05 Dec 2012
Operesheni salimisha silaha yatangazwa
Mali ya mabilioni imeibwa Januari-Sept.
Kasi kubwa ya vitendo vya uhalifu imeitisha serikali na kulazimika kutoa siku 30 kwa mtu au kikundi chochote kinachomiliki silaha kinyume cha sheria kuisalimisha kwa hiyari.
Serikali imesema kuwa ikiwa silaha hizo hazitasalimishwa, utafanyika msako mkali wa kuwakamata wanaozimiliki isivyo halali nchini kote.Silaha hizo zinatakiwa kusalimishwa katika vituo vya polisi, wenyeviti wa vitongoji, vijiji, watendaji wa kata, taasisi za kidini, wakuu wa wilaya na mikoa na kwamba, zoezi hilo linatakiwa kuanza leo hadi Januari 4, mwakani.
Hatua hiyo inafuatia kuwapo kwa tatizo la kuzagaa na matumizi holela ya silaha hizo, ambazo zimekuwa chimbuko la uhalifu, unaohusisha matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha, ambao umekuwa ukijitokeza katika sehemu mbalimbali nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alitangaza amri hiyo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Dk. Nchimbi alisema kumbukumbu zilizopo na taarifa za operesheni zilizofanyika maeneo mbalimbali nchini kuanzia Januari hadi Septemba, mwaka huu, zinaonyesha kuwapo kwa matukio 876 ya uhalifu, ikiwamo unyang’anyi wa kutumia silaha.
Waziri Nchimbi alisema katika kipindi hicho, silaha 62 ziliibwa ama kunyang’anywa kutoka kwa wamiliki wake halali na jumla ya silaha 304 zilikamatwa katika matukio mbalimbali ya uhalifu.
Pia alisema katika kipindi hicho, matukio ya ujambazi yalikuwa ni 876, ambayo yalisababisha vifo 138 vya raia na sita vya askari.
Hata hivyo, Waziri Nchimbi hakueleza idadi ya matukio ya uhalifu kabla ya takwimu alizozieleza jana kutokana na kukataa kujibu maswali ya waandishi wa habari, akisema kuwa kufanya hivyo kungesababisha habari aliyotaka umma ufahamu isipewe uzito na vyombo vya habari.
Vilevile, alisema katika kipindi hicho, jumla ya mali zenye thamani zaidi ya Sh. bilioni 4.5 ziliibwa kwa kutumia silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria, zikiwamo zinazomilikiwa kisheria, lakini zinatumika isivyo halali.
Kwa mujibu wa Waziri Nchimbi, takwimu hizo zinaonyesha kwamba, miongoni mwa jamii kuna baadhi ya watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na isivyo halali.
“Kufuatia hali hiyo, natoa wito kwa mtu yeyote ama kikundi chochote kinachomiliki silaha kinyume cha sheria na isivyo halali hapa nchini kusalimisha silaha hizo katika vituo vya polisi, wenyeviti wa vitongoji, vijiji, watendaji wa kata, taasisi za kidini, wakuu wa wilaya na mikoa,” alisema Dk. Nchimbi.
Alisema hakutakuwa na hatua zozote za kisheria dhidi ya yeyote atakayesalimisha silaha kwa hiari na kwamba, msalimishaji wa silaha hiyo hatabughudhiwa kwa namna yoyote ile.
Hata hivyo, alisema baada ya muda huo kumalizika, operesheni kali itafanyika nchini kote na kwamba, yeyote atakayebainika akimiliki silaha isivyo halali atakamatwa na sheria itachukua mkondo wake.
Operesheni salimisha silaha ilikwisha kufanyika nchini mara kadhaa.
Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokine aliendesha msako kama huo miaka ya themanini; pia aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu, Augustino Mrema naye aliendesha operesheni hiyo miaka ya tisini.
|
No comments :
Post a Comment