NA MUHIBU SAID
20th March 2013
Baadhi ya maofisa waandamizi wa Kitengo cha Itifaki cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wameshushwa vyeo, wengine kukatwa mishahara na wengine kupewa onyo, baada ya kubainika kuhusika na tuhuma za uzembe na nia ya kutaka kuiba Sh. bilioni 3.5 kutoka Hazina.
Miongoni mwa maofisa waliobainika kuhusika na tuhuma hizo, yumo pia Mkuu wa Kitengo hicho, Balozi Anthony Itatiro.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mahadhi Juma Maalim, aliiambia Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa jana kuwa, wizara haina mamlaka ya kumchukulia hatua Balozi Itatiro na kwamba, hatma yake inasubiri mamlaka ya Rais.
Mahadhi alieleza hayo baada ya kutakiwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Edward Lowassa, kueleza hatima ya maofisa hao, katika kikao kati ya watendaji wa wizara walioongozwa na naibu waziri huyo, katika ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam jana.
Mahadhi alieleza hayo baada ya kutakiwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Edward Lowassa, kueleza hatima ya maofisa hao, katika kikao kati ya watendaji wa wizara walioongozwa na naibu waziri huyo, katika ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema maofisa hao walibainika kutaka kuiba fedha hizo, kufuatia ukaguzi uliofanywa na wakaguzi wa ndani ya wizara hiyo pamoja na uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru).
Fedha hizo zilitolewa Hazina kati ya Machi 1 na 8, mwaka jana na kwa mujibu wa naibu waziri huyo, zilitengwa na maofisa hao kwa ajili ya safari hewa za nje za viongozi wa serikali.
Taarifa za awali zilieleza kuwa, maofisa hao walitenga fedha hizo kwa ajili ya safari za Rais Jakaya Kikwete kwenda Geneva, Brazil, Adis Ababa na Arusha.
“Kwa bahati mbaya fedha hizo ziliombwa wakati waziri hayupo, naibu waziri hayupo, katibu mkuu hakuwapo wala naibu katibu mkuu hakuwapo. Wote walikuwa nje ya kituo,” alisema Mahadhi wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo jana.
Alisema aliyekuwapo wizarani wakati fedha hizo zinaombwa na maofisa hao kutoka Hazina, ni kaimu katibu mkuu wa wizara hiyo.
Hata hivyo, alisema fedha hizo zilipatikana, kwani baada ya viongozi wa wizara, akiwamo waziri, naibu waziri, katibu mkuu na naibu wake kurudi, waligundua kuwapo kwa fedha hizo wizarani, ambazo hazijaguswa na kwamba, zote bado zipo.
“Lakini tukaweza ku-establish (kugundua) kwamba, safari hizo hazikuwapo. Kwa hiyo, tukaona kwamba, kuna mazingira ambayo yanatia wasiwasi. Na ndiyo maana tukataka sasa uchunguzi wote wa wakaguzi wa ndani wa hesabu pamoja na Takukuru wafanye kujiridhisha kama taratibu zilizotumika na kama fedha hizo zilizoombwa kama kuna zilizotoka,” alisema Mahadhi.
Alisema katika uchunguzi huo, ilibainika kuwa fedha zote zilikuwapo na kwamba hakukuwa na fedha yoyote iliyotumika.
Hata hivyo, alisema hawakuishia hapo, bali walitaka kujiridhisha zaidi kama utaratibu uliotumiwa na maofisa hao kuziomba na kuzipata fedha hizo ulikuwa ni wa kawaida au la na lengo lilikuwa lipi.
“Sasa ndiyo katika uchunguzi imeonekana kwamba, kulikuwa na uzembe katika utaratibu wa kuziomba na kuzipata fedha hizo. Lakini pia kulikuwa na ni ya kuiba,” alisema Mahadhi.
Alisema wakaguzi hao pamoja na Takukuru wana utaalamu, lakini imeonekana kuwa kwa ushahidi uliopo, kama itaamuliwa kufunguliwa kesi ya jinai mahakamani dhidi ya maofisa hao, itakuwa vigumu kuthibitisha bila kuacha shaka yoyote kulingana na 'vionjo' vya mahakama vya kujiridhisha na ushahidi.
“Kwa hiyo, unaweza kushindwa kuthibitisha. Lakini hatua za kiutawala za kinidhamu zinaweza kuchukuliwa kwa sababu mazingira yanaonyesha kuna kosa la kiutawala,” alisema Mahadhi.
Alisema katika uchunguzi huo, kuna baadhi ya maofisa wa kitengo hicho walionekana hawahusiki moja kwa moja na wengine wanahusika katika viwango tofauti katika tuhuma hizo.
Hata hivyo, naibu waziri huyo alisema maofisa wote wamerudi kazini.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment