea Muungano huo ulipoanzishwa.
Aidha aliwafahamisha wananchi hao kuondokana na dhana ya serikali
mbili kwani haina maslahi ya nchi kwani hata rais wa Zanzibar huwa
anabezwa katika kufanya baadhi ya maamuzi kwa nchi yake.
“Mimi sina haja ya kuficha wala kutafuna maneno, mimi ni muumini wa Muungano wa Mkataba, maana ni imani yangu kuwa muundo wa
Muungano huu tuliuonao hauwezi kuondoa kasoro zilizopo hadi kiama”,
alisema Katibu Mkuu wa CUF.
Alitoa wito kwa wananchi katika Wilaya ya Mjini kujitokeza kwa wingi
kwenda kutoa maoni kuanzia leo, na wasikubali kudanganywa na baadhi
ya watu wanaotoa fedha kuwarubuni wakatoe maoni, kama
wanavyowaelekeza wao.
Mapema, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma na Haki za Binaadamu
wa CUF, Salum Bimani aliwataka Wazanzibari kuweka mbele maslahi
ya Zanzibar katika zoezi la kutoa maoni ya katiba na kuweka kando
itikadi zao za vyama vya siasa.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Hamad Massoud Hamad,
kwa upande wake amesema Chama hicho kimezidi kuimarika kuliko
wakati wowote tangu kuanzishwa kwake, na kuwaomba wananchi
waendelee kukiunga mkono ili kutimiza malengo yake ya kutetea
maslahi ya Zanzibar ndani na nje ya nchi.
Hassan Hamad (OMKR).
Chanzo: Vijimambo
No comments :
Post a Comment