WANANCHI wa Chwaka Mkoa wa Kusini Unguja wamemuomba Rais Kikwete na Dk Shein kushughulikia suala la katiba kwa kurejesha mamlaka kamili na hadhi Zanzibar kama ilivyokuwa zamani kabla ya nchi mbili hizo kuungana.
Maoni hayo yametolewa juzi katika mkutano wa wazi uliofanyika katika Kijiji cha Chwaka Wilaya ya Kati wakati wa kutoa elimu ya katiba na Baraza la Katiba Zanzibar (BAKAZA) katika mfululizo wake wa utoaji wa elimu juu ya katiba kwa wananchi wa Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano huo Mzee Fadhil Mussa Haji alisema kwa kuwa suala la kuunganisha nchi limefanywa na watu wawili ambao ni Mwalimu Nyerere na Mzee Karume na wote wameshakufa hakuna budi viongozi waliopo madarakani kulishughulikia ipasavyo ili wananchi wa pende mbili hizo waweze kuishi kwa amani bila yamanunguniko.
“Mwalimu Nyerere na Mzee Karume waliunganisha nchi kwa kuamua wao wenyewe na kisha Mzee Karume akaja uwanja kutuuliza mnakubali union watu wakaitikia kwa kuwa akijua hakuna atakayeweza kupinga kwa wakati ule lakini sisi hatujakubaliana na hayo tokea wakati huo, sasa kilichobaki tunamuomba Rais Kikwete na Rais Shein wao ndio wapo madakarakani waturejeshee mamlaka na hadhi ya Zanzibar” alisema Mzee huyo huku akipigiwa makofi na vijana waliohudhuria katika mkutano huo.
Mzee Haji alisema yapo baadhi ya mambo ambayo yameingizwa katika orodha ya mambo muungano bila ya ridhaa ya wazanzibari lakini baadhi ya mambo wazanzibari wenyewe ndio walioshriki kuizamisha nchi yao kutokana na tamaa na kupenda madaraka jambo ambalo amesema hivi sasa linawafanya wajue.
“Ni sisi wenyewe tumefanya na tumetaka tutendewe hivi kwa sababu sisi tulikuwa tumeshapata uhuru wetu hapa mwaka 1963 lakini ni wazanzibari wenyewe wakaleta mapinduzi na kuukataa ule uhuru halali sasa tunasema hizi tamaa na kupenda madaraka sasa hivi ndivyo vitu vinavyotuadhibu sote katika nchi yetu kwa tamaa za hao wachache waliokuwa wakitumulia” aliongeza Mzee Fadhil ambaye ni mtu mzima.
Akitoa mfano wa wazanzibari walivyojikaanga na mafuta yao wenyewe alisema ni tamaa ndizo zilizosababisha mambo yote hayo ya nchi kutokuwa na hadhi na kuporwa mamlaka yake kamili na hivyo kubakisha nchi ambayo haina mamlaka ya kujiamulia wala kujipangia mambo yake huku akitoa mifano ya wazanzibari wanavyokosa uwakilishi kwa yale mambo ambayo sio ya muungano yanavyokwenda kuwakilishwa nchi za nje.
Alisema ni wakati sasa wa kila mmoja kufahamu kwamba mamlaka ya Zanzibar yanahitaji kuheshimiwa na kila raia na kupiganiwa ili hadhi ya Zanzibar irudi na iweze kujiamulia ambapo alipendekeza katiba mpya utakapokuja iweke bayana mamlaka ya Zanzibar na rais wake kwani rais wa Zanzibar hana hadhi hivi sasa.
Mzee Haji alisema hakuna ubishi kwamba baadhi ya wazee walikataa nchi mbili kuunganishwa na hawakuwa wakipenda kwa kukhofia mambo matatu muhimu wakati huo lakini bahati mbaya watawala walikuwa tayari wameshaamua na hivyo hakukuwa na hila kwa wananchi kwa kuwa ni maamuzi ya watawala wa wakati huo.
“Haya yanayotokea sasa yalijulikana na wazee wetu walikuwa wakiyapinga walisema nchi hii isipelekwe bara kwa sababu walijua mambo matatu hayo yatakuwepo uzanzibari utapotea, ukiristo utashamiri na kodi itapanda na hayo yote kwa Zanzibar halikuwa yakiogopwa sana na wazanzibari wenyewe” alisema Mzee huyo mbele ya vijana waliohudhuria katika mkutano huo.
“Ni jambo la kusikitisha sana sana tupo tu hatuna mamlaka yoyote na huyo rais wetu hana nafasi yoyote ya heshima na hadhi inayostahiki kuonekana au kupewa kama rais sasa nadhani katiba iweke wazi hilo na wazanzibari tumaaajiii na hata tukitaka kujikwamua hatuwezi wallah hatuwezi” Mzee Haji alisema huku akishangiriwa.
Nae kwa upande wake Mohammed Nuur Mohammed alisema wanasheria wengi wanakubaliana kwamba kutokana na kukiukwa kwa hati ya muungano basi muungano huu sio halali na hivyo hakukuwa na haja ya wananchi kuja kutakiwa kutoa maoni yakatiba na badala yake walikuwa wahojiwe iwapo wanautaka muungano au laa.
“Huu muungano sio halali ndio wanasheria wanavyosema kwa hivyo basi hatuna haja ya kujadili au kutoa maoni ya katiba lakini tuulizwe kama tunautaka muungano au hatuutaki kwisha” alisema Nuur.
Katika hatua nyengine Nuur alionesha khofu yake katika kipengengele cha sheria cha kutozungumza Muungano kimeongewa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba ambapo alisema hakimo katika hadidu rejea.
“Kipengele hiki cha kujadili muungano hakimo katika sheria kimeletwa na Jaji Warioba sasa jee haya maoni yetu ya muungano tunayotoa haitakuwa sisi tunapoteza muda tu” alihoji Nuur.
Akitoa ufafanuzi katika mkutano huo Professa Abdul Sheriff alisema ni kweli awali katika hadidu rejea kulikuwa na suala hilo kwa tume kuwataka wananchi wasijadili muungano lakini haingekuwa rahisi watu kutoa maoni yao juu ya katiba bila ya kugusa suala la muungano.
Aidha Professa Sheriff aliwaambia wananchi katika mkutano huo kwamba kitu muhimu kwa wazanzibari kuzungumzia katika katiba hiyo ni kwa yale ambao mambo ya muungano ndio wanapaswa kutoa maoni yao na mambo ambayo sio ya muungano hawatakiwi kuyagusa kwa kuwa hayawahusu.
Professa alisema mchakato huu wa katiba umewapa mamlaka wananchi kuamua juu ya mustakabali wa nchi yao hivyo bado kuna hatua ya kura ya maoni mwisho wa kuandikwa katiba mpya na hivyo wananchi wataulizwa kama wanakubaliana na katiba mpya au laa na hivyo kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo vilivyo.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Sheha wa Shehia ya Chwaka Simai Msaraka Pinja na Naibu Sheha Simai Mvuma Simai na wananchi mbali mbali wakiwemo wanafunzi wa Chuo Cha Fedha Chwaka.
Chanzo: ZanzibariYetu
No comments :
Post a Comment