NA BEATRICE SHAYO
6th January 2013
Jaji Warioba alisema jana katika mkutano wa waandishi wa habari wakati akitoa tathimini ya awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa maoni iliyofanyika katika mikoa 30 ya Tanzania Bara na Visiwani.
Alisema Tume yake imeanza mchakato wa kuunda mabaraza atakayoyatangaza hivi karibuni na kukutana nayo kwa ajili ya kujadili rasimu na kupokea maoni yao.
Alisema mikutano ya mabaraza ya katiba itafanyika Juni mwaka huu na itahudhuriwa na wajumbe watakaochaguliwa na wananchi kuanzia ngazi ya kijiji. Jaji Warioba alisema wajumbe hao watapaswa kuwakilisha maoni ya wananchi katika mikutano ya mabaraza.
"Kwa sasa tume inakamilisha utaratibu wa namna bora na ya kidemokrasia ya kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ambao utasambazwa nchini kote na kutangazwa katika vyombo vya habari ili wananchi waufahamu," alisema Jaji Warioba.
Alisema kwa sasa wameshamaliza awamu ya nne ya kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba kwa watu binafsi. Alisema jumla ya mikutano iliyofanyika ni 1,776 katika awamu zote nne na kuhudhuriwa na wananchi 1,365,337.
Jaji Warioba alisema kuanzia kesho wanaanza kukusanya maoni ya katiba katika makundi maalamu kuanzia na vyama vyote vya siasa na kufuatia na taasisi zingine zikiwamo za kidini.
Alisema Machi mwaka huu Tume yake itakaa na kufanya uchambuzi wa maoni ili kuandaa rasimu ya katiba kwa ajili ya kuiwasilisha katika mabaraza ya katiba yatakayoitishwa na tume nchini.
Jaji Warioba alisema baada ya wajumbe hao wa mabaraza kuijadili rasimu hiyo tume itakaa na kuipitia kabla ya kuiwasilisha katika bunge maalamu la katiba ambalo linatarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
"Baada ya bunge maalum la katiba kuipitisha wananchi watapata fursa ya kupiga kura ya ndiyo au hapana ili kuidhinisha katiba," alisema Jaji Warioba. Wakati huo huo, Jaji Warioba alisema kuwa tume yake haipo tayari kulumbana na wanasiasa kwani wanakijua wanachokifanya, hivyo waachwe wafanye kazi yao bila kuingiliwa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment