25th December 2012
CCM kimetangaza kuzunguka nchi nzima kuanzia mwakani na kuhusisha viongozi wao kuanzia ngazi ya shina hadi ngazi ya Taifa na kusema kwamba wameshindwa kufanya kazi hiyo mwaka huu kutokana na kuwepo uchaguzi ndani ya chama hicho.
Chadema kimekuwa kikitumia kauli mbiu ya “Nguvu ya Umma” kupitia Movement For Change (M4C) huku Chama cha Wananchi (CUF) nacho kikizunguka mikoani kikitumia falsafa ya “Vugu vugu la Mabadiliko maarufu kama Vission For Change (V4C) kwa ajili ya kujijenga kwa wanachama wake.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dra es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba, alisema kazi ya kuzunguka mikoani kuanzia mwaka 2013, itafanywa na Sekretarieti ya CCM.
“Chadema wao wanasema wanatumia nguvu ya umma, lakini sisi CCM tunasema tutaweza kufanikisha kazi ya kuzunguka mikoani kuangalia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kutumia nguvu ya Mungu,” alisema.
Nchemba alisema kila kiongozi wa CCM katika eneo lake atatakiwa kukagaua miradi iliyotokana na Ilani yao ya mwaka 2010 na kutoa taarifa katika ngazi ya juu huku Sekretarieti iifazunguka mikoani kwa makundi kuangalia utekelezaji wake.
Hata hivyo, Nchemba alikiri kwamba baadhi ya ahadi zilizotolewa na CCM, ikiwamo kununua Meli katika baadhi ya maziwa makubwa pamoja na kujenga majengo ya kusaidia wafanyabaishara ndogo ndogo (Wamachinga), bado zimeendelea kuwa kitendawili.
“Ahadi hizi kubwa inabidi tuwaulize watu wa serikalini ili watuambie imefikia wapi, lakini bado haijatekelezwa mpaka sasa ingawa ahadi hizo zilitolewa na mgombea wetu,” alisema Nchemba.
Wakati CCM kikitangaza mikakati kwa mwaka 2013, mwaka huu pia kilitangaza mpango kama huo na viongozi wake walifanya ziara mbalimbali zilizolenga kuangalia utekelezaji wa Ilani ya CCM wakiwa wameambatana na Mawaziri kwamba hazikuwa na tija wala maana yoyote.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment