NA JESSE KWAYU
18th March 2013
Asimulia mkasa mzima hospitalini A. Kusini
Asema anahisi kilichomponza ni taaluma yake
Akizungumza na NIPASHE jana hospitalini alikolazwa kwa matibabu alisema kuwa baada ya kujitahidi kupambana na wavamizi waliomshambulia na kuona wakizidi kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili, alitambua dhahiri kwamba nia ya waovu hao ilikuwa ni kutoa uhai wake.
“Nakwambia baada ya kujaribu kupambana na wale jamaa nikijaribu kuwazuia dhidi ya mashambulizi yao, wawili wakinishambulia huku mmoja akiwa kando, niliona dhahiri nia yao ilikuwa ni uhai wangu,” alisema Kibanda.
Alisema watu walionivamia walikuwa wamevaa kofia za sweta, lakini ambazo hazikuwa zimefunika uso, lakini akasema hawezi kukumbuka sura zao kwani kulikuwa na giza.
Alisema watu walionivamia walikuwa wamevaa kofia za sweta, lakini ambazo hazikuwa zimefunika uso, lakini akasema hawezi kukumbuka sura zao kwani kulikuwa na giza.
Pia aliongeza kuwa baada ya kitambo alipoteza fahamu na alipopata fahamu alikuta jicho likiwa limeharibiwa vibaya.
“Ninahisi kuwa wale jamaa walikuwa wamejibanza nje ya nyumba yangu. Kwa muda mrefu nilikuwa nimedokezwa na rafiki yangu mmoja kuwa ninapokwenda nyumbani niwe mwangalifu kuangalia nani hasa yuko nyuma yangu usiku. Siku ile sikuona kama kuna watu wananifuatilia,” alisema Kibanda.
“Nilipofika getini nilipiga honi mara mbili, nikiwa nasubiri nilisikia kishindo kikubwa cha kuvunjwa kwa kioo cha mlango wa gari upande wa dereva, kile kishindo kilinishtua, nilipotoka kwa upande wa mlango wa abiria wa mbele, nikaanza kukimbia niliteleza na kuanguka. Waliniwahi na kuanza kunishambulia kwa nia ya kuniteketeza kabisa,” alisema Kibanda akielezea jinsi waovu hao walivyokuwa wanataka kumuondoa duniani.
Alisema anachokiamini ni kwamba shambulizi dhidi yake linatokana na kazi yake ya uandishi wa habari ijapokuwa hafahamu ni kazi ipi ambayo inaweza kuwa kichocheo cha kujeruhiwa kwake.
Kibanda alitekwa na watu wasiofahamika mapema mwezi huu na kisha kumjeruhi vibaya kwa nondo, mapanga na kisha kumng’oa meno, kucha na kumharibu jicho la kushoto.
Tukio hilo la kinyama linafanana kwa kiasi fulani na lile la alilofanyiwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania, Stephen Ulimboka.
Kibanda alipatwa na mkasa huo wakati akirejea nyumbani kwake Goba Punguni, Kata ya Mbezi Juu, kutoka kazini.
Tayari mwandishi huyo mkongwe wa habari, amesafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Aliondoka akisindikizwa na daktari kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimu (MoI).
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment