Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, December 25, 2020

ASSASSINATION OF IRINGA RC DR. WILBERT KLERUU BY "MNYALUKOLO" SAID MWAMWINDI IN IRINGA ON 25.12.1971!

SAID MWAMWINDI


Na MZEE WA  ATIKALI ✍️✍️✍️

1. Usuli

Ijumaa mujarab ya leo tarehe 25.12.2020, siku ya Krisimas, ni miaka 49 toka "Mnyalukolo" SAID ABDALLAH SIULANGA MWAMWINDI (42) ammiminie risasi na kumuua Mh. Dk. WILBERT ANDREW KLERUU, aliyekuwa RC wa Iringa, siku ya Krismas, Jumamosi, tarehe 25.12.1971 katika kijiji cha Mkungugu, Isimani, maili takriban 25 toka Iringa mjini.

"ATIKALI" hii inatiririsha kinagaubaga kilichopelekea "Mnyalu" huyu machachali kusema "Swela" na kisha kumuua RC huyo, ikianzia na historia fupi ya marehemu  RC Dk. KLERUU aliyekuwa Mjamaa wa aina yake.


2. Dk. KLERUU: Msomi Mbobevu


Marehemu Dk. WILBERT ANDREW KLERUU alikuwa ni mzaliwa wa Mwika, mkoani Kilimanjaro. Alikuwa na akili sana darasani na alipofanya mtihani wa shule ya msingi na shule ya kati alifaulu vizuri sana.

Dr. KLERUU alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya "Old Moshi" alikosoma na watu wengine waliokuja kuwa mashuhuri mf EDWIN MTEI, HERMAN SERWATT & DANIEL MFINANGA. Baadaye, baada ya kufaulu tena mitihani yake kwa kiwango cha juu, Dk. KLERUU alichaguliwa kujiunga na "Tabora school" alikosoma na MTEI, JOB LUSINDE, OSCAR KAMBONA, MARK BOMANI  GEOFREY MMARI nk. Dk. KLERUU alipomaliza masomo ya sekondari akaenda Marekani. Huko alisomea shahada ya uzamivu (PHD) ya Chuo Kikuu cha California, Los Angeles, US. Hivyo, Dk. KLERUU alikuwa mmoja wa ma- "Regional Commissioners" "RCs" wachache sana TZ waliokuwa elimu ya juu kiasi hicho katika miaka ya 60 & 70.


3. Dk. KLERUU Awa Msaidizi wa Mh. KAMBONA


Dr. KLERUU, aliporejea nchini, aliteuliwa kuwa msaidizi wa Katibu Mkuu wa TANU, Mh. OSCAR KAMBONA, kazi aliyoifanya kwa takriban muongo mmoja.


4. Rais NYERERE Amteua Dk. KLERUU Kuwa RC


Baada ya kufanya kazi nzuri ndani ya TANU, Rais JK NYERERE alimteua Dk. KLERUU kuwa RC wa Ntwara. Hii ilitokana na imani kubwa ya Rais NYERERE kwa Dk. KLERUU. 


5. Dk. KLERUU RC Machachari


Dk. KLERUU alikuwa ni RC machachari aliyekuwa akiwapeleka "mpetumpetu" wakazi wa Ntwara na  kuonekana "mnoko" sana. Dr. KLERUU alifanya kazi kubwa kuhakikisha ulinzi uko vizuri mkoani humo kwani enzi hizo kulikuwa na mapambano makali ya kusaka uhuru wa Msumbiji. Aidha, Dr. KLERUU hakusita kufokea wafanyakazi, hata Wakurugenzi hadharani, mara tu alipobaini wamembwelambwela, kama Bw. PHILIP RAIKES alivyodadavua katika kitabu chake "Agrarian Crisis & Economic liberalisation in TZ, 1979-:"


"Dk. Kleruu had achieved a certain local popularity largely because of his habit of abusing civil servants in public. His expropriation of the rich peasants also seems to have been quite popular".


6. RC Dk. KLERUU Avunja Rekodi


Mwaka 1970 akiwa RC wa Ntwara, Dk. KLERUU aliweka rekodi ya kuanzisha vijiji vingi vya ujamaa TZ. Kati ya vijiji 2000 vilivyoanzishwa TZ, yeye peke yake alianzisha vijiji 750.


7. Rais NYERERE Amhamishia Iringa RC Dk. KLERUU


Rais NYERERE alimpongeza sana Dk. KLERUU kwa mafanikio hayo makubwa ya uanzishwaji vijiji vya ujamaa na katikati ya mwaka 1971, akamuhamishia mkoani Iringa, moja ya mikoa iliyounda "The Big 4"  TZ, ili akasambaze mafanikio hayo ya Ntwara. RC Dk. KLERUU, alipohamia Iringa, alichukua nafasi ya RC JOHN MWAKANGALE.


8. Ntwara Wafurahia RC Dk. KLERUU Kuhamishwa!


Katika hali ya kustaajabisha, baadhi ya wakazi wa Ntwara walifurahia mara tu baada ya RTD kutangaza uhamisho wa RC huyo wa shoka!. 


Bw. DAVID BUTININI aliyekuwa askari polisi na kada wa TANU enzi hizo akiwa Ntwara kabla ya kuhamishiwa Iringa na ambaye pia alikuja kuwa shahidi kesi ya MWAMWINDI, anaelezea jambo hili-:


"Kule Mtwara, Dk. Kleruu alionekana mtemi sana. Lakini tuelewe kuwa wakati ule tulikuwa tunawasaidia ndugu zetu wa Frelimo hivyo kulihitaji mtu mbabe kama Dk. Kleruu".


9. RC Dk. KLERUU Atinga Iringa


RC Dk. KLERUU hakuwa mtu wa mchezo-mchezo. Alipotinga tu Iringa aliwachimba mkwara mzito "Wanyalukolo" kuwa uzembe na tabia yao ya kushinda wakifakamia ulanzi ni marufuku!. 


Aidha, RC Dk. KLERUU hakuwa mtu wa kukaa ofisini bali aliwafuata wananchi na kushiriki nao bega kwa bega katika shughuli za ujenzi wa Taifa. Kushika jembe na kulima au panga na kukata miti kwake ilikuwa ni kama uji na mgonjwa! Mzee maarufu Iringa mjini, Bw. OMAR MSELEM NZOWA, rafiki wa zamani wa MWAMWINDI, anaeleza kuwa Dk. KLERUU alikuwa machachari sana na alipoingia tu Iringa akawachimbia mikwara mizito "Wanyalukolo" na mmoja wa mikwara hiyo ni huu-:


"Hamnijui mimi, kawaulizeni watu wa Mtwara ndio watawapeni habari zangu. Mimi sina mchezo hata kidogo".


10. RC Dr. KLERUU Aanzisha Kampeni Kabambe ya Kilimo


Moja kati ya shughuli za mwanzo za RC Dk. KLERUU alipofika Iringa ilikuwa ni kuanzisha Kampeni kabambe ya kutaifisha mashamba makubwa ili yawe ya vijijiji vya ujamaa kufikia mwishoni mwa Novemba 1971.


Huyu ndiye RC DR. KLERUU. 


Baada ya kumjua RC Dk. KLERUU, ni vyema sasa kumjua Bw. MWAMWINDI. 


11. "Mnyalu" MWAMWINDI ni Nani?"


Bw. MWAMWINDI alizaliwa Iringa mjini mwaka 1929, enzi za ukoloni. Baba yake alikuwa "Jumbe" eneo la Mshindo, Iringa mjini. Baadae, Bw. MWAMWINDI akaja kuwa dreva. Mwaka 1954, Bw. MWAMWINDI na familia yake walihamia Mkungugu, Isimani. Bw. MWAMWINDI alivamia mapori makubwa na kupambana na wanyama na wadudu wakali mf nyoka hatimaye aliweza kulima kidogokidogo, hadi kuwa na hekali nyingi. Kilimo kilimnufaisha sana hadi akawa tajiri mwenye mashamba makubwa, matrekta na majumba  kadhaa Iringa mjini.


Huyu kwa kifupi ndiye Bw. MWAMWINDI. 


Je, nini kilijiri Iringa kati ya mafahari hawa wawili mwaka 1971?.


12. RC Dk. KLERUU Aitisha Mkutano na Wakulima Wakubwa


Tarehe 23.12.1971, RC Dk. KLERUU aliitisha mkutano na Wakulima wakubwa wa Isimani kuwaelezea azma ya serikali kutaifisha mashamba yao. Enzi hizo, Isimani ndiyo ilikuwa ikiongoza TZ nzima kwa ukulima wa mahindi. Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa "Welfare" mjini Iringa. Wakulima hao wa "Kinyalukolo" , Bw. MWAMWINDI akiwa mmoja wao, walicharuka vibaya sana. Hoja yao ilikuwa kwamba si sahihi kuwapoka wao mashamba wakati mapori bado yako mengi. Hivyo, mkutano huo ulivunjika bila kupata muafaka wowote.


13. RC Dk. KLERUU Atinga Kwa Bw. MWAMWINDI Siku ya Xmass


Jioni ya siku ya Jumamosi ya tarehe 25 Desemba 1971, RC Dk. KLERUU alichukua gari la RC Peugeot 404 rangi ya bluu ubavuni ikiwa imeandikwa "RC Iringa", akavaa kofia ya pama na kwenda Isimani. Katika hali ya kustaajabisha, RC huyo alienda bila mlinzi wala ulinzi wowote!. Alienda kwanza kwa mkulima mkubwa aliyeitwaye RASHID JUMA huko Nyang'olo lakini akamkosa.


Saa 10 jioni, RC Dk. KLERUU akafika shambani kwa Bw. MWAMWINDI na akamkuta akilima. Bw. MWAMWINDI alikuwa juu ya trekta lake pamoja na mwanae (MOHAMED) na watu 2 aliokuwa amewaajiri (YADI CHAULA & CHARLES MWAMALATA) na mkwewe JOSEPH KISAVA.


14. RC Dk. KLERUU Atunishiana Msuli na Bw. MWAMWINDI!


RC Dk. KLERUU, aliyekuwa jeuri kwelikweli, alianza kumvurumushia Bw. MWAMWINDI maswali chechefu yaliyomkera sana Bw. MWAMWINDI; RC Dk. KLERUU-: "Ebu shuka, kwanini unalima hapa?" . Bw. MWAMWINDI-: "Ni shamba langu". RC Dr. KLERUU -: "Mwongo, shenzi wewe". Bw. MWAMWINDI-: "Mbona unanitukana?" RC Dk. KLERUU- : "Funga domo lako, ng'e ng'e ng'e, hii hii nini? Bloody  fool!". 


RC Dk. KLERUU alikuwa akiuliza maswali hayo huku akimtomasatomasa Bw. MWAMWINDI tumboni kwa kifimbo chake alichopenda kutembea nacho!.


Bw. MWAMWINDI akasema "Swela" na akaamua kwenda kwenye nyumba yake iliyokuwa jirani huku akifuatwa kwa nyuma na RC Dk. KLERUU. Walipopitia makaburini kabla ya kuifikia nyumba hiyo, RC Dk. KLERUU akamwambia- "Tazama unaendelea kujenga nyumba za kudumu". Bw. MWAMWINDI akajibu- "Hizi sio nyumba, ni makaburi ninapozikia ndugu zangu". RC Dk. KLERUU-: "Ni mahali unapozikia mirija wenzio, mbwa wee!".


 "Mnyalu" MWAMWINDI akazidi kufura hasira!.


15. MWAMWINDI Ammiminia "Shaba" RC Dk. KLERUU!!!


Kufumba na kufumbua, Bw. MWAMWINDI aliingia ndani na kuchukua bunduki kisha, bila kutoa onyo lolote, akammiminia risasi RC Dk. KLERUU ambaye alianguka na kufariki hapohapo bila hata kuomba maji!.


16. Bw. MWAMWINDI Aripoti Polisi


Bw. MWAMWINDI alichukua pama ya RC Dk. KLERUU, akatoa ufunguo wa gari mfukoni mwa suruali kisha akauingiza mwili wa marehemu kwenye  Peugeot 404 kwa kisaidiana na mwanae, MOHAMMED. Baada ya hapo akawasha gari lilikokuwa na bendera ya Taifa akaenda Iringa mjini.


17. Bw. MWAMWINDI Aukabidhi Mwili Polisi, Aswekwa Lupango!


Alipofika Iringa mjini, Bw. MWAMWINDI aliwashangaza watu kwani alikuwa akiendesha gari upande wa kulia hali iliyofanya watu wahisi RC ana dharura kwani mtaa wa Jamatini ni "One way" na gari zinashuka Kusini, hazipandi Kaskazini. Bw. MWAMWINDI alipofika Kituo Kikuu cha Polisi, alienda "counter" na kumkuta PC MBETA KASONDA akamkabidhi funguo na bunduki kisha  akamueleza-:


"Nendeni kachukueni mbwa yenu kwenye gari, tayari nimeishaiua".


18. PC KASONDA  Ashangaa Kubaini ni RC Dk. KLERUU!


PC KASONDA alipigwa butwaa kubwa na hakuamini macho yake alipobaini kuwa mwili uliokuwa kwenye gari ni wa RC Dr. KLERUU! RC Dk. KLERUU alikuwa amevaa ovaroli jeusi huku mwili ukiwa umetapakaa damu. Mara moja PC KASONDA akamuweka Bw. MWAMWINDI chini ya ulinzi. Tarumbeta likapigwa na askari wakakusanyika na kujuzwa kifo hicho kisha gari likahifadhiwa nyuma ya kituo hicho cha polisi. Askari wanne walienda kuleta kitanda cha magurudumu toka hospitali ya mkoa na mwili ukaenda kuhifadhiwa "mortuary" ya hospitali ya mkoa.


19. RTD Yatangaza Kifo


"Bongolanderz" waliokuwa wakisheherekea Krismasi maeneo mbalimbali nchini, walipigwa butwaa baada ya RTD kuutangazia umma kuhusu kifo cha RC Dk. KLERUU katika taarifa yake ya habari saa 2 usiku. Majonzi yalitamalaki nchi nzima hasa kutokana na jinsi kifo hicho kilivyotokea.


20. Baadhi ya "WANYALU" Washangilia Kifo!


Baadhi ya  "Bongolanderz"  mkoani Iringa walikuwa wakimchukia sana RC Dk. KLERUU. Hivyo, usiku huo, watu hao walinunua makreti ya bia kwenye baa mbalimbali na wengine wakiwa eneo la Mlandege walinunua ulanzi na kuanza kunywa kwa kushangilia waziwazi kifo hicho kwa maneno "chechefu" huku wakimwaga ofa za bure kwa wapita njia!.


21.  "WANYALU" Wachanga $ 2500 Kumtafuta "Advocate" wa Nje


Baada ya Bw. MWAMWINDI kuswekwa Lupango, baadhi ya wakulima wenzake matajiri wa "Kinyalu" walijiorodhesha ili kuchanga $ 2500 kwaajili ya kumpata wakili toka nje ya nchi ili amtetee Bw. MWAMWINDI.


22. Kamatakamata Yarindima Iringa


Kufuatia kadhia hiyo ya kushangilia kifo cha RC Dr. KLERUU,  kufumbua na kufumbua, kamatakamata "ya kufa mtu" ilirindima usiku huo huo mjini Iringa na kuwakumba watu takriban 50 wakiwemo watu maarufu enzi hizo mf SAID MOHAMMED, IBRAHIM KHALIL, PESAMBILI na MURSAL. Aidha, kamatakama hiyo ya aina yake iliwakumba hata waliojiorodhesha kumtafutia Bw. MWAMWINDI wakili wa nje! Waliokamatwa walipelekwa maeneo tofauti nchini mf. Mwanza, Shinyanga na ZNZ huku ndugu zao wakiwa  hawajui walikopelekwa!. Bw. MWAMWINDI alipelekwa gerezani la Isanga, Idodomia huku nyumba zake Isimani na Iringa mjini zikilindwa 24/7!.


23. Mtoto Wake Amtembelea Gerezani


Kamatakamata iliyotamalaki Iringa ilipelekea kutokea kwa uhasama mkubwa sana kati ya ndugu wa Bw. MWAMWINDI na ndugu wa watu waliokamatwa kwani walidai tatizo hilo limesababishwa na Bw. MWAMWINDI! Hivyo, mwanae (AMANI, akiwa na miaka (21) tu, akaomba Kibali cha DC na akaweza kwenda kumuona baba yake gerezani na kumuhabarisha yanayojiri uraiani. Bw. MWAMWINDI alihuzunika sana.


24. Bw. MWAMWINDI Amwandikia Barua Rais NYERERE


Bw. MWAMWINDI akaamua mara moja kumwandikia barua Rais NYERERE na kumueleza kuwa yeye pekee ndiye aliyemuua RC Dk. KLERUU hivyo ni vyema wengine waachiwe kwani hawahusiki kwa namba yoyote na kifo hicho.


25. Rais NYERERE Awaachia Waliotiwa ndani


Rais NYERERE, siku chache tu baada ya kupokea ombi la Bw. MWAMWINDI, aliwaachia wananchi wote waliokamatwa kwenye "msala" huo. Hata hivyo, baada tu ya kuachiwa, baadhi yao waliamua kuhama kabisa eneo la Isimani na wengine walienda mikoa mingine kwani waliona imeishakuwa nuksi!.


26. Kesi ya Bw. MWAMWINDI Yaanza Kurindima Mahakama Kuu


Upelelezi wa kesi hii ulifanywa kwa haraka na spidi isiyo ya kawaida na Bw. MWAMWINDI akafikishwa Mahakama Kuu akikabiliwa na kesi ya "Murder"  chini ya Kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu, Sura ya 16. Wananchi lukuki walikuwa wakijitokeza kufuatilia kesi hiyo ya aina yake kila siku. Kesi hiyo ilikuwa mbele ya Mh. Jaji GABRIEL CHIKE ONYIUKE wa Nigeria (ambaye alikuwepo nchini toka 1970 hadi 1973).


27. Bw. MWAMWINDI Apelekwa Kortin kama Mfalme


Kutokana na unyeti wa kesi yake, Bw. MWAMWINDI alikuwa akipelekwa kortin na msafara mkubwa wa magari na ulinzi mkali huku wananchi lukuki wakijipanga barabarani kutaka kumuona "Mnyalu" huyo. Kwa hakika, Bw. MWAMWINDI alionekana kama mfalme na siku za kesi yake ni kama mji ulisimama!.


28. DPP SAMATTA Aendesha Kesi!


Kutokana na unyeti wa kesi hii, DPP BARNABA A. SAMATTA ndiye aliyekuwa akiiiendesha kesi hii yeye mwenyewe na si wasaidizi wake. DPP SAMATTA aliiendesha kesi hii kwa weledi mkubwa.


29. RPC Atoa Ushahidi Upande wa Bw. MWAMWINDI


RPC wa Iringa, ABUBAKAR HASSAN, alitoa ushahidi upande wa Bw. MWAMWINDI ambapo alieleza kuwa siku ya tukio hakutaarifiwa kuwa RC Dk. KLERUU alikuwa na safari ya Isimani ndio maana hakumpa "police escort".


30. Bw. MWAMWINDI Ajitetea Alikuwa "Provoked"


Utetezi wa Bw. MWAMWINDI ulikuwa wa aina mbili. Kwanza alidai kuwa yeye huwa mara nyingine ana "mawenge" na huwa anakuwa "waruwaru" (insane). Mama yake alitoa ushahidi kuthibitisha kuwa mwaka 1958 ndipo alipoanza kupata "mawenge" ambayo hujirudia. Pili, Bw. MWAMWINDI alidai kuwa alikuwa "provoked" (alikasirishwa) na "maneno ya shombo" ya RC Dr. KLERUU. 


31. DPP Adai Bw. MWAMWINDI Aliua Kwa Kukusudia


DPP alileta ushahidi na kudai kuwa Bw. MWAMWINDI aliua kwa kukusudia. Mmoja wa mashahidi wake alikuwa Dr. PENDAEL ambaye alieleza kuwa ingawa Bw. MWAMWINDI aliwahi kupata mawenge, lakini wakati akifanya mauaji hayo akili yake ilikuwa iko sawa kabisa.


32. Hukumu Yasubiriwa kwa Hamu!


Baada ya Jaji ONYIUKE kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili kwa makini sana, alipanga tarehe 2 Octoba 1972 kuwa siku ya hukumu. "Wanyalukolo", maofisini, vilabuni, mashuleni nk wakawa wakitabiri hukumu itakuwaje. Kila mmoja alibashiri jinsi alivyoona yeye!.


33. JAJI ONYIUKE "Amnyonga" Bw. MWAMWINDI!


Siku kuntu ya Jumatatu, tarehe 2 Octoba 1972, Mahakama Kuu ilifurika hadi pomoni. Mh. Jaji ONYIUKE alimtia hatiani Bw. MWAMWINDI kwa kosa la mauaji ya kukusudia na kuamuru anyongwe hadi afe. Mh.Jaji aliona kwamba kitendo cha Bw. MWAMWINDI kwenda hadi nyumbani kuchukua bunduki kiliakisi dhamira ovu, hivyo alifanya kitendo hicho kwa kukusudia ( "Saidi Mwamwindi Vs R (1972") No.212).


34. Kesi ya MWAMWINDI Yaweka Rekodi TZ


Nchini TZ, kesi za mauaji ni kesi zichukuazo miaka mingi hadi kutolewa hukumu. Kesi ya Bw. MWAMWINDI iliweka rekodi nchini kwani ilichukua takriban miezi 10 tu kwa upelelezi kukamilika, ushahidi kutolewa na hukumu kusomwa!  (Desemba 1971 - Octoba 1972)!.


Rais NYERERE alitia saini mara moja Hati ya kunyongwa kwa Bw. MWAMWINDI na hivyo huo ndio ukawa ndio mwisho wa maisha yake hapa duniani!.


35. Rais NYERERE Alihofia RCs Wangevunjika Mioyo


Moja ya sababu kubwa zilizozopelekea Rais NYERERE kuchukua uamuzi huo wa kutia saini hati hiyo haraka ni kuogopa RCs wangevunjika mioyo baada ya kuona mwenzao akiuawa kinyama.


36. Rais NYERERE Aliidhinisha Kunyongwa kwa Watu 10


"Bongolanderz" wengi wemekuwa wakijiuliza iwapo Baba wa Taifa  aliwahi kuidhinisha mtu yeyote kunyongwa  na kama aliwahi, je aliidhinisha watu wangapi kunyogwa akiwa madarakani toka tarehe 9.12.1962 hadi 5.11.1985?. Jibu la swali hili lilitolewa bungeni tarehe 30.1.2008 ambapo Mh. MATHIAS CHIKAWE, aliyekuwa Naibu Waziri wa Sheria na Katiba  alilijuza Bunge-:


"Mh. Spika, toka nchi yetu ipate uhuru, jumla ya watu 82 wamenyongwa kuanzia awamu ya kwanza. Kati ya watu hao, 10 walinyongwa wakati wa awamu ya kwanza na 72 wakati wa awamu ya pili. Hakuna mtu aliyenyongwa kwenye awamu ya tatu na ya nne".


Aidha, Mh. KHAMIS KAGASHEKI, alipokuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, alilifahamisha Bunge, tarehe 31.10.2008-:


"Mh. Naibu Spika, amri ya kutekeleza adhabu ya kifo kwa mara ya mwisho ilitolewa mwaka 1994".


37. Familia ya RC Dk. KLERUU Yarejea Kilimanjaro


Marehemu RC Dk. KLERUU aliacha mke na watoto 4 (EVA, ANDREW, CARMEN & EDWIN). Baada ya kifo hicho, familia ya marehemu Dk. KLERUU ilirejea nyumbani Kilimanjaro. 


38. Serikali Yawasomesha Watoto wa Dk. KLERUU Mamtoni


Rais NYERERE alihuzunishwa sana na mauaji ya RC Dk. KLERUU. Hivyo alisaidia wanawe kusoma Bulgaria na Urusi. Viongozi wengine nao walikuwa karibu sana na mjane na watoto hao mf KARUME, JUMBE, KAWAWA & MONGELLA. 


39. Rais NYERERE Ateua RC Mpya


Baada ya kuuawa kwa RC Dk. KLERUU, Rais NYERERE alimteua Mh. MOHAMED KISSOKY kuwa RC mpya wa Iringa. 


40. MBARAKA MWINSHEHE Amtungia Wimbo Dk. KLERUU


MBARAKA MWISHEHE, mwimbaji Bora kabisa kuwahi kutokea nchini, alimtungia Dk. KLERUU wimbo mujarab uliovuma sana enzi hizo "Dk. KLERUU: SHUJAA & MWANAMAPINDUZI".


41. Familia ya Dk. KLERUU na ya Bw. MWAMWINDI Zamaliza Tofauti Zao


Mwezi Machi 2014, Bi. EVA W. KLERUU (60), mtoto wa kwanza  wa Dk. KLERUU na Bw. AMANI MWAMWINDI (67), mtoto wa kwanza wa MWAMWINDI aliyekuwa Meya wa Iringa, walikutana kwaajili ya Maridhiano. Wawili hao walipiga picha kwa bashasha katika ofisi ya Bw. AMANI ie Mstahiki Meya wa Iringa mjini yalikofikiwa Maridhiano hayo.


Bi. EVA, huku akububujikwa machozi alinena-:


"Tukio la mauaji ya 1971 lilifanya familia iogope kuja Iringa. Hata hivyo, niliweka nadhiri ya kufika kuona mahali baba yangu alipouawa. Hatimaye leo nimefika na pia nimeonana na Amani, mtoto wa Mwamwindi na tumefanya Maridhiano".


Naye Meya AMANI, alitiririka-:


"Ninayo furaha kukutana na dada yangu Eva na kuondoa tofauti zetu. Ni jambo la kumshukuru Mungu".


42. Chuo cha Ualimu chapewa jina la Dk. KLERUU


Ili kukumbuka na kuenzi mchango mujarab wa marehemu RC Dk. KLERUU, chuo cha ualimu mkoani Iringa kilipewa jina lake "Dk. KLERUU Teachers Training College". Hii ilikuwa ni heshma kubwa kwake.


43. MNARA wa Dk.  KLERUU Wajengwa "Mji" wa Bw. MWAMWINDI


Mnara wa RC Dk. KLERUU ulijengwa kwenye "mji" wa Bw. MWAMWINDI sehemu ambayo RC huyo alimiminiwa risasi ikiwa ni ukumbusho wa tukio hilo la kihistoria.


44. TAMATI


Ijumaa mujarab ya leo tarehe 25 Desemba 2020 imetimia miaka 49 toka "Mnyalukolo" SAID ABDALLAH SIULANGA MWAMWINDI amuue kwa risasi RC Dk. WILBERT ANDREW KLERUU, tarehe 25 Desemba 1971.


"MZEE WA ATIKALI" ANAWATAKIA WASOMAJI WAKE WOTE WA "ATIKALI", MAMIA KWA MAELFU, SIKUKUU NJEMA YA KRISMASI!!!



BY MZEE WA ATIKALI✍️✍️✍️


No comments :

Post a Comment