NA MWANDISHI WETU
2nd December 2012
Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato (CCM) Dk. John Magufuli amemuomba radhi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema, kufuatia uharibifu wa mali za jeshi hilo uliofanywa na wananchi wa Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Dk. Magufuli aliomba radhi kwa niaba ya wananchi wake kufuatia, kujeruhi, kuchoma moto na kuharibu mali za jeshi hilo uliofanywa na baadhi ya wananchi wilayani humo Julai 10, 2007.
Aliomba radhi wakati alipopewa fursa ya kuzungumza kwenye uzinduzi wa kituo kipya cha polisi uliofanywa na IGP Mwema, baada kile kiichokuwepo kuteketezwa kwa madai ya kumsaka mwanamke aliyetuhumiwa kukutwa na ngozi ya binadamu.
Waziri Magufuli alisema ana kila sababu ya kuwaombea radhi wananchi wake kwa Jeshi la Polisi kwa kitendo cha kuwajeruhi askari watano ambapo mmoja alivunjwa taya, mwingine kutobolewa jicho na kuchoma moto kituo cha polisi.
“Hata hivyo namshukuru IGP Mwema kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa kituo kipya cha polisi na nyumba za askari wetu katika Wilaya ya Chato… Jamani lakini wananchi wasingeyafanya yale hiki kituo cha kisasa tungekipata wapi?... Sifurahii waliyoyatenda ila nafurahia ujenzi wa kituo kipya kukamilika na leo kinazinduliwa.” Alisema Magufuli.
Aidha aliwataka wananchi kulithamini Jeshi la Polisi na kushirikiana kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa kutoa taarifa za uhalifu unapojitokeza.
Katika uzinduzi huo wa kituo kipya cha polisi na nyumba za askari Waziri Magufuli aliikabidhi hospitali ya Wilaya ya Chato shuka 200 za wagonjwa .
Alisema hafurahishwi na kuwalaza wagonjwa kwenye mashuka machafu na kutishia kuwa atafanya ziara za ghafla kuangalia usafi wa hospitali hiyo akisisitiza kuwa usafi ni muhimu ili kuzuia magonjwa ya milipuko.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment