Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, April 28, 2013

Kikongwe auawa, azikwa kaburi moja na aliyetuhumiwa kumroga

NA EMMANUEL LENGWA

28th April 2013


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman
Kikongwe mmoja ameuawa kwa kupigwa mawe na waombolezaji wenye hasira na kuzikwa kaburi moja na marehemu anayetuhumiwa kumroga.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, alisema kuwa tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi saa 9 alasiri, katika kitongoji cha Maweni, Kijiji cha Mkwajuni wilayani Chunya.

Alimtaja mtu aliyeuawa kwa kupigwa mawe hadi kufa kuwa ni Flovian Mwachuki (70).

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Diwani alisema kuwa, kabla ya tukio hilo, kulikuwa na msiba wa mwananchi mmoja kijijini hapo aliyetambulika kwa jina la Peter Robert (28).

Kamanda Diwani alisema kuwa wananchi kijijini hapo walimtuhumu Floviana kuwa ndiye mchawi aliyemroga Peter na kusababisha kifo chake kwa imani za kishirikina.

Alisema kuwa wakati waombolezaji wakiwa makaburini kwa ajili ya kumzika Peter, walimuona Floviana akienda kuhudhuria mazishi hayo, ndipo wananchi hao walipoghadhibika kwa kujichukulia sheria mkononi na kumkamata, kumpiga mawe na  kumuua papo hapo.

Alisema baada ya kumuua waliuchukua mwili wake na kuuweka kwenye kaburi moja na marehemu Peter, kisha kuwafukia wote ndani ya kaburi hilo.

Kwa mujibu wa Kamanda Diwani, Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali wa kuwapata waliohusika na tukio hilo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Aliwaomba wananchi wenye taarifa za walipo waliohusika wa mauaji hayo kuzifikisha Polisi haraka ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Kamanda Diwani alitoa wito na kuwaasa wananchi kuacha tabia ya kuamini mambo ya kishirikina na uchawi kwa kuwa hayana faida kwao bali huchochea migogoro katika jamii. 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment