Posted Alhamisi,Marchi21 2013 saa 9:46 AM
KWA UFUPI
Mahakama itachukua hatua zote zinazohitajika kuhakikisha kuwa mtuhumiwa huyo anafikishwa haraka mjini The Hague
Fadi El-Abdullah
Kongo. Kiongozi wa wapiganaji wa M23 ambao wamekuwa wakipambana dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo (DRC), Jenerali Bosco Ntaganda amejisalimisha katika Ubalozi wa Marekani mjini Kigali, ikielezwa kwamba uamuzi huo unatokana na kuhofia usalama wake.
Hatua hiyo ilitokana na kushindwa kwa Ntaganda na kamanda mwingine wa waasi, Sultan Makenga siku ya Jumamosi baada ya wiki kadhaa za msuguano ndani ya M23, kundi la waasi la hivi karibuni kuongozwa na Watutsi dhidi ya Serikali ya mbali.
Uasi wa M23 katika Mkoa wa Kivu Kaskazini wenye utajiri mkubwa wa madini, ulisababishwa na mipango ya Rais Joseph Kabila kumkamata Ntaganda na kumkabidhi kwa ICC. Taarifa zinaeleza kwamba kiongozi huyo aliamua kujisalimisha kwenye Ubalozi wa Marekani nchini Rwanda, baada ya kuripotiwa kuvuka mpaka Jumamosi iliyopita, ambapo Serikali ya Rwanda ilikana kumkamata.
Shirika la habari la AFP lilieleza kwamba Ntaganda aliamua kujisalimisha baada ya kundi la wapiganaji alilokuwa akiliongoza kuzidiwa nguvu kutokana na vita ya ndani iliyoligawanya Kundi la M23.
Ntaganda alikuwa kiongozi wa kijeshi aliyemuunga mkono aliyekuwa kiongozi wa kisiasa wa kundi la M23 Jean Marie Runiga ambaye aliripotiwa kukamatwa Jumamosi na kuhifadhiwa sehemu maalumu baada ya kukamatwa na wanausalama wa Rwanda alipovuka mpaka kuingia nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Rwanda, Ntaganda aliamua kujisalimisha kwa Ubalozi wa Marekani mjini Kigali kwa kuhofia usalama wake iwapo angeingia mikononi mwa Serikali ya Rwanda.
Mmoja wa maofisa wa Jeshi la Rwanda ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kwamba, “Nina uhakika kwamba anatuogopa sisi kuliko anavyoiogopa Marekani kwa sababu amekuwa akitusababishia migogoro mingi na jirani zetu.”
Ofisa huyo alisema kwamba maelezo ya awali yaliyokuwa yakitoka kwa watu wake wa karibu yalikuwa yakieleza kwamba alikuwa amepotolea misituni lakini yalikuwa yakitiliwa shaka na wanausalama wa Serikali ya Rwanda.
Kwa kujisalimisha mjini Kigali, ambako ofisa mmoja wa ubalozi alisema wafanyakazi walishtushwa na kuwasili kwake kwa ghafla, Ntaganda amehitimisha safari ndefu iliyomshuhudia akipigana kama muasi na mwanajeshi wa Serikali kwa pande mbili za mpaka wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, wakati wa mgogoro wa karibu miaka 20 katika Kanda ya Maziwa Makuu.Uwepo wa Ntaganda ulikuwa haujulikani baada ya mamia ya wapiganaji wake kukimbilia nchini Rwanda na wengine kujisalimisha kwa Umoja wa Mataifa mwishoni mwa wiki, baada ya kushindwa kwake na kundi hasimu la M23 walilojitenga nalo.
Msemaji wa ICC, Fadi El-Abdullah alisema mahakama hiyo itachukua hatua zote zinazohitajika kuhakikisha kuwa mtuhumiwa huyo anafikishwa haraka mjini The Hague na kuongeza kuwa hakuna kizuizi kwa taifa lisilo mwanachama wa mahakama hiyo kushirikiana nayo kwa msingi wa kujitolea.
Rwanda na Marekani zote siyo wanachama wa ICC na kwa hivyo haziwajibiki kumkabidhi Ntaganda, lakini Nuland alisema nchi yake inaunga mkono.
No comments :
Post a Comment