Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, April 28, 2013

Muungano wa Tanzania ni historia Afrika

NA EDITOR

28th April 2013


Maoniya Katuni
Muungano wa Tanzania, ambao uliasisiwa na Rais wa kwanza wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Rais wa Zanzibar Abeid Aman Karume miaka 49 iliyopita, (wote marehemu), umeweka rekodi ya kuwa Muungano uliodumu kwa muda mrefu zaidi kuliko nchi zozote zilizowahi kuwa na Muungano barani Afrika.

Pamoja na kuwepo kwa kasoro ndogo ndogo ambazo zinalalamikiwa na baadhi ya wananchi, kasoro hizo zinaweza kurekebishwa ili kuuimarisha zaidi Muungano huu.

Sherehe za kuadhimisha miaka 49 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilifanyika kitaifa juzi jijini Dar es Salaam ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Jakaya Kikwete aliongoza mamia ya wananchi waliofurika katika uwanja wa Uhuru kusherehekea sikukuu hiyo ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Aprili 26.

Viongozi wa kitaifa kutoka Serikali zote mbili za Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na viongozi wakiwemo marais wastaafu, walikuwa miongozi mwa walioshiriki kuadhimisha sherehe hizo adhimu.

Watanzania wameaswa kutokubali kuvunja Muungano kwani hiyo ni nguzo ya umoja katika Afrika. Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Beregu alisema wote wanaodhamiria kuuvunja Muungano wana upeo finyu. 

Baregu alisema mafanikio mengi hapa nchini yametokana na Muungano na kwamba hata wakati wa kukusanya maoni ya Katiba mpya, wananchi aliowasikiliza katika kundi lake, ni wachache waliotoa mawazo ya kutoutaka Muungano.

Profesa Baregu, ambaye pia ni mshauri wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema Muungano huu ni wa kipekee kwani kuna nchi nyingi za Afrika zilijaribu kuungana lakini haikuwezekana na baadhi zilijaribu kuwa na Muungano ambao haukudumu kwa muda mrefu.

Alisisitiza kuwa kwa Muungano wa Tanzania, ambao sasa una umri wa miaka 49, kinachotakiwa ni kufanya marekebisho na kasoro zilizopo na kwamba wananchi wengi nchini hivi sasa wanajisikia zaidi kwa Utanzania na si Uzanzibari wala Utanganyika.

Ni dhahiri kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania wenye nguvu ya uzalishaji wamezaliwa ndani ya Muuungano, wamekua na kusoma wakiwa wanasimuliwa historia ya namna waasisi wa Muungano walivyoiweka misingi mizuri na imara ya umoja na undugu baina ya wananchi wa Tanzania bara na wa Tanzania visiwani.

Kizazi hiki ndicho kinachowajibika kuwa na nguvu pamoja na wajibu wa kuimarisha zaidi maelewano ya Watanzania wa pande zote bila kubaguana.

Kama alivyosema Profesa Baregu kuwa wale wachache wenye dhana ya kutaka kuuvunja Muungano inawezekana kuwa na fikra potofu akilini kwa alichosema kuwa haimjengei mtu umaarufu wa aina yoyote kwa kutamka hadharani kuwa Muungano ni kitu kisichokuwa na maana.

Muungano ndio unaotufanya tukaitwa Watanzania, na kutokana na sifa nyingi za amani, utulivu, mshikamano na upendo wa Watanzania ambao unatambulika duniani, sifa na heshima hizo zinatokana zaidi na maelewano yaliyojengeka miongoni mwa Watanzania wote.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholas Mgaya pia anaunga mkono akisema Muungano una manufaa kwa wananchi wote wakiwamo wafanyakazi.

Aanataka yafanyike marekebisho madogo katika kasoro zilizopo ili kujenga umoja zaidi, akibainisha upungufu uliopo katika sheria za kazi na kusema wafanyakazi wa Zanzibar na Tanzania Bara wanatumia sheria mbili tofauti wakati wao ni wamoja.

Anashauri ni vyema sheria zikafanyiwa kazi ili Watanzania wajisikie kuwa ni wamoja kweli kwa kuwa na sheria moja katika nchi moja. Nakiri kuwa mengine yote ndani ya Muungano ni mazuri na yamejenga umoja kwa Watanzania.

Wakati wa kilele cha sherehe hizo jijini Dar es Salaam, baadhi ya wananchi walisema wanafarijika kuona viongozi wote wa Tanzania Bara na Visiwani wapo pamoja wakionesha umoja wa Watanzania huku wananchi wa pande zote wakiwa huru kwenda upande wowote wa Muungano, wakadai hao wanaotaka Muungano uvunjike wana maslahi yao binafsi.

Ni kweli kuwa yapo mapungufu machache katika masuala ya Muungano, na hayo hayana uzito mkubwa wa kuyumbisha Muungano wetu, na kwa vile yanafahamika, inawezekana kabisa yakapatiwa ufumbuzi katika mapendekezo ya Katiba mpya ijayo.

Ni imani yetu kuwa viongozi watayachukulia kwa uzito unaostahili mapungufu yote ya Muungano yanayoonekana kuwakera baadhi ya Watanzania ili nchi yetu iendelee kustawi katika umoja, mshimano na maendeleo kwa Watanzania wote. Mungu ubariki Muungano wa Tanzania na watu wake.  
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment