Na Zanzibari Yetu
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameonya kuwa Serikali haitavumilia na itawachukulia hatua za kisheria watu watakaobainika kukata miti na kusafirisha miche ya miti ya mikarafuu nje ya nchi kinyume cha sheria.
Maalim Seif alitoa onyo hilo huko Bwagamoyo Mtambwe, mkoa wa Kaskazini Pemba, alipokuwa akizindua kampeni ya upandaji miti Zanzibar.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kukata miti ovyo, ikiwemo mikarafuu na wapo ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kuisafirisha miche ya mikarafuu nje ya nchi, ikiwemo Kenya.
Alisema tabia ya kukata miti kiholela ni hatari kwa mazingira na husababisha athari kubwa kiuchumi, lakini vitendo vya kusafirisha nje ya nchi miche ya mikarafuu linaweza kushusha hadhi ya Zanzibar iliyojijengea kwa miaka mingi kuwa mzalishaji mkuu wa karafuu.
“Ndugu zanguni hapa Pemba na Unguja miongoni mwetu wamo wenye tabia ya kukata miti ovyo, ikiwemo mikarafuu na wapo wanaotumia misumeno ya moto iliyopigwa marufuku, kamwe Serikali haitavumilia jambo hilo, wananchi tusaidieni kuwafichua watu hao”, alionya Maalim Seif.
Alieleza kuwa karafuu ni alama ya Zanzibar, ambayo imeifanya ijuilikane Duniani kote kuwa ni visiwa vya viungo, lakini baada ya watu kuona thamani ya zao hilo ilishuka katika miaka miliyopita walilidharau na kuikata miti hiyo kwa ajili ya kujengea nyumba, kuni na makaa.
Maalim Seif alisema katika karne iliyopita zao la karafuu lilithaminiwa sana na wazee waliliotesha kwa wingi hadi kufikia hatua Zanzibar ikizalisha tani zaidi ya 35, 000 katika msimu mmoja.
Alisema uzalishaji ulishuka kidogo kidogo hadi kufikia tani 2000 katika miaka ya hivi karibuni. Alisema Serikali ya awamu ya saba imeamua kwa dhati kabisa kufufua ari ya uzalishaji wa zao la karafuu, pamoja na mazao mengine mbali mbali, ikiwemo ya viungo, ili kurejesha hadhi ya Zanzibar Duniani.
Hata hivyo, alisema karafuu hivi sasa inatoa mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi Zanzibar na ndio maana imewajengea mazingira mazuri ya bei wakulima wake, pamoja na upatikanaji wa miche ya kupanda.
Wakati huo huo, Makamu wa Kwanza wa Rais aliwataka wananchi katika maeneo yaliyokumbwa na uvamizi wa maji ya bahari katika maeneo ya kilimo kujenga tabia ya kupanda miti ya mikoko, na kuhifadhi mazingira kuepusha athari za uharibifu huo.
Akikagua tuta lilojengwa kuzuia maji ya bahari yasiingie katika mashamba ya mpunga huko Wingwi, Wilaya ya Micheweni, Maalim Seif alisema Zanzibar isipokuwa na tahadhari juu ya mabadiliko ya tabia nchi madhara mabaya ya kiuchumi na kijamii yataendelea kujitokeza.
Alieleza kuwa njia muafaka ya kuiepusha Zanzibar na balaa linalosababishwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi ni kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti, kuepuka kukata miti ovyo, pamoja na kuhifadhi matumbawe baharini.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi, alimueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa, eneo la lililojengwa tuta hilo upande wa baharini awali lilikuwa likitumika kwa kilimo, lakini hivi sasa limekuwa ni sehemu ya bahari.
Alisema hali hiyo ilisababishwa na tabia ya wananchi kukata miti kwa wingi, ikiwemo mikoko kando ya bahari, hivyo maji ya bahari kupanda juu hadi sehemu zinazotumika kwa shughuli za kiuchumi, na kijamii kama vile sehemu za makaburi kuvamiwa na maji ya chumvi.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili, Afan Othman Maalim alisema suala la maji ya bahari kuvamia maeneo ya wananchi wanayoyatumia kwa shughuli za kilimo na kijamii ni kubwa sana, ambapo Zanzibar tayari imeorodhesha maeneo 148 yaliyokwisha kukumbwa na hali hiyo kote Unguja na Pemba.
No comments :
Post a Comment