Na Mwinyi Sadallah
28th April 2013
Dk. Ali Mohamed Shein
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar (JUMIKI) hawana ubavu wa kuwaamsha Wazanzibari kwa kuwa wananchi wake wamekwisha amshwa kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964.
Dk. Shein alitoa tamko hilo mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika tawi la CCM Kinuni na kuwahutubia wananchi katika ziara yake ya kukagua uhai wa chama chake visiwani Zanzibar, juzi.
Dk Shein alisema kuzinduka kwa wananchi na kupigania haki zao kasi yake iliongezeka kuanzia mwaka 1957 pale jumuiya mbili za Waafrika na Washiraz zilipoungana na kuzaliwa kwa chama cha Afro Shiraz Party (ASP).
“Uamsho unamuamsha nani, ni nani aliyelala wakati Wazanzibari waliamka kitambo na ilipofika mwaka 1964 wazee wakafanya Mapinduzi ya umma yaliyoongozwa na Mzee Abeid Karume,”alisema Dk Shein.
Alisema watu wanaofanya vitendo vya vurugu ikiwamo uharibifu wa mali na kuchomwa moto kwa matawi na maskani za CCM serikali yake haitawavumilia kwani mikono ya sheria itawakamata.
Alisema nchi nyingi duniani zimesifia muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Tanzania ikiendelea kupata sifa kutokana na kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, kuwapo kwa misingi ya demokrasia na kufuata utawala bora wa sheria.
Dk Shein aliyasema hayo baada ya wananchi kulalamika mbele yake kuwa tawi moja la chama hicho katika eneo la Kununi kuchomwa moto na watu wasiojulikana zikiwamo na maskani kuu za Kisonge na Kachorora mjini Zanzibar.
“Siogopi mtu ila mimi hufanya kazi kwa mujibu wa katiba na sheria, sitomchelea kiongozi yeyote anayevunja sheria za nchi, Zanzibar ni yetu sote, ili tuishi kwa amani ni wajibu wetu kutii sheria zilizopo,”alisema.
Alisema watalii na wageni mbalimbali mashuhuri duniani huitembelea Zanzibar na kuingiza asilimia 80 ya fedha za kigeni kupitia sekta ya utalii na kwamba vitendo vya fujo na vurugu ni sawa na kuwafukuza watalii wakati ndiyo nguzo ya uchumi wa Zanzibar.
Alisema Zanzibar kwa asili yake haina historia ya matukio ya uchomaji moto kwa mali za serikali au watu binafsi na kuwaonya wanaofanya vitendo hivyo watafute kazi za kufanya kwa vile serikali yake imeshaamua kupambana nao kwa gharama yoyote.
Alisema vitendo vya vurugu na ghasia vilivyojitokeza mwaka jana haviwezi kukubalika katika nchi inayoongozwa kwa misingi ya utawala wa sheria na kuwaasa vijana wakatae kutumiwa na wanasiasa waliopoteza mwelekeo kwa kutafuta mafanikio ya kisiasa kwa njia za mkato.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment