Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, March 21, 2013

Uchaguzi wa Kenya somo kwa Zanzibar

Na Salim Said Salim

WATU wengi wa Zanzibar walifuatilia kwa karibu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya.
Kutokana na mazungumzo yao inaonekana wamejifunza mengi. Lakini sijui kama wale ambao hawataki kujifunza wamekuwa tayari kubadilika.
Yapo mambo mengi yaliyowasababishia watu wa Visiwani kufanya hivyo, mojawapo ni ujirani na uhusiano wa karibu walionao na watu wa Mombasa, eneo ambalo zamani lilikuwa sehemu ya Zanzibar, lakini chini ya himaya ya Serikali ya Ungereza.
Kubwa zaidi ni kwa sababu Kenya, kama Zanzibar, ilipata mtihani mkubwa tokea kuachana na siasa za chama kimoja na kuja mfumo wa vyama vingi vya siasa miongo miwili sasa.
Wakati chaguzi Zanzibar ziligharimu maisha na hasa katika mwaka 2001, Kenya nayo ilikuwa na vurugu ulipofanyika uchaguzi wa mwaka 2007 na mamia ya watu kuuawa na kupata hasara kubwa za mali.
Wakati vurugu za Zanzibar zilisababisha mamia ya watu kuwa wakimbizi Mombasa, Kenya na nchi nyingine, ikiwemo Somalia, zaidi ya Wakenya 600,000 walihama sehemu walizozaliwa au kuishi kwa miaka mingi na kwenda kwengine kuanza maisha mapya.
Hivi sasa baadhi ya viongozi wa Kenya wamefunguliwa mashitaka ya kuchochea mauaji yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambayo baada ya mvutano yalisababisha kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Tuombe Mungu na viongozi wetu na waandishi wa habari wasijisahau hata kulazimika jumuiya ya kimataifa kuwawajibisha kisheria.
Nayo Zanzibar, labda kwa kujifunza kutokana na balaa za uchaguzi walizokumbana nazo na yaliyotokea Kenya, nayo ilipata mwafaka uliosababisha kufanyika uchaguzi wa amani mwaka 2010 na baadaye kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Kwa bahati mbaya inaonekana wapo ambao hawakufurahia hili na tayari panasikika na kuonekana chokochoko za kuleta balaa.
Badala yake ni viongozi wa Uamsho tu ndio unaosikia wanachunguzwa na polisi, lakini hatuelezwi kinachoendelea juu ya vikaratasi vya uchochezi na matusi yaliyoporomoshwa kwa marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Amani Abeid Karume. Sijui viongozi waliopo madarkani hivi sasa (Bara na Visiwani) watahisi vipi na wao wakija kukashifiwa katika vikaratsi watakapoachia ngazi za uongozi.
Sasa Kenya baada ya kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa imefanya uchaguzi ambao nao umekuwa na shaka kutokana na kuwepo kwa madai ya mizengwe wakati wa kuhesabu kura.
Hata hivyo, watu wake wamekataa uchaguzi kuwarudisha kwenye vurugu za kutoana roho. Badala yake malalamiko ya uchaguzi yamepelekwa mahakamani kwa sababu sheria ya uchaguzi inatoa fursa hiyo, tofauti na ilivyokuwa kabla ambapo uamuzi wa tume ni wa mwisho na hauwezi kupelekwa mahakamani.
Hili ni eneo ambalo Tanzania na hasa Zanzibar inafaa kuliona kama somo kwa vile kutotoa nafasi kwa uamuzi wa Tume ya Uchaguzi kuhojiwa si demokrasi bali ni udikteta.
Lakini zuri zaidi ni kuwa kesi za uchaguzi, hasa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais zitasikilizwa katika kipindi cha sio zaidi ya wiki mbili tokea matokeo kutolewa.
Vilevile kesi zote zinazohusu uchaguzi zitasikilizwa hata siku za mapumziko na hadi usiku.
Hapa kwetu na hasa Zanzibar kesi za uchaguzi hupigwa tarehe kutoka uchaguzi mmoja hadi ufikie mwengine.
Hii si demokrasia wala utawala bora. Ni vizuri tukajifunza kutoka Kenya.
Uchaguzi uliopita wa Kenya ulikumbana na matatizo ya kiufundi ya teknolojia, lakini palikuwepo uwazi wa kiasi fulani na wananchi kuelewa kilichokuwa kikiendelea, tofauti na Zanzibar ambapo ukimya hutanda na kusababisha kuwepo kila aina ya uvumi.
Ukweli ni kwamba Kenya imefanya marekebisho makubwa katika kuendesha uchaguzi, ijapokuwa bado inayo safari ndefu.
Hapakuwa na malalamiko ya watu wengi kunyimwa haki ya kupiga kura kama inavyoendelea kuonekana Zanzibar na wala hazikusikika habari za wapiga kura mamluki kupelekwa vituoni.
Kenya ilikwenda hatua moja mbele zaidi ya hata kuwa na Jimbo la Uchaguzi wa Rais kwa raia zake wanaoishi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hii ni tofauti na Zanzibar ambapo watu zaidi ya 40,000 walinyimwa haki hiyo licha ya sio tu kuzaliwa Zanzibar, bali wengine wakiwa hawajawahi hata kusafiri nje ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Katika uchaguzi wa Kenya maofisa wa uchaguzi ndio waliokuwa wakifanya uamuzi katika vituo vya kupiga kura, tofauti na Zanzibar ambapo masheha ndio wenye uamuzi wa nani awe na haki ya kupiga kura.
Hawa masheha wamelaumiwa sana, hata na wachunguzi wa uchaguzi wa ndani na nje, kuwa ndio waliokuwa tatizo na kuwa chanzo cha vurugu.
Baadhi yao bila ya aibu wamekuwa wakidai hawawajui watu wanaoishi mitaani kwao na hata vijana waliowaozesha binti zao. Ni watu wanafiki kwa kiwango ambacho hakielezeki.
Kinachosikitisha ni kwamba hakuna hata sheha mmoja aliyechukuliwa hatua za kisheria kwa kusema uongo na hapakuwepo taarifa ya kufanyika uchunguzi juu ya madai kuwa baadhi ya masheha walitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa uchaguzi.
Badala yake tuliona mamia ya watu wakifunguliwa mashitaka bandia, ikiwa hata vizee kudaiwa kuwanyang’anya silaha polisi.
Askari wa Jeshi la Polisi Kenya walionekana kila pembe, lakini walikuwa hawaingilii shughuli za uchaguzi au kutisha wananchi.
Katika chaguzi za Zanzibar, askari wa SMZ walikuwa ndani ya vyumba vya kupigia kura kama vile wao ni makarani wa Tume ya Uchaguzi.
Nimeyaona hayo Unguja na Pemba na nilipowauliza maofisa wa Tume ya Uchaguzi walinieleza ati wanalinda usalama.
Wagombea nao walionesha uungwana wa hali ya juu kwa kila mmoja kuweka uzalendo mbele na sio utashi wa kisiasa licha ya kutoridhika na baadhi ya matokeo, kama madai kuwa baadhi ya vituo vilipokea wapiga kura masaa kadha baada ya muda unaoruhusiwa kwa mpiga kura kufika kituoni.
Kwa upande mwingine, vyombo vya habari vya Kenya, hata vile vya umma, havikuonyesha utashi mkubwa wa kisiasa kama unavyoonekana katika chaguzi za Zanzibar.
Jingine ambalo Zanzibar inapaswa kujifunza ni kwamba uchaguzi ulikuwa wa watu wazima, wale waliofikia umri wa miaka 18 na kuendelea, wakati Zanzibar watoto ambao umri wao hauwaruhusu kuwa wapiga kura walishiriki.
Moja ya kambi maarufu iliyotumika kufanya mizengwe ni katika jengo lililokuwa kiwanda cha viatu hapo Mtoni, mjini Unguja.
Nani aliwakusanya watoto hao na walitoka wapi wanajuwa hao waliofanya hayo, lakini ukweli ni kwamba walikuwepo hapo na walipoulizwa na waandishi wa habari walikuwepo hapo kufanya nini jawabu yao ilikuwa waliwekwa hapo ili wapige kura.
Nilipowauliza walitokea wapi waliniambia wengi wao walitoka Kunduchi, Kawe na maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.
Wapo watu ambao huwa wanachukia haya yakielezwa eti kwa madai anayefanya hivyo anatonesha vidonda, lakini ukweli ni kwamba uchafu huu umefanyika na kama walikuwa hawataki yazungumzwe basi wasingefanya madhambi haya.
Ukweli lazima usemwe na kurudiwa ili wasitoke tena vidudu mtu vya kutufanyia manyago yatakayosababisha Zanzibar kurejea katika mizengwe ya uchaguzi.
Wakati tunaelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 ni vizuri kujifunza kwa yaliyotokea siku za nyuma na mamia ya watu kuuawa, na hatua zilizochukuliwa na Kenya katika uchaguzi wake ili kuinusuru Zanzibar na kuwapa watu wake nafasi ya kusonga mbele.
Viongozi wa Zanzibar wanapaswa kuelewa kama wanakataa kujifunza na kushikilia kwamba ushindi lazima, hata ikiwa kwa kufanya mizengwe, basi dunia itawafunza baadhi ya wakati kwa njia ambazo zitawadhalilisha.
Tusisahau wazee walivyotuasa kwa hekima na busara kwa kutuambia: “Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu.”
Chanzo: Tanzania Daima

No comments :

Post a Comment