NA ELIZABETH ZAYA
22nd March 2013
Rais Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kuwa makini na watu wanaoisema nchi vibaya.
Alitoa wito huo jana alipofanya ziara na kuzindua jengo la umoja wa vijana wa Kikiristo Tanzania (Uvikiuta) katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Alisema limekuwa jambo la kawaida watu kuona fahari kuisema vibaya nchi yao badala ya kuweka uzalendo mbele.
“Siku hizi watu wanaona fahari kuisema na kuiponda vibaya nchi yao na hata kuwashabikia na kuwashangilia wale watu wanaoisema vibaya nchi, sijui tuliteleza wapi?” alihoji na kuongeza:
“Kuna mahali tumepotoka kwa sababu kipindi sisi tunakua, hatukukubali kuona mtu yeyote anaisema vibaya nchi, tulikuwa na moyo wa kujituma na kufanya kazi kwa ajiri ya nchi yetu tofauti na ilivyo sasa.”
Aidha alitembelea Hospitali ya Temeke na kuzindua jengo la huduma ya mama na mtoto na kuitaka sekta ya afya nchini kufanya mara moja mchakato wa kutafuta eneo la kujenga jengo maalum ambalo litatumika kutoa huduma za akina mama wajawazito na watoto.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment