Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa jengo la watu wa kijiji cha Kibokwa Mkoa wa Kaskazini Unguja, “SAEMAUL COMMUNITY HALL”.
- Kibokwa na Kiuyu vitakuwa vijiji vya mfano kwa Zanzibar
Tarehe 27 na 28 Februari mwaka 2013, zilikuwa ni tarehe muhimu sana katika mwelekeo wa ujenzi wa Zanzibar mpya kimaendeleo. Ni tarehe hizo ambapo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alifungua rasmi jengo la watu wa kijiji cha Kibokwa Mkoa wa Kaskazini Unguja, chini ya udhamini wa serikali ya Korea ya Kusini, pamoja na kuweka mwelekeo mpya wa kijiji cha Kiuyu Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Al-Yousef.
Katika makala hii, nitaelezea ni kwa namna gani maendeleo ya vijiji yanaweza kubadili mwelekeo wa maendeleo ya nchi nzima kama ilivyotokea kwa vijiji vya Korea na Saudi Arabia, huku tukiangalia vijiji vya Kibokwa na Kiuyu kama vijiji mfano vinavyoweza kubadili mwelekeo wa Zanzibar.
Na Hassan Hamad, OMKR Zanzibar
Kama nilivyoeleza hapo awali kuwa kijiji cha Kibokwa kimetajwa kuwa kimoja kati ya vijiji vinavyotarajiwa kujengwa na kuwa vya kisasa kwa Zanzibar. Haya yamebainika katika sherehe maalum za ufunguzi wa jengo la wanakijiji wa Kibokwa “SAEMAUL COMMUNITY HALL”, uliofanywa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Mradi huu wa miaka mitano (2010-2015) ulio chini ya ufadhili wa Serikali ya Korea ya Kusini unalenga kukiendeleza kijiji cha Kibokwa kuwa kijiji cha mfano kwa Zanzibar na hata Tanzania. Matarajio makuu ya mradi huo ni kuwaendeleza wanakijiji kuweza kujiajiri katika sekta mbali mbali na kuongoza kipato chao na hatimaye kuweza kujikwamua na umaskini.
Hivi sasa tayari wanakijiji wameanza kunufaika na mradi huo kwa kujipatia ajira katika maeneo ya kilimo, ufugaji wa kuku na mbuzi, maduka na maktaba, ushoni pamoja na kuwepo ukumbi mkubwa wa mikutano katika kijiji hicho yaani “SAEMAUL COMMUNITY HALL”.
Katika sherehe hizo za ufunguzi Serikali ya Korea kupitia balozi wake nchini Tanzania Jeong Il, kwa mara ya kwanza iliweka bayana kuwa inawezekana kabisa maendeleo ya vijiji kubadilisha mwelekeo wa maendeleo kwa nchi nzima. “Mara nyingi marafiki zangu wa Tanzania wamekuwa wakiniuliza juu ya siri ya mafanikio ya nchi yetu lakini sikuwaambia hata siku moja, sasa leo nataka nikwambieni siri ya mafanikio yetu kuwa ni maendeleo ya vijiji”, alieleza Balozi Jeong Il wa Korea.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akipokea msaada wa nguo kutoka kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Al-Yousuf, Sheikh Al-Youseif, kwa ajili ya wananchi wa kijiji cha Kiuyu Micheweni.
Alifahamisha kuwa katika miaka ya 1960’s, vijiji vya Korea vilikuwa kama vilivyo vijiji vya Tanzania kimaendeleo, lakini sasa viko tofauti sana kwamba vijiji vya Korea vimepata maendeleo makubwa na vimeweza kubadilisha mwelekeo mzima wa maendeleo ya nchi ya Korea. Hii ni kutokana na ukweli kwamba katika mipango yao ya maendeleo waliweka mkazo wa kujenga vijiji vipya na kuviendeleza, mipango ambayo ilifanikiwa kwa asilimia kubwa, hadi kufikia leo Korea inajivunia maendeleo ya kupigiwa mfano.
Kwa mujibu wa Balozi Jeong Il, mantiki ya suala hili ni kwamba maendeleo ya kijiji kimoja huchochea maendeleo ya vijiji vyengine, na ndio maana akaahidi kuwa iwapo kijiji hicho cha Kibokwa kitafanya vizuri atajenga kijiji kama hicho Kisiwani Pemba. Hii ni kusema kwamba kijiji cha Kibokwa kina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa kwa asilimia mia moja ili kuchochea maendeleo ya vijiji vyengine kama ilivyoahidiwa na balozi huyo wa Korea.
Alipopata fursa ya kutoa nasaha zake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alifahamisha kuwa Korea ya Kusini ni rafiki wa kweli, na kwamba Serikali inathamini sana mchango unaotolewa na nchi hiyo kupitia miradi mbali ya maendeleo.
Korea ya Kusini imekuwa miongoni mwa washirika wa karibu katika kukuza maendeleo ya Zanzibar kupitia ufadhili wa miradi kadhaa ya maendeleo ikiwemo ile ya umwagiliaji katika mabonde ya Kibokwa na Bumbwisudi, sambamba na kutoa mashine za kisasa za kulimia “power tillers”.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Affan Othman Maalim akitoa ufafanuzi kuhusiana na miradi inayoendeshwa katika kituo cha wananchi cha Kibokwa, wakati Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alipotembelea na kufungua rasmi kituo hicho.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Affan Othman Maalim alieleza kuwa mchango wa Korea katika sekta ya kilimo umeibua ari ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na kutimiza azma ya serikali ya kuwa na “Mapinduzi ya Kilimo” nchini. Kama hayo hayatoshi, Jumuiya ya Al-Yousuf nayo imejitolea kukijenga upya kijiji cha Kiuyu Micheweni katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Chini ya mpango huo, pamoja na mambo mengine Jumuiya hiyo imejipanga kujenga nyumba mia nne (400) za mkopo nafuu katika kijiji hicho. Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Al-Youseif alidhihirisha hayo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Ofisini kwake Migombani tarehe 28/02/2013, mazungumzo ambayo yalikwenda sambamba na kukabidhi shehena ya nguo za aina mbali mbali za kike kwa kiume kwa ajili ya wakaazi wa Kiuyu Micheweni. Sheikh Al-Youseif alibainisha kuwa mradi huo wa ujenzi wa nyumba pamoja na ule wa kilimo, inalenga kukibadilisha kijiji hicho kuwa cha kisasa na chenye maendeleo.
“Jumuiya yetu imeshawishika kuanzisha miradi hiyo ya maendeleo, baada ya kuona kuwa wananchi wa kijiji hicho wanaishi katika mazingira magumu kuliko vijiji vingi vya Zanzibar”, alifahamisha. Imefahamika kuwa tayari juhudi za ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi huo zimeshaanza kuchukuliwa, sambamba na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ambacho kimebainika kustawi vyema katika eneo hilo.
“Tumefanya uchunguzi tukabaini kuwa ardhi ya Kiuyu ni ya jiwe sehemu ya juu, lakini chini ni nzuri na yenye rutba, na kwamba inakubali kustawisha kilimo cha aina mbali mbali hasa cha mboga mboga”, alifafanua Sheikh Al-Youseif. Katika hatua nyengine kiongozi huyo wa juu wa Jumuiya hiyo inayojishughulisha na utoaji wa misaada ya kibinadamu aliiomba serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kumpatia orodha ya wanafunzi wote wa Kiuyu ili aweze kuwapatia sare za skuli.
Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alisema uamuzi wa kutoa kipaumbele kwa kijiji cha Kiuyu ni sahihi, kwani ni miongoni mwa vijiji vilivyoachwa nyuma kimaendeleo kwa kipindi kirefu. Alieleza kuwa mradi wa kilimo ulioanzishwa katika kijiji hicho utakuwa chachu ya maendeleo, na kuwaomba wakaazi wa eneo hilo kuuenzi na kuuendeleza kwa juhudi zao zote ili uweze kuleta mafanikio.
Ni dhahiri kuwa mafanikio ya miradi hiyo ya vijiji vya Kibokwa ni Kiuyu yataibua hamasa na shauku ya maendeleo kwa vijiji vyengine, sambamba na kuwashawishi washirika wengine wa maendeleo kuweza kusaidia maendeleo ya vijiji vyengine.
Hivyo ni wajibu wa wasimamizi wa miradi hiyo kuisimamia ipasavyo ili kuweza kuleta mafanikio yaliyokusudiwa na kupelekea ujenzi upya wa vijiji vyengine vya Zanzibar, na hatimaye kuweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa maendeleo ya nchi yetu yenye rasilimali za kila aina zikiwemo historia iliyotukuka pamoja na mandhari ya kuvutia. Inawezekana ikiwa kila mmoja atatekeleza wajibu wake ipasavyo.
Chanzo: OMKR
No comments :
Post a Comment