NA ROMANA MALLYA
6th January 2013
Jumuiya ya Vijana CUF Taifa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) kwa nyakati tofauti kwenye vikao vyao wameunga mkono na kuishutumu serikali kwa hatua yake ya kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano wa Jumuiya ya Vijana CUF, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Katani Katani, alisema uamuzi wa kupeleka gesi Dar es Salaam haukuzingatia misingi ya kiuchumi.
Katani alisema inasemekana bomba moja la mita tano ambalo litatumika kupitishia gesi hiyo linagharimu kiasi cha Sh. Bilioni tatu.
“Umbali uliopo kati ya Mtwara na Dar es Salaam ni zaidi ya kilomita 560 sasa tukizidisha mara bilioni tatu je, ni kiasi gani kitatumika kwenye mradi huu, kwa nini mabilioni haya yasiokolewe kwa kujenga mitambo ya kufulia gesi Mtwara,” alihoji.
Mwenyekiti huyo alisema ujenzi wa vinu vya kufulia gesi asilia Mtwara utasaidia kuchochea maendeleo ya mikoa ya Kusini kwa kuwahakikishia vijana ajira ambao kila siku hupanga mikakati ya kwenda Dar es Salaam kutafuta maisha bora.
Aidha, Jumuiya hiyo imeeleza kushangazwa na kauli zilizotolewa na viongozi wa serikali huku ikiwakumbusha kauli ya Rais Kikwete ya Julai 25, 2011.
Alisema Rais akihutubia wananchi wa Mtwara, aliwahakikishia katika utawala wake atainua mikoa ya Kusini kiviwanda lakini hadi sasa hauna dalili ya kiwanda kimoja.
Pia jumuiya hiyo imeeleza kushangazwa na taarifa ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuwa asilimia 14 ya gesi iliyogunduliwa ndiyo inayotoka Mtwara na kuhoji kwa nini serikali isipeleke mradi wa bomba la gesi sehemu nyingine.
“Kwa sasa tupo katika mchakato wa kufanya wananchi wa mkoa huu waliopo sehemu tofauti waandamane, tunahamasisha suala hili lifanikiwe ikiwa tu halitafanyiwa kazi,” alisema.
BAVICHA WAUNGA MKONO
Bavicha limeishutumu serikali kwa kuwajengea wananchi wa mkoa wa Mtwara chuki na Watanzania wengine kutokana na kitendo chao cha kupinga bomba la gesi kupelekwa Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya utendaji cha Bavicha kilichoanza jana na kumalizika jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Taifa wa Bavicha, John Heche alisema serikali kupitia waziri wake wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo, wanawatengenezea chuki wananchi wa Mtwara ili waonekane hawaitakii nchi mema.
“Wananchi wa Mtwara walikuwa na kila sababu ya kuandamana kupinga bomba la gesi kusafirishwa Dar, kwa sababu ni moja ya maendeleo yanayopatikana katika mkoa wao…sasa waziri Muhongo anapowashutumu inaonyesha anawagombanisha wananchi hao na Watanzania wengine,” alisema Heche.
MBUNGE APINGA
Mbunge wa Kilwa Kaskazini Murtaza Mangungu (CCM), amesema haungi mkono hatua ya kufanya maandamano ya kupinga ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kwenda jijini Dar es Salaam na badala yake serikali ikae pamoja na wananchi hao ili kulimaliza tatizo hilo.
Kauli hiyo aliitoa jana kwa vyombo vya habari ambapo alisema kuna haja kwa serikali na wananchi kukaa kwa pamoja ili kuweza kujadiliana badala ya kulipinga kwa kutumia maandamano ambayo si kielelezo cha kufikia suluhu.
Mangungu, alisema sekta ya gesi na mafuta ni moja kati ya sekta kubwa kwani imekuwa ikitegemewa na Watanzania wengi ambapo ilitumia muda mrefu kugundulika.
Alisema katika kipindi cha miaka ya 1970 na 1980 serikali ya awamu ya kwanza ilifanya kazi kubwa ya uwekezaji katika utafiti wa mafuta na gesi nchini lakini bila ya mafanikio ya uwekezaji.
“Lakini kwa sasa kiasi kikubwa tumeanza kuona manufaa ya uwekezaji ule japo kwa uchache na changamoto nyingi ndani yake. Tumeanza mwaka 2012 na kumaliza na mfululizo wa matukio ya aina tofauti ikiwemo uchambuzi pamoja na kufutiwa na maandamano ya wananchi wa Mtwara ambao waliweka pembeni itikadi tofauti za vyama vyao,” alisema na kuongeza
“Nilipata wasiwasi mkubwa sana baada ya kuona wanaojua ukweli wa jinsi mambo yalivyo na wale wasiojua kuamua kwa dhati kabisa kuupotosha umma wa Watanzania na dunia kwa ujumla,” alisema
Alisema pamoja na hatua hiyo kuna makubaliano kadhaa ambayo yamewekwa baina ya serikali na kampuni za uwekezaji kwa ajili ya kuendeleza gesi iliyopatikana .
Alisema katika eneo la Rushungi Kilwa kuna kampuni kubwa kutoka Norway na mshirika wake kutoka Marekani wanaofanya uchunguzi wa uwezekano wa kujenga LNG terminal ili kuisindika gesi hiyo na sehemu mbalimbali za mwambao wa Mkoa wa Lindi na Mtwara zinafanyiwa uchunguzi kwa sasa.
Mangungu alisema uwekezaji huo umechelewa kufanyika haswa ukizingatia kuwa gharama zinapanda siku hadi siku, hivyo huwezi kuzuia gesi isipitiswe bila kuwapo kwa sababu za msingi wakati inatumika gharama kubwa mpaka kuipata.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment