NA MWANDISHI WETU
2nd December 2012
Kutokana na usiri huo, nchi huingia kwenye hasara hasa katika mikataba ya uchimbaji wa madini.
Afisa Mwandamizi wa Kanda, Revenue Watch Institute, Silas Olan’g, amesema kuwa usiri huo unatokana na waliosaini mikataba hiyo kuogopa fedheha ya kuulizwa na wananchi kutokana na maajabu yaliyomo kwenye mikataba hiyo.
Alisema hata wabunge ambao ni watunga sheria wakati mwingine wanapoiomba hunyimwa.
“Kama wataiona wataambiwa waisome hapo hapo na kuiacha, haruhusiwi hata kupiga picha ,” alisema.
Alisema hayo katika mkutano wa Wahariri wa Habari, ulioandaliwa na Kituo cha Haki za Binadamu na Msaada wa Sheria (LHRC) uliohusu uchimbaji wa madini ya Urani na madini mengine nchini na athari zake kimazingira.
Alisema baadhi ya nchi zilizofanikiwa katika mikataba ya madini ni Ghana, Botswana na Niger, kwa sababu mikataba yao huiweka kwenye tovuti zao na kuwapa wananchi fursa ya kuisoma.
Utafiti wa Revenue Watch Institute umebaini kuwa mikataba 150 ambayo imesainiwa na nchi mbalimbali barani Afrika imefanikiwa kutokana na nchi hizo kuweka mikataba yao wazi.
“Kwa Tanzania mikataba ni kitu cha siri, haiwekwi wazi kwa sababu walioisaini wanaogopa embarrassment (fedheha) kwa sababu ni ya ajabu,” alisema.
Olan’g alisema kinachowafanya kutoiweka wazi ni kugopa kuulizwa na Watanzania kutokana na maajabu yaliyopo kwenye mikataba hiyo.
Hata hivyo, alisema pamoja na mikataba hiyo kuwa siri hakuna kelele za kutosha kutoka kwa wananchi ya kutaka kuonyeshwa mikataba hiyo.
“Ni vizuri mikataba ikawekwa wazi ili kuona kama ina manufaa kwa umma, ili kuepuka migogoro inayojitokeza,” alisema.
Akizungumzia kuhusu uchimbaji wa madini ya Urani ambayo yamegundulika katika eneo la Namtumbo, mkoani Ruvuma, Olan’g alisema kuwa utafiti wa Taasisi yake umebaini kuwa Tanzania haina mfumo wa kisheria madhubuti wa kuruhusu uchimbaji wa madini hayo.
Alisema sheria inayotumika ni Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambayo ndio inayowaongoza kuhusu uchimbaji wa madini hayo.
Kwa mujibu wa sheria hiyo kifungu cha 25, kinasema madini ni mali ya umma lakini sheria mama ambayo ni Katiba haisemi na kusababisha mkanganyiko.
Alitoa mfano wa nchi ya Botswana ambayo sheria inasema kuharibu rasimali yoyote ya nchi ni kosa (rasilimali ya nchi kama thamani ya taifa) na sheria hiyo inalindwa.
Alisema kutokana na kuwa na sheria madhubuti taifa limeweza kuweka akiba ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 37 kutokana kuthamini rasilimali zao.
Kwa upande wake, Mwandishi mwandamizi, Ndimara Tegambwage, alisema kabla ya kuruhusu uchimbaji wa madini hayo kuna umuhimu wa kutafiti ili serikali iweze kujua madhara yake.
Madini hayo pia yanachimbwa pia katika nchi za Namibia, Afrika Kusini, Niger, Malawi na Amerika ya Kusini.
Hata hivyo, alisema imefahamika kuwa madini hayo ya Urani yana hatari kubwa kwa binadamu katika uchimbaji kutokana na madini hayo kuwa na mionzi yenye madhara.
Alisema ni lazima watu wajifunze kutoka kwenye uchimbaji wa madini mengine kama dhahabu, almasi, Tanzanite na chokaa ambapo umesababisha madhara kwa wananchi kwa kupata magonjwa ya ngozi, saratani, uchafuzi wa maji na vifo vya mifugo.
“Ni lazima uchunguzi ufanyike hatari iko wapi…Ni muhimu kutafiti ili serikali ijue madhara yake,” alisema.
Aidha, alisema inasemekana uchimbaji wa madini hayo unahitaji umeme mwingi na maji mengi na kuhoji kwa nchi kama Tanzania ambayo imeshindwa kutosheleza mahitaji ya wananchi wake kutokana na nishati hizo, mradi huo utajitoshelezaje.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment