HALI ya uchumi wa Zanzibar ni ya kusikitisha mno. Na inazidi kusikitisha kwa vile sasa ni takriban nusu karne baada ya Mapinduzi yaliojigamba kuwa moja ya malengo yake lilikua lengo la kuunyanyua uchumi wa Visiwa hivyo. Lakini badala ya kunyanyuka uchumi huo umekuwa ukiporomoka…
Nani wa kulaumiwa kwa hali hii? Hili ni swali ambalo jibu lake halina utata kwani kwa kiwango kikubwa — tena kikubwa sana — sera za kiuchumi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kiwango fulani zile za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ndizo zilizochangia pakubwa hata uchumi huo ukawa hivi ulivyo, uliooza kama ulivyooza. Na uoza huo ndio wenye kuyafanya maisha ya kila siku ya Wazanzibari yawe magumu laisa kiasi.
Sisemi kwamba katika muda wote huu unaokaribia miaka 50 hakuna walionufaika Zanzibar. Wapo. Nao ni wale wachache walio ngazi za juu serikalini au waliogaiwa ekari tatu tatu za ardhi na serikali. Lakini Wazanzibari wengi wamekuwa na maisha ya dhiki.
Ushahidi u wazi na umekuwa wazi kwa muda wote huu. Wakati ushahidi huo ukiwa unatukodolea macho hakuna ushahidi wowote wenye kuonyesha kwamba serikali hizo mbili zimechukua hatua za pamoja za kuustawisha uchumi wa Zanzibar ambao kwa kweli tukiuangalia kwa kina ni uchumi uliotengeka na ule wa Bara.
Zanzibar ina sifa nyingi zinazoweza kuifanya iwe nchi tajiri. Kwanza kijiografia iko pahala pazuri katika sehemu hii ya Afrika. Pili idadi ya watu wake ni ndogo ukiilinganisha na idadi ya visiwa vingi vingine duniani vilivyopata ufanisi wa kiuchumi. Na tatu ni kwamba ingawa idadi ya watu wake ni ndogo lakini hao watu wake ni watu wanaoweza kufunzwa wakafunzika kufanya kazi katika nyanja mbalimbali kwa mfano katika karakana na viwanda vidogo vidogo.
Hizo ni sifa tatu tu na ziko nyingine kadhaa zinazoweza kuifanya nchi hiyo iwe tajiri. Kwa upande mwingine kuna sababu moja kuu inayoirejesha nyuma nchi hiyo badala ya kuiendeleza.
Sababu yenyewe ni kutojali kwa serikali zote mbili za Muungano na Zanzibar kwamba maisha ni magumu Visiwani. Hii leo wengi wa wakaazi wa Zanzibar, hasa vijana, hawana ajira. Hivyo sehemu kubwa ya wananchi wa huko hawana mbele hawana nyuma, wanajiendea tu.
Ukweli ni kwamba wananchi hao hawatoweza kuwa na mustakbali mzuri ila ikiwa serikali hizo mbili zitachukua hatua za dharura na kutunga sera zifaazo zilizo endelevu zenye lengo la kuviendeleza Visiwa hivyo na kuzuia uporomokaji wa hali za kiuchumi na kijamii.
Inafaa tukumbushe kwamba Serikali ya Muungano inawajibika kuwa na jukumu kubwa zaidi kuhusika na uchumi wa Zanzibar kwa sababu yale mambo 22 yaitwayo ‘Mambo ya Muungano’ yanahusika zaidi na shughuli za kiuchumi na za kijamii na SMZ imenyimwa madaraka ya kuyashughulikia mambo hayo.
Miongoni mwa hayo ‘Mambo ya Muungano’ ambayo Zanzibar kwa muda wa miaka 50 haikuwa na ubavu nayo na ambayo Serikali ya Muungano ina nguvu juu yake ni:
a. Mikopo na Biashara ya nchi za nje.
b. Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
c. Kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha.
d. Bandari, mambo yanayohusika na Posta na Simu.
e. Mambo yote yanayohusika na Sarafu na Fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti). Benki pamoja na benki ya kuweka akiba na shughuli zote za benki, fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni.
f. Leseni ya viwanda na takwimu.
g. Elimu ya juu.
h. Mali asili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta aina ya petroli na aina nyenginezo za mafuta au bidhaa na gesi asilia.
i. Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania na mambo yote yanayohusika na kazi za baraza hilo.
j. Usafiri na usafirishaji wa anga.
k. Utafiti.
l. Utabiri wa hali ya hewa.
m. Takwimu.
b. Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
c. Kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha.
d. Bandari, mambo yanayohusika na Posta na Simu.
e. Mambo yote yanayohusika na Sarafu na Fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti). Benki pamoja na benki ya kuweka akiba na shughuli zote za benki, fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni.
f. Leseni ya viwanda na takwimu.
g. Elimu ya juu.
h. Mali asili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta aina ya petroli na aina nyenginezo za mafuta au bidhaa na gesi asilia.
i. Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania na mambo yote yanayohusika na kazi za baraza hilo.
j. Usafiri na usafirishaji wa anga.
k. Utafiti.
l. Utabiri wa hali ya hewa.
m. Takwimu.
Serikali ya Zanzibar haina nguvu yoyote katika kila jambo lililo katika hiyo orodha ya ‘Mambo ya Muungano’. Nguvu zote zenye kuhusika na mambo hayo zimo kwenye serikali ya Muungano.
La kusikitisha, kwa sababu lingeweza kuepukika, ni kuwa serikali hiyo imeshindwa kuzitumia nguvu hizo kwa manufaa ya Zanzibar. Hiyo kama nilivyokwishagusia ndiyo sababu kubwa ya kuzorota kwa hali za kiuchumi na kijamii huko Zanzibar.
Hiyo pia ndiyo sababu kubwa inayowafanya Wazanzibari wasiwe na hamu na Muungano na yenye kuwahamasisha wadai pafanywe mageuzi makubwa na ya kimsingi katika mahusiano baina ya Tanganyika na Zanzibar. Ndiyo sababu kubwa inayowafanya wadai warejeshewe mamlaka kamili ya nchi yao ili Serikali ya Zanzibar iwe na nguvu ya kujipangia namna ya kuuokoa uchumi wake na shughuli zake za kijamii.
Kuna hoja kubwa ya kwa nini Zanzibar inapaswa kuiiga mifano ya visiwa vingine duniani na ifuate sera itayoifanya iwe nchi ya bandari huru na hatimaye iwe nchi isiyo na ushuru. Hatua hizo zitajenga msingi wa maendeleo ya haraka ya kiuchumi na ustawi wa kijamii, zitajenga uwezo na zitasaidia kurejeshwa kwa viwango vya hali ya juu katika sekta ya elimu.
Hili la mwisho ni muhimu sana kwani ikiwa Wazanzibari hawatopatiwa mafunzo muafaka na wakapikwa wakapikika basi watazikosa fursa zitazopatikana pale uchumi utapokuwa unafufuka.
Katika mfumo wa kiuchumi wa bandari huru viwango vya utozwaji kodi na ushuru wa forodha vitabidi vishushwe ili serikali iweze kuukuza uchumi na iwe na raghba ya kuyatanzua matatizo yaliyopo ya kiuchumi na ya kijamii. Yakifanyika hayo Zanzibar itakuwa na ustawi wa haraka wa kiuchumi, zitapatikana fursa za kuwapatia watu ajira na kwa jumla Wazanzibari watanufaika kutokana na mfumo wa uchumi ambao soko lake litakuwa na bidhaa za bei ya chini.
No comments :
Post a Comment