Mtwara Gas Exploration Project
SALAM KWA RAIS WANGU MPENDWA…..MTWARA KUNA TATIZO.
Na Baltazar B.komba.
Nianze kwa nukuu za jumbe kutoka kwa ndugu zangu na rafiki zangu wa
Mtwara jumbe hizi zimezagaa katika simu za mkononi huko Mtwara jumbe
hizi zinaashiria kuna jambo linahitaji kushughulikiwa kwa mstakabali
mwema wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla
Mali za kusini zilichukuliwa wakati kuna makambi ya wapigania uhuru na
mali hizi zilitumika kuletea sifa taifa na mikoa mingine, Leo gesi
yetu inahamishwa kwenda huko huko tunaambiwa ni mali ya taifa, je
kusini ni taifa gani?Tusikubali kuondolewa gesi yetu ndio urithi wa
vizazi vyetu kama wewe ni mzalendo tuma sms hii kwa watu ishirini kama
na wewe unakubali kuwa fisadi kujidhulumu urithi wa watoto wako, basi
nyamazia kusini bila kanda zingine inawezekana amka jitambue okoa
vizazi vyako.(0652 137989)
Mikoa ya kusini ndio ilikuwa mikoa ya kimkakati katika mapigano ya
vita kusini mwa afrika,Mazao yetu kama mihogo,Mpunga,ufuta na mahindi
yalichukuliwa kwa ajili ya kuwachangia ndugu zetu walio kuwa
wanapigana vita , na mikoa hii ilikuwa kama yenye vita kwa kipindi
kirefu hali hii ilitufanye tukose fursa za maendeleo mpaka sasa,
Lakini pia tukumbuke kuwa reli iling’olewa bila sababu kuwekwa wazi na
sasa gesi inaondolewa bila sababu kuwekwa wazi ndgu wana Mtwara
tusikubali tukatae tuma ujumbe huu kwa watu wengi uwezavyo(0715616006)
Rais wangu hizi ni jumbe zilizo ingia katika simu yangu siku ya Tarehe
24/11/2012 na 25/11/2012 zikiwa zimetumwa na wananchi wakazi wa Mtwara
na siku ya tarehe 14/11/2012 nilihudhuria mkutano ulioandaliwa na TPDC
katika ukumbi wa Makonde pale Mtwara mjini mkutano huu ulikuwa na
lengo la kuchuka maoni ya wananchi juu ya utengenezaji wa rasimu ya
sera ya gesi. KIlicho tokea katika mkutano huu unaweza kumuuliza
mkurugenzi wa TPDC na najuwa hawezi kusema uongo tena kwa kuwa
aliambiwa kuwa atakuja kukudanganya kuwa wananchi wa Mtwara
wamefurahia sera hiyo ingawa haikuwa hivyo kilicho tokea ni wananchi
kumwambia mkurugenzi wa TPDC hawaihitaji maswala ya sera wakati tayali
gesi imekwisha ondoka na mikataba imekwisha ingiwa dhidi ya zao hilo
na wananchi hawakutoa mawazo yao kama ilivyo kusudiwa walikataa kutoa
maoni wakidai kuwa hawaja shirikishwa katika hatua zozote za
uchakatuaji mradi huo muhimu kwa mustakabali wa maisha yao.
Katika salam hizi sitaki kurudia kilicho wakuta mawaziri walio
ambatana na msafara wa sekretarieti mpya ya chama chetu haya najua
umeshaambiwa na katibu mpya wa chama cha CCM Mzee kinana, lakini si
mbaya nikakudokeza kuwa Yule mama aliye jitambulisha kwa jina la Rukia
Ismail Athumani ni mama mmachinga muuza samaki katika beseni usafiri
wake miguu trela yake kichwa maisha yanaenda, nafikiri umeambiwa namna
alivyo mshambulia dada yetu,mbunge wetu waziri wetu Hawa ghasia juu ya
suala hili hili la uchakatuaji mradi wa gesi na usafirishaji wa gesi
kwenda Dar salaam, Si rahisi kwa utamaduni wa wanawake wa mikoa ya
pwani wewe unajua hilo, kuwa na ujasiri mkubwa wa kuongea mbele za
watu katika hadhira kama ile tena kuongea kwa kukemea kwa jazba na
kumkemea mwanamke mwenzie zile ni dalili kuwa kuna tatizo linalo
hitaji kushughulikiwa mapema na wewe mwenyewe ,sitaki kuongea kuhusu
zile zomea zomea za wahuni…..!
Muh,Rais salam hizi sijui kama zitakufikia kwa wakati, ila kuzileta
niliapa tokea siku ile nilipo hudhuria mkutano wa kutoa maoni kuhusu
sera najua kipindi hiki muheshimiwa utakuwa unapumzika kutokana na
majukumu mazito uliyo yafanya ya kupanga safu katika chama chetu
chadema…lakini naomba unisamehe nimeoana nizitume mapema ili ratiba
yako ya majukumu itakapoanza kwa siizoni hii basi ikiwezekana uje
uongee na wananchi (si wazee wa chama chetu peke yao) wa Mtwara.
Muheshimiwa Rais wangu naomba unisikiliza kuhusu masuala mawili
makubwa yanayo zizima hapa Mtwara swala la kwanza ni suala la gesi,
wananchi hawajui chochote kuhusu gesi na unajua kama ulivyo sema siku
ile ukihutubia pale Dar salaam wakati timu yetu ya ushindi ikiwa
inapongezwa nakumbuka ulisema hivi nanukuu wao wakisema tusipo jibu
hata kama ni uongo utakuwa ni ukweli.
Mheshimiwa Rais Mtwara wananchi wana hamu ya kujua kwanini gesi
imepelekwa Dar salaam kwa bahati mbaya hakuna hata kijana wako mmoja
aliye mudu kuwaeleza wananchi kwa ufasaha juu ya suala hili na dalili
zinaonyesha kuwa hawajui, kwa bahati mbaya zaidi hata hawa wabunge
wetu maarufu kwa jina la Kaka(mjini) na Dada(vijijini) nao wapo kimya
tena hawana muda kabisa wakuongea na wapiga kura wao juu ya suala hili
na wananchi wameshindwa kuwashinikiza chochote wanadai kuwa kaka
alifanya mambo yetu yale wakati wa kumchagua naogopa kusema moja kwa
moja kwa kuwa sina evidensi ila huyu kaka anaonekana hajui chochote
juu ya wajibu wake kwa wananchi walio mchagua na wala hili ninalo
kuambia kuwa ni fukuto sijui kama hata anajua ila ukweli ni kuwa
Mtwara si shwari kuna tatizo
Muheshimiwa Rais jambo la pili ni Ardhi muheshimiwa Rais Mtwara ya leo
sisi watoto wa Kudihalika, Nammohe, Minjale, Lupanda, Namdimba na
wengine hatuna tena uwezo wa kununua ardhi hata kipande cha robo ekari
kwa matumizi yeyote ardhi katika mji huu imeshakuwa ni bidhaa adimu,
Manispaa wako kimya kupima ardhi na wakipima tayari imekwisha ombwa na
kunamaombi mengi ya muda mrefu sijui sasa kizazi hiki kitapata wapi
ardhi, na tunachoshuhudia hapa ni wanasiasa kuotesha majumba na
kuporomosha vitega uchumi na kuendelea kujilimbikizia viwanja si hivyo
tu muheshimiwa hata viongozi wa serikali yako nao wanajipatia maeneo
huku kwa kasi ya ajabu na kwa habari tulizo zichomoa zikiwa mbichi ni
pamoja na malalamiko ya madiwani eti kila wanapo kaa katika vikao vyao
wanapo taka kupima viwanja wanakutana na maombi kwa ajili ya matumizi
maalum maombi ambayo hayatakiwa kuhojiwa wala kuulizwa kwa kuwa ni
maalum mimi mwandishi wa salam hizi nakumbuka niliandika maombi kwa
njia ya barua kuomba kiwanja mwaka 2008.mpaka naandika waraka huu
kwako hata jibu sijapatiwa…!
Jambo jingine ambalo kelele zake inawezekana umezizowea ni kuhusu zao
la korosho kuna minong’ono huku mitaani kwetu kuwa wanao angusha bei
ya zao letu hili la korosho ni hawa viongozi wetu tulio waamini kuwapa
nafasi za kutuwakilisha huku katika jumba la maamuzi na kutungasheria
na kisa kikubwa kinazungumzwa huku ni kuwa hao nao ni miongoni mwa
wenye makampuni haya ya kifisadi yanayo jifanya yananunua Korosho kwa
mfumo usiotakiwa na wananchi mfumo wa stakabadhi gharani,
Muheshimiwa kama kuna vita inakuja Mtwara ni vita ya Ardhi kwa kuwa
wananchi wa kawaida wamepoteza matumaini kabisa ya umiliki Ardhi na
hakuna kiongozi wetu tuliye mchagua anaye onyesha utashi wa kisiasa wa
kuja na mbinu au mkakati wowote wa kumilikisha wananchi Ardhi.
Muheshimiwa Rais kupitia salamu hii tunaomba utusaidie haya yafuatayo
kwanza uje utuambie tusiuze tena kura mwaka 2015, Na utuambie umuhimu
wa hicho kitu kinacho itwa ARDHI katika maeneo yanayo patikana
Rasilimali kama gesi au mafuta hivyo tusiraghaiwe kwa kuwauzia
mafisadi wenye tamaa ya kuinunua nchi yote hii, na uje uwaambie
mafisadi na viongozi wa kisiasa na serikali wanao jilimbikizi a ardhi
kuwa hawataweza kuikalia kwa starehe kama hawa maskini wengi
wataendelea kuitwa wavamizi katika ardhi ya mababu zao, lakini kubwa
zaidi uje na mkakati maalumu wa kuwafanya vijana wa Mtwara walio
poteza matumaini ya kuwa wana Mtwara kwa kuwa hawana uhakika
wakuendelea kuwa Mtwara kwa kukosa ardhi uwasadie wapate ardhi,
muheshimiwa Rais yanayotokea katika nchi za wenzetu yaweza tokea kwetu
na dalili zimeanza kuonekana maana viongozi wakisiasa na serikali
wanajilimbikizia maeneo kwa kuendelea kuwalaghai wazee maskini
wawauzie bila kujali kuwa maeneo ya Ardhi hayapanuki na watu
wanaongezeka hali hii inasababishwa na uwepo wa uwekezaji wa gesi na
mafuta.
Lakini umaskini, kukosa elimu kutokana na mlimbikizo wa mkoa huu
kukosa fursa ni sababu za msingi za wakazi wake kutokuelewa umuhimu wa
masuala ya umiliki wa ardhi, sawa na sheria ya ardhi na 5 ya mwaka
1999.
Tukumbuke kuwa wajukuu zetu watahoji asili zao na wataambiwa kuwa wao
ni wana Mtwara achilia mbali wamakonde,wayao,wamakuwa,wango ni,wamwela
na wataonyeshwa makaburi ya baba,bibi,babu zao wakiwa wamezikwa katika
Ardhi ya Mtwara lakini wakati huo watakuwa hawana hata kipande cha
Ardhi na watakuwa wanaiona ardhi inayo milikiwa na Mushi, Shirima,
Mrema, Mfinanga, Mkama, Bundala katika hali kama hiyo maswali yatakuwa
mengi kuliko majibu na mwisho wake watakuwa hawana cha kupoteza na
hatua ya kukosa cha kupoteza ikifika maamuzi yeyote yanaweza kufuatwa
tusishangae kuona ya Biafra yakitokea pia hapa kwetu mungu apishe
mbali
Mimi ninaye kuandikia salaam hizi ni miongoni mwa wamachinga wenye
jina kutokana na shughuli zangu na sina tumaini la kumiliki ardhi leo
wala kesho kwa muujiza wowote zaidi yakuendelea kuitwa mvamizi tu
katika ardhi ya mababu zangu hii ni hatari sana,Naelewa muheshimiwa
Rais maandishi haya yanaweza kunibadilisha jina sijui nitaitwaje,
mwongo, mgombanishi,mpinzani au hata mchochezi au hata
vyovyote ,lakini nimeyaandika nikijua kuwa maandishi hayafutiki na
hasa maandishi kama haya yaliyo beba sauti ya kutafuta haki za watu
wengi wasio na sauti.
Muheshimiwa rais mungu amekujalia wewe binafsi kuwa na huruma hebu
tuhurumie sisi vijana wa Mtwara, hebu tumia hiyo huruma yako kuiokoa
Tanzania, hebu tumia huruma yako kuondosha balaa, na katika hili
usimuamini mtu njoo uongee na sisi wamachinga, uongee na sisi bodaboda
na wengine wengi
Muheshimiwa Rais nisikuchoshe na ujumbe huu usio na maana sana kwako
lakini kabla sija hitimisha ni vema nikakujulisha majibu nilyo wapa
wale wana Mtwara wenzangu walio nitumia ujumbe pale juu niliwajibu
hivi.
No.. No..Situmi ujumbe huu kwa mtu yeyote kwa kuwa huu ni ujinga wetu
wa kuuza kura kama chapati na sasa tunakumbuka shuka asubuhi, hivi
kweli gesi hii ingekuwa katika jimbo la Mchungaji Msigwa, Mnyika, au
January makamba, mwiguru nchemba, zitto kabwe ingesafirishwa bila
wananchi kujua au bila kuzingatiwa maslahi ya jimbo husika au mkoa
husika No situmi NO,huu ni uzembe wetu Sambaza ujumbe huu kadri
uwezavyo.
Haya ndiyo majibu yangu kwa jumbe nilizotumiwa na rafiki zangu hao
hapo juu kutoka Mtwara.
Ahsante muheshimiwa rais wewe pekee ndio tumaini letu okoa Mtwara okoa
Tanzania.
(Mtumwa wa watu)
+255 786-821744,767 821744,779 8217144.
(HAPA KUNA BANGO LENYE BENDERA MBALIMBALI LIKIWA MBELE YA OFISI YA
JIMBO MTWARA MJINI)
Bango lenye maneno ya…. Gesi kwanza vyama baadaye hakitoki kitu
hapa….. likiwa limewekwa nje ya ofisi ya Jimbo ya chama cha NCCR-
Mageuzi siku ya Tarehe 12/12/2012 siku ambayo vyama vyote vya siasa
isipokuwa CCM vimeungana na kufanya mkutano wa Pamoja wenye ajenda ya
kupinga kusafirishwa kwa gesi kutoka mnazi bay Mtwara kwenda Dar-es-
salaam
huuu ujumbe(kama ulivyo) nimetumiwa kwenye email nifikishe kwa zitto
kabwe.
Chanzo: Wanabidii
No comments :
Post a Comment